Mashimo yakichimbwa kwa ajili ya kujengwa tanki eneo la Bwigiri. Waliopewa kazi ya ujenzi huo ni Kampuni ya Suma JKT.
Naibu Katiu Mkuu, Kemikimba akipata maelezo kuhusu eneo patakapotandazwa bomba litakalotoa maji tanki la Bwigiri kusambaza maji Hospitali ya Uhuru, Chamwino.
Kemikimba (kulia) akitoa maagizo kwa mafundi wa Duwasa kuhakikisha wanamaliza kuchimba kisima kipya kwa siku tatu eneo la Ihumwa.
Mabomba yatakayotumika kwenye kisima hicho.
Ramani eneo kilipo kisima hicho
Baadhi ya watumishi wa Duwasa wakinawa kwa kutumia maji ya kisima cha mwaka 1989 kilichofufuliwa na Duwasa eneo la Nzuguni.
Na Richard Mwaikenda, Dodoma.
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba ameridhishwa na ubunifu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Dodoma (DUWASA), wa kufufua visima vya maji vilivyojengwa zamani na kukosa usimamizi.
Alitoa pongezi hizo baada ya kukagua uchimbaji wa visima vipya na ufufuaji wa visima vya zamani katika maeneo ya Ihumwa na Nzuguni na jijini Dodoma.
Licha ya pongezi hizo, Kemikima aliitaka Duwasa kuongeza kasi ya kukamilisha ufufuaji na uchimbaji wa visima hivyo kwa muda uliopangwa ili wananchi wa Dodoma wapate nafuu na kuondokana na adha wanayopata upungufu wa maji.
“Nimefurahi sana kwa jitihada zenu, huo ni ubunifu mzuri, tangu mwanzo nimesema kabisa, changamoto huleta maarifa, na hayo mliyofanya ni maarifa, kufufua visima vya zamani vilivyokosa usimamizi, na endapo visima vyote vikifufuliwa itasaidia kupunguza adha ya upungufu wa maji katika jiji la Dodoma,” alisema Kemikimba.
Akielezea kuhusu kisima kilichojengwa mwaka 1989 na kufuliwa na Duwasa eneo la Nzuguni, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Joseph Aron amesema kuwa majaribio yameonesha kitakuwa na uwezo wa kutoa lita za maji 8000 kwa saa na kwamba vipimo vimeonesha maji hayo ni mazuri na salama kwa matumizi ya watu.
Aidha, amesema kuwa hadi sasa Duwasa ipo kwenye piilikapilika ya kuchimba visima vipya na kufufua visima 11 ambapo vikikamilika, maji yake yataunganishwa kwenye mabomba makubwa huku mengine yakitunzwa kwenye matanki ili kupunguza gharama ya kuyapampu.
Awali, Kemikimba katika ziara yake aliyoongozana na viongozi wa Duwasa, alikagua ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhia lita mil. 2.5 za maji eneo la Bwigiri yatakayo sambazwa Hospitali ya Uhuru, Ikulu ya Chamwino na maeneo ya jirani. Ujenzi huo unaofanywa na Suma JKT gharama yake ni Sh. Mil. 998.
Baada ya hapo alikwenda eneo la Hospitali ya Uhuru, Chamwino kuona eneo ambalo bomba la kupokelea maji kutoka tanki la Bwigiri litatandazwa kwa ajili ya kutumika katika hospitali hiyo. Pia alikagua uchimbaji wa kisima kipya eneo la Ihumwa na kumpa mkandarasi siku tatu kumaliza kuchimba kisima hicho.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇