LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 19, 2021

RAIS SAMIA: NCHI IPO IMARA, TUMEJIPANGA VIZURI KUENDELEZA ALIPOISHIA DK. MAGUFULI KATIKA KUTEKELEZA MAONO YAKE KWA TANZANIA

Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihutubia Taifa baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania.


Na Bashir Nkoromo, Dar es Salaam

Rais Samia Suluhu Hassan amewaomba Watanzania kushikamana, kuwa na moyo wa subira na  kujenga umoja katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao Hayati, Dk. John Magufuli na amewahakikishia Wananchi kuwa nchi iko imara na kuwa yeye na viongozi wenzake wamejipanga vizuri kuendeleza pale Dk. Magufuli alipoishia katika maono yake na kwamba hakuna jambo litakaloharibika.


“Nawaomba Watanzania tuwe na moyo wa subira, tujenge umoja na mshikamo katika kipindi hiki kigumu, niwahakikishie kuwa tuko imara na sisi viongozi tumejipanga vizuri kuendeleza pale mwenzetu alipoishia hakuna jambo litakaloharibika”, Rais Samia  alisema wakati akilihutubia taifa baada ya kuapishwa kuwa Rais, leo Ikulu jijini Dar es Salaam, amesema, 


Rais Samia katika kipindi cha Uongozi wake Hayati Dk. Magufuli aliweza kuibadili taswira ya Tanzania kutokana na  maono yake na kwa kumtegemea Mungu katika mipango na mikakati ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa nchini.


Amesema wakati akifanya naye kazi Dk. Magufuli alikuwa mwalimu asiyechoka kuelekeza na kwamba kutokana na kufanyanaye kazi aliweza kujifunza mengi ambayo yataendelea kuwa hazina katika utendaji kazi wake siku zote akiongeza kuwa katika kipindi chote alichofanya kazi na  Hayati Dk. Magufuli alikuwa akimuelekeza kwa vitendo namna anavyotaka nchi iende, nini kifanyike na alimfundisha mengi, kumlea vya kutosha.


Rais Samia kuondokewa na Dk. Magufuli taifa limepoteza kiongozi shupavu na mzalendo aliyeipenda nchi yake na kujali watu wake katika kutekeleza mapinduzi makubwa ya uchumi wa wananchi wa Tanzania.

“Tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa Bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli, Magufuli alikuwa chachu ya maendeleo kwa nchi yetu”,  amesema Samia. 


Akitangaza  ratiba ya kumuaga amesema kuwa  Hayati, Rais Magufuli ataanza kuagwa Machi 20 ambapo Ibada ya kumuombea itafanyika katika kanisa la Mtakatifu Peter Oysterbay  na baadaye mwili utapelekwa katika Uwanja wa Uhuru kwa viongozi kuuaga. Machi 21 Wakazi wa Dar es Salaam watapata nafasi ya kumuaga mpendwa wao katika Uwanja wa Uhuru, Machi 22  Wakazi wa Dodoma watamuaga,  Machi 23 wakazi wa  Mwanza watapata nafasi ya kumuaga mpendwa wao na  Machi 24 Hayati Rais Magufuli ataagwa Mjini Chato ambapo Machi 25, 2021 atazikwa nyumbani kwake Chato.



Rais Samia ametoa rambirambi kwa familia ya  mjane wa Hayati, Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli, watoto, ndugu na jamaa kwa  kuondokewa na mpendwa wao na  taifa linaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha msiba mzito na amewataka wawe na subira.



Pia ametoa rambirambi za pole kwa Watanzania wote kwa kuondokewa na kipenzi chao, Hayati, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwani Watanzania hawakutarajia jambo hilo.


“Natoa rambirambi kwa wananchi wote wa Tanzania kwa pigo hili kubwa,  ni msiba mzito ambao hatukutarajia, sote tunafahamu jinsi Rais Magufuli alivyoipenda nchi, alivyowapenda Watanzania na kujitoa kwa watu wake kwa dhamira ya dhati na nia njema ya kuibadilisha tasirwa ya nchi yake”, Rais Samia.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages