Mbunge wa Jimbo la Chemba Mh Mohammed Lujuo Moni akijadiliana jambo na Mhandisi wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salome Kabunda walipotembelea eneo lililoharibiwa vibaya na maji katika barabara inayoziunganisha Wilaya za Chemba na Kiteto.
Mh Mbunge wa Jimbo la Chemba Mh Mohammed Lujuo Moni Tarehe 14 Januari 2021 alifanya ziara Jimboni Chemba ambapo alitembelea Kata ya Mrijo.
Mh Mbunge akiongozana na Kaimu Mhandisi wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salome Kabunda kwa pamoja waliweza kufika eneo lililoharibiwa vibaya na Maji katika Barabara inayoziunganisha Wilaya za Chemba na Kiteto na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano baina ya maeneo hayo na hata magari kushindwa kupita.
Wakiwa eneo la tukio Mhandisi Salome Kabunda aliwaeleza wananchi kuwa baada Mh Mbunge kuripoti hali hiyo hivi karibuni tayari wao kama TANROADS wameshaweka mkakati wa upatikanaji wa fedha za dharura kufanya marekebisho hayo ambapo mpango huo ni kupata Sh milioni 160 ili ziweze kusaidia kujenga kivuko cha muda huku Barabara hiyo ikiwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Pamoja na mpango huo pia Mhandisi Salome na Mh Mbunge wakiwa eneo hilo waliweza kuweka maazimio ya pamoja kuhakikisha kuwa wakati unasubiriwa mkakati wa ujenzi wa kivuko,. kuwa ni muhimu kijengwe kivuko cha dharura ili kwa sasa shughuli ziweze kuendelea kama kawaida na hapo maazimio yakawa kuanzia Jumatatu ya Tarehe 18 Januari 2021 Timu kutoka TANROADS Mkoa wa Dodoma wafike eneo hilo kujenga kivuko hicho cha dharura.
Kwa niaba ya wananchi wote Mh Mbunge alimshukuru Mhandisi Salome kwa kukubali kufika eneo hilo na hata kuchukua hatua za haraka kurejesha mawasiliano ya wananchi hao na shughuli kuendelea.
Pia Mh Mbunge aliwaeleza wananchi kuwa anaendelea na juhudi za kuhakikisha miundombinu yote iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea irejee katika hali ya awali na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa na imani naye na kuonesha ushirikiano.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇