Maalim Seif Sharif Hamad
Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki Dunia, jijini Dar es Salaam.
Akitangaza kifo hicho, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi amesema, Maalif Seif amefariki leo saa 5 asubuhu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa tangu tarehe 9 mwezi huu akipatiwa matibabu.
Kufuatia kifo hicho Rais Dk. Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo, akisema pia kwamba taratibu za mazishi zitaendelea kutolewa na Serikali kwa ushirikiano wa ndugu wa marehemu na Chama cha ACT Wazalendo.
Maalim Seif pamoja na kuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo pia alifanikiwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar baada ya kugombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Tazama Video Rais Dk. Mwinyi akilitangazia Taifa msiba huo.👇
Kufuatia kifo hicho Rais Dk. John Magufuli ameelezea kushtushwa na kuandika katika mtandao wa Twitter akisema; 👇
Historia fupi ya Maalim Seif Sharif Hamad
Maisha
Maalim Seif Shariff Hamad alizaliwa eneo la Nyali, Mtambwe Kisiwani Pemba, Oktoba 22, 1943
Alipata elimu yake ya msingi katika skuli ya msingi Uondwe, 1950 na baadaye alijiunga na elimu ya sekondari katika skuli ya watoto wa kiume Wete Pemba 1952.
Baadaye aliendelea na elimu ya sekondari katika skuli ya King George na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1963 ambapo baadaye kati ya mwaka 1972 na 1975 alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa (Political Science).
Kazi
Kati ya mwaka 1972 na 1975 alifundisha katika skuli mbalimbali za Unguja na Pemba, zikiwemo Fidel Castro na Lumumba.
Siasa
Baadaye Maalim Seif alianza kuingia katika masuala ya siasa, ambapo mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Mwaka 1977 hadi 1987, alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya chama hicho.
Mwaka 1982 hadi 1987 alikuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya Chama cha Mapinduzi na 1984 aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi mwaka 1988.
Baada hapo, misukosuko mikubwa ya kisiasa ilianza kumkumba ambapo Januari 1988 alipoteza nafasi ya Uwaziri Kiongozi na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi baada ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Idrisa Abdulwakil kutangaza kulivunja Baraza la Mawaziri.
Kujiengua CCM
Maalim Seif alitoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) mnamo mwezi Mei 1988
Mwaka 1992, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama cha Civic United Front (CUF) na kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho kwa mda mrefu hadi alipoondoka katika chama hicho na kuhamia ACT- Wazalendo mwaka 2019.
Maamuzi ya Maalim Seif kutangza kuhamia ACT- Wazalendo Machi 28, 2019 yalifanyika muda mchache baada ya kesi iliyokuwa Mahakamani kuishia kwa Profesa Ibrahim Lipumba kutsmbuliwa kuwa ndiye Mwenyekiti halali wa CUF.
Akiwa ACT, Maali Seif alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, nafasi aliyopewa kando ya Kiongozi wa Kitaifa wa chama hicho Zitto Kabwe.
Akiwa na kofia hiyo ya Mwenyekiti wa chama hicho, aligombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Hatua hiyo ya kugombea Urais wa Zanzibar kupitia ACT Wazalendo ndiyo hatua iliyomwezesha kuwa Makamu wa kwanza wa Rais kufuatia Chama hicho kuwa cha pili kwa wingi wa kura baada ya CCM iliyoshinda kiti cha Urais wa Zanzibar.
Ina Lilah waina Ilayhi Rajiuun
Imetayarishwa na Bashir Nkoromo, Msimamizi Mkuu wa Blog hii ya Taifa ya CCM.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇