Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akizungumza na wataalamu wanaotengeneza programu rununu ya NAPA (hawapo pichani) mjini Morogoro. Anayesikiliza ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekeleza
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza akiwasilisha taarifa kuhusu utengenezaji wa programu rununu ya NAPA kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula (anayesikiliza) wakiwa mjini Morogoro ambapo wataalamu wanaotengeneza programu hiyo hawapo pichani
Mhandisi Jampyon Mbugi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akieleza utendaji kazi wa programu rununu ya NAPA kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula (anayesikiliza) na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekweleza (aliyeketi katikati) wakiwa Morogoro kwenye kazi ya utengenezaji wa programu hiyo
Wataalamu wanaotengeneza programu rununu ya NAPA wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula (hayupo pichani) wakati wa kikao chao mjini Morogoro cha kutengeneza programu hiyo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula (aliyeketi mbele katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu wanaotengeneza programu rununu ya NAPA mjini Morogoro. Aliyeketi kulia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekweleza.
**********************************
Na Prisca Ulomi, WMTH
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula amekutana wa wataalamu wa TEHAMA wanaotengeneza Programu Rununu ya Anwani za Makazi na Postikodi (National Addressing and Postcode Mobile Application – NAPA) mjini Morogoro ili kukagua ujenzi wa programu hiyo unaotekelezwa na wataalamu hao
Dkt. Chaula amesema kuwa malengo ya Wizara ya kutengeneza programu rununu ya NAPA ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mfumo wa TEHAMA wa utambuzi wa maeneo ya makazi ya watu na kukusanya taarifa ili kuwezesha utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii nchini
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekweleza amesema kuwa programu rununu ya NAPA itakuwa na faida mbali mbali ikiwemo kusajili na kuhuisha anwani za makazi; kumwezesha mtumiaji kutambua mwelekeo wa anwani kwa kutumia ramani; kutambua mitaa/vitongoji vyote vyenye anwani za makazi; kumwezesha mtumiaji kutambua mwelekeo wa anuani kwa kutumia ramani; kutambua anuani za makazi kwa kutumia namba za TIN za TRA na za NIDA; kutambua maeneo yote ya huduma za kijamii na kiuchumi kama vile benki, polisi, ofisi za Serikali; kumwezesha mtumiaji kutambua umbali wa anuani kwa kutumia ramani; kumwezesha mwananchi kupata msaada wa huduma za dharura kwa urahisi na uharaka; na kuwezesha posta kuwafikia wateja wa huduma za posta kiganjani
Akiwasilisha taarifa ya utengenezaji wa programu hiyo kwa Dkt. Chaula kwa niaba ya wataalamu wengine, Mhandisi Jampyon Mbugi wa Wizara hiyo amesema kuwa ili kufanikisha utengenezaji wa programu rununu ya NAPA wataalamu wa TEHAMA wamekusanya mahitaji ya programu hiyo; usanifu wa mfumo; uundaji wa mfumo; majaribio ya mfumo; majaribio ya kukubali kwa mfumo huo kabla ya kufanya uzinduzi wa mfumo huo ambapo kazi hiyo imeanza kufanyika tarehe 12 Januari mwaka huu na utakamilika tarehe 28 Februari mwaka huu ili uanze kutumika
Naye Mhandisi Richard Magubila wa Wizara hiyo amesema kuwa programu rununu ya NAPA itaunganishwa na mifumo mingine ya TEHAMA ya Serikali kama vile ya kodi, ukusanyaji wa mapato, afya, biashara mtandao, ardhi, vitambulisho vya taifa na mifumo mingine ili kuwezesha kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kuendana na mahitaji, mabadiliko na ukuaji wa TEHAMA nchini
Wataalamu wanaohusika kuandaa programu rununu ya NAPA ni wataalamu wa ndani ya nchi yetu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Wizara ya Fedha na Mipango; Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee, Watoto na Ustawi wa Jamii; Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Shirika la Posta Tanzania; Wakala wa Serikali Mtandao; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Chuo Kikuu cha Dodoma; Chuo Kikuu cha Ardhi; na wataalamu wa TEHAMA wa taasisi za sekta binafsi
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇