Na Richard Mwaikenda, CCM Blog, Dodoma.
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Dodoma
(DUWASA), imefufua kisima cha maji kilichojengwa mwaka 1989 eneo la Nzuguni, jijini
Dodoma.
Akielezea kuhusu kisima hicho mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Duwasa, Joseph Aron
alisema kuwa matokeo ya majaribio ya kisima hicho, yameonesha kitakuwa kina uwezo wa kutoa lita 8000 kwa
saa na kwa siku lita 192,000.
Aron, alisema kuwa Duwasa imeamua kufufua visima vya zamani 11
vilivyotelekezwa na kukosa usimamizi mzuri, ili kuongeza kiwango cha
upatikanaji wa maji katika jiji la Dodoma kupunguza adha ya upungufu wa maji
wanayopata wakazi wa jiji hilo ambalo kila siku idadi ya watu inaongezeka.
Aidha,
Aron alimweleza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Kemikimba kuwa maji ya
visima vilivyochimbwa na kufufuliwa yataingizwa kwenye mabomba makubwa kwa
ajili ya kusambazwa kirahisi katika makazi ya jiji hilo.
Baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Nadhifa Kemikimba kufika katika eneo hilo alishangaa kuona maji ya kisima hicho
yakitoka kwa wingi, huku yakimwagika kutoka kwenye ndoo walizokinga, ambapo aliwaambia
maafisa wa Duwasa kuwaita wakazi wa eneo hilo kwenda kuteka maji hayo, lakini
alijibiwa kuwa waliruhusiwa kuyateka na wote wana maji ya kutosha majumbani.
Kemikimba
baada ya kuelezwa na wataalamu wa Duwasa kuwa kisima hicho kilichokuwa kwenye
majaribio, maji yake wameyapima na kujiridhisha kuwa yana ubora na yako salama
kwa matumizi ya watu, aliamua kuteka kwa kutumia kiganja na kuyaonja.
Pia, alikagua kibanda cha mota na pumpu ambapo pia aliona jiwe la msingi la linaloonesha kisima hicho kilizinduliwa mwaka 1989 na alaliyekuwa Mkuu wa Wilaya Dodoma wakati huo.
Kemikimba
akizungumza na wanahabari, watumishi wa Duwasa na baadhi ya wakazi wa Nzuguni
waliokuwepo eneo hilo, alisema ameridhishwa na ubunifu wa Menejimenti ya Duwasa
wa kufufua visima vya maji vilivyojengwa zamani vilivyotelekezwa na kukosa
usimamizi mzuri.
“Nimefurahi
sana kwa jitihada zenu, huo ni ubunifu mzuri, tangu mwanzo nimesema kabisa,
changamoto huleta maarifa, na hayo mliyofanya ni maarifa, kufufua visima vya
zamani vilivyokosa usimamizi, na endapo visima vyote vikifufuliwa
itasaidia kupunguza adha ya upungufu wa maji katika jiji la Dodoma,”
alisema Katibu Mkuu Kemikimba.
Licha ya
pongezi hizo, Kemikimba aliitaka Duwasa kuongeza kasi ya kukamilisha ufufuaji
na uchimbaji wa visima hivyo kwa muda uliopangwa ili wananchi wa Dodoma wapate
nafuu na kuondokana na adha wanayopata ya upungufu wa maji.
Baadhi ya
wakazi wa Nzuguni waliozungmza na mwandishi wa habari hii, hawakusita kuonesha
furaha yao na kwa nyakati tofauti kila mmoja alieleza kuwa kufufuliwa kwa
kisima hicho utakuwa ni ukombozi kwao, kwani sasa wataondokana na adha ya
kuhangaika kutafuta maji.
Doris Sumisumi, aliishukuru serikali kwa kuwakumbuka kufufua kisima hicho kitakachowa saidia kupata kirahisi maji safi na salama.
Kabla ya kukagua kisima hicho na kujiridhisha, Kemikimba awali katika ziara yake alikagua uchimbaji wa kisima kipya eneo la Ihumwa ambapo aliwapa siku tatu kumaliza kuchimba, alikagua ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhia maji eneo la Bwigiri ambapo pia alikwenda Hospitali ya Uhuru Chamwino kuangalia eneo patakapotandazwa bomba litakalokuwa linatoa maji tanki la Bwigiri kusambaza katika hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇