Tume ya uchaguzi nchini Uganda, leo Jumamosi, Januari 16, 2021 imemtangaza rasmi Yoweri Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa juzi Alkhamisi, Januari 14. Mashirika ya habari ya ndani na nje ya Uganda yameitangaza kwa wingi habari hiyo na kusisitiza kuwa, zoezi la kuhesabu kura limemalizika leo kabla ya kutangazwa ushindi wa Museveni.
Kwa ushindi huo, Museveni (76) amepewa miaka mitano mingine ya kuendelea kuiongoza Uganda katika utawala wake wa miaka 35 sasa huku wapinzani wakilalamikia uchakachuaji mkubwa wa kura na kuwataka wananchi wakatae matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi.
Museveni ameshinda kwa kura milioni 5.85 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote wakati mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wite amepata kura milioni 3.48 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote, imesema taarifa ya tume ya uchaguzi ya Uganda iliyotangazwa leo kwa njia ya televisheni.
Bobi Wite 38, ana uungaji mkono mkubwa wa vijana nchini Uganda kutokana na kwamba ni mwanamuziki na mwito wake wa mabadiliko nchini humo na kuwahamasisha waendeshe mapambano dhidi ya kile alichokiita ni utawala wa kidikteta na ubadhirifu ulioenea kila sehemu nchini humo.
Mgombea huyo kijana jana Ijumaa aliwaambia waandishi wa habari kwamba, ana mkanda wa video unaoonesha uchakachuaji mkubwa wa kura uliofanywa na serikali ya Rais Museveni. Serikali ya Uganda ilifunga Intaneti siku moja kabla ya uchaguzi na kukata umeme sehemu nyingi hadi wakati tunaandika habari hii.
Vikosi vya usalama na polisi vimetanda kila mahali. Leo Jumamosi vikosi hivyo vimefunga utepe wa usalama wa kuizingira nyumba ya Bobi Wine huko Magere katika wilaya ya Wakiso, jijini Kampala na kuwaambia waandishi wa habari wa kigeni kwamba hawana ruhusa ya kuingia katika eneo hilo .
Jana mgombea huyo kijana ambaye anaonekana kuwa na uungaji mkono pia mashinani aliwaambia waandishi wa habari kwamba, mapambano ndio kwanza yameanza na hayana ishara ya kumalizika leo na kesho.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇