Minja akifafanua jambo alipokuwa akijibu maswali ya wanahabari.
Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), iliyopo Barabara ya Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Na Richard Mwaikenda, Dodoma.
WASTANI wa Mfumuko wa Bei wa Taifa kutoka mwezi
Januari hadi Desemba, 2020 umepungua hadi asilimia 3.3 mwaka 2020 kutoka
asilimia 3.4 mwaka 2019.
Wastani wa
Mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula umeongezeka hadi asilimia 5.0 mwaka 2020
kutoka asilimia 4.3 mwaka 2019. Kwa upande mwingine, wastani wa Mfumuko wa Bei
wa bidhaa zisizo za vyakula kwa mwaka 2020 umepungua hadi asilimia 2.8 kutoka
asilimia 4.0 mwaka 2019.
Takwimu hizo zimetolewa na Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS),
Minja amesema kuwa wastani wa Mfumuko wa Bei ambao
haujumuishi vyakula na nishati umepungua hadi asilimia 2.3 mwaka 2020 kutoka
asilimia 3.0 mwaka 2019.
“Mfumuko wa Bei wa
Taifa kwa kipimo cha mwaka unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za
bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi,”amefafanua.
Aidha, Minja amesema mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi
Desemba, 2020 umeongezeka hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka
ulioishia mwezi Novemba, 2020.
“Hii inamaanisha kuwa,
kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi
Desemba, 2020 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka
ulioishia mwezi Novemba, 2020. Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 120.79 mwezi
Desemba, 2020 kutoka 117.10 mwezi Desemba, 2019,”amesema Minja.
Akiangazia upande wa nchi za Afrika Mashariki, alibainisha kuwa nchini Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Desemba, 2020 umeongezeka hadi asilimia 5.62 kutoka asilimia 5.33 kwa mwaka ulioishia Novemba 2020. Kwa upande wa Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Desemba , 2020 umepungua hadi asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia Novemba,2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇