LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 30, 2021

MKUU WA MKOA WA RUVUMA MNDEME AAGIZA WATENDAJI KUSIMAMIA UTUNZAJI VYANZO VYA MAJI

Na Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewaagiza maafisa Tarafa na viongozi wote ngazi ya Wilaya kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili viwe endelevu.


Mndeme ametoa agizo hilo wakati anafungua mkutano wa wadau wa sekta ya maji mkoani Ruvuma uliofanyika leo katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuagiza wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji kuondolewa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ya sheria ya RUWASA ya mwaka 2019.


Maagizo mengine yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa katika mkutano huo ni Halmashauri zote na sekretarieti ya Mkoa kuwajibika kikamilifu katika kutekeleza na kusimamia majukumu yote yaliyoorodheshwa kwenye sheria namba tano ya huduma ya maji ya mwaka 2019.


“Mameneja wa RUWASA Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri zote zihakikishe kwamba miradi iliyopo na mingine itakayojengwa inaunda vyombo huru vya watumiaji maji kwa sheria namba tano ya mwaka 2019 kabla au ifikapo Mei 31,2021’’,amesisitiza Mndeme.


Mndeme pia ameagiza katika mkutano huo wa Baraza la madiwani wa kila robo kuwa katika Halmashauri zote iwepo mada ya kudumu ambapo Mameneja wa RUWASA katika wilaya husika watatoa taarifa kuhusu hali ya upatikanaji na usajili wa vyombo vya watumiaji maji huku akiagiza pia  RUWASA Wilaya na Mkoa  zishirikiane na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira SOUWASA sanjari na ofisi za mabonde ya maji katika kutafuta vyanzo vya maji na kuandaa mipango ya utunzaji wa vyanzo vya maji.


“Naagiza fedha zitokanazo na mauzo ya maji zikaguliwe na mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ili kujiridhisha namna fedha hizo zilivyotumika,endeleeni kuwachukulia hatua wanaoharibu kwa makusudi miundombinu ya maji na vyanzo vya maji’’,alisema Mndeme.


Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga ameyataja majukumu ya RUWASA kuwa ni kuandaa mipango ya kusanifu miradi,kujenga na kusimamia uendeshaji wake.


Majukumu mengine ni kuendeleza vyanzo vya maji kwa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi,kuchimba visima na kujenga mabwawa sanjari na kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu ya maji.

HABARI PICHA

 Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizungumza wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya maji mkoani humo, uliofanyika leo katika ukumbi wa Manispaa ya Songea 
Baadhi ya wadau wa maji mkoani Ruvuma wakimsikiliza mkuu huyo wa mkoa wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea, leo.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga akitoa mada ya majukumu  ya RUWASA kwenye mkutano huo. (Picha zote na
 Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages