LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 20, 2021

KIPANGA APIGA MARUFUKU FEDHA ZA MIRADI YA UJENZI KUTUMIKA KULIPA POSHO

 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhandisi Mkuu wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Butiama.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga akifafanua jambo wakati alipotembelea kukagua Mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Butiama.

Mkuu wa Chuo cha VETA Mara ambaye ndiye Msimamizi mkuu wa Mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Butiama, Vedasto Rutahakana, akisoma taarifa ya ujenzi mbele ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga.

 

Muonekano wa mojawapo ya majengo yanayojengwa katika Chuo cha VETA Butiama.



• Aagiza milioni 75 zirudishwe mara moja


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga amepiga marufuku fedha za miradi ya ujenzi wa Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutumika kulipa posho kwa wasimamizi wa miradi hiyo.


Mhe. Kipanga ameyasema hayo Februari 18, 2021 Wilayani Butiama Mkoani Mara wakati alipotembelea kukagua Mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Butiama ambapo hakuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa huku fedha nyingine kiasi cha milioni 75 zikiwa zimetumika kulipa posho watu mbalimbali.


“Hizo pesa zaidi ya milioni 75 mlizolipana posho zirudishwe mara moja kwa kuwa lengo la pesa hizo halikuwa kulipa posho bali kufanyia ujenzi na kuanzia leo ni marufuku pesa za miradi ya ujenzi kutumika kulipana posho,” amesisitiza Mhe. Kipanga.


Katika hatua nyingine, Mhe. Kipanga amevunja Kamati za Ujenzi na Mapokezi na kuwasimamisha Msimamizi mkuu wa Mradi huo, Vedasto Rutahakana ambaye ni Mkuu wa Chuo cha VETA Mara na Afisa Manunuzi, Mwesiga Tebuka kutokana na kushindwa kusimamia vizuri Mradi huo na amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Pancras Bujulu kuhakikisha anaweka wasimamizi wengine mara moja ili ujenzi ukamilike kwa wakati uliopangwa.


Aidha, Naibu Waziri Kipanga amewaomba Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkurugenzi wa Halmashauri, Mbunge na Mkuu wa Wilaya ya Butiama na Wilaya nyingine ambapo vinajengwa vyuo vya VETA kushirikiana na wasimamizi wa mIradi hiyo ili kuhakikisha ifikapo Machi 31 mwaka huu ujenzi unakamilika.


Akiongea katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi amesema wamefurahishwa sana na ujenzi wa chuo hicho katika wilaya yao na ameomba chuo hicho kitoe mafunzo ya madini na ufugaji kwa kuwa ndio shughuli kuu za kijamii zilizopo katika wilaya hiyo.


“Kwa kweli tumefurahia sana chuo hiki kujengwa wilayani kwetu ila niombe kitoe mafunzo yanayoendana na shughuli za kijamii za eneo hili ikiwemo madini na ufugaji,” amesema Nyamubi.


Katika ziara hiyo, Mhe. Kipanga pia alitembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) cha Wilaya ya Musoma na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya ambayo ni bweni moja, jiko, karakana nne na jengo la Utawala.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages