LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 7, 2020

TUNDU LISSU ANANDAA VIKOSI VYA UJASUSI VYA UINGEREZA NA MAREKANI TENA?

 


NA JOHN DANIEL

KWANZA niombe radhi kwa wasomaji wa safu hii kwa kuwakosesha haki yao ya msingi baada ya kukosekana wiki iliyopita. Kukosekana uko kulitokana na sababu zisizozuilika.

 

Mara ya mwisho Jicho la Demokrasia ilimulika kwa sehemu, umuhimu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kuangalia kwa jicho la huruma sekta binafsi kama alivyoahidi mwenyewe wakati akizindua Bunge la 12 mjini Dodoma mwezi uliopita.

 

Nilitumia mifano kadhaa kujenga hoja kuhusu umuhimu wa kiongozi huyo mkuu wa nchi kuangalia upya sekta hiyo bila kuingia kwa undani kuhusu madai ya sekta binafsi kwa serikali, jambo iliyozua malalamiko na minong’ono mengi ya chini kwa chini.

 

Baadhi ya sekta binafsi walifikia hatua ya kupunguza wafanyakazi, wengine wameshindwa kuwalipa mishahara na haki zao za msingi wafanyakazi kwa madai mbalimbali ikiwemo serikali kutolipa madeni yao ya muda mrefu hadi sasa huku matumaini ya kulipwa ikizidi kutoweka, kukosekana kwa kazi hususan zabuni na mengine mengi.

 

Nilihitimisha kwa kuweka wazi kwamba watakapopata fursa hiyo ya kukutana na mkuu wa nchi wataweka wazi kila kitu na kwa jinsi ninavyomfahamu Rais Magufuli mwarobaini itapatikana siku hiyo.

 

Leo Jicho linalumuka japo kwa sehemu ndogo safari ya aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Tundu Lissu, kurejea nchini Ubelgiji Novemba 10, 2020 takriban wiki moja tu baada ya kupigwa mwereka katika sanduku la kura Oktoba 28.

 

Lissu alitaja sababu kubwa tatu zilizomfanya kufikia hatua hiyo ya kurejea Ubelgji kuwa ni kuhofia usalama wake,  kujipanga upya kisiasa na kueleza hali halisi ya Tanzania kwa watu wake na kuomba msaada.

 

Ieleweke kwamba taifa la Ubelgiji si rafiki wa kweli kwa bara zima la Afrika. Nchi hiyo ina historia hasi na maendeleo ya nchi za Afrika kwa ujumla na hasa zile zenye rasilimali muhimu kama Tanzania na hii ni kutokana na kilichotokea nchini Congo mwaka 1961.

Ubelgiji ndiyo iliyotuhumiwa kumuua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo mpigania uhuru, komrade Patrice Lumumba, huku majasusi wa Uingereza na Marekani wakidaiwa kutoa msaada kufanikisha unyama huo baada ya kiongozi huyo kuonyesha uzalendo kwa nchi yake na kukataa kushiriki ulaghai na ulafi wa kibeberu kutaka kuvuna rasilimali kwa mbinu mbalimbali.

 

Lumumba aliyekuwa waziri mkuu wa Kongo baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Ubeljiji mwaka 1960 aliuwawa Januari 17 mwaka 1961 katika mazingira ya kutatanisha huku jino lake likidaiwa kuchukuliwa na kiongozi mmoja wa polisi wa Ubeljiji aliyekuwa anasaidia mauaji yake.

 

Kuuawa kwa Lumumba kulizua malalamiko na mvutano ya miaka mingi na baadaye Ofisa huyo wa Polisi alidai kuwa mwili wa Lumumba uliunguzwa kwa kutumia tindikali maalum.

Hata hivyo mwaka 2002 nchi hiyo ilikubali yaishe na kuomba radhi baada ya kubanwa kila kona na baadaye mahakama moja ya nchi hiyo iliridhia jino la Lumumba lililoko nchini umo lirudishwe kwao.

   

Uamuzi huo wa mahakama ya Ubeljiji ulisababisha Waziri wa Haki za Binadamu wa Kongo, André Lite, kuweka wazi kuwa kurejeshwa kwa mabaki hayo ya Lumumba ingelifanya taifa hilo kuandaa mazishi ya kitaifa kwa shujaa wao ikiwa na heshima zote za kiongozi wa taifa.

 

Septemba mwaka huu, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilifikia uamuzi na kutangaza rasmi kwamba itaandaa mazishi ya kitaifa ya shujaa wao wa uhuru Lumumba baada ya nahakama moja ya Ubelgiji kuridhia jino la kiongozi huyo kurudishwa kwao.

   

Kitendo cha Lissu kuchagua Ubelgiji japo kuna hoja inajengwa  kuwa ni kwa lengo la matibabu inazua maswali mengi bila majibu kwa wadadisi wa mambo hususan masuala ya usalama kwa kuwa taifa hilo bado lina doa kwa nchi za Afrika hususan zile zenye baraka za Mungu kwa kujaliwa rasilimali tele kama madini ya thamani kubwa kama Tanzania.

Uhalali wa Hoja tatu za Lissu

Kama nilivyosema awali Lissu alitaja sababu kubwa tatu zilizomfanya kukimbilia Ubelgiji kuwa ni kuhofia usalama wake, kujipanga upya kisiasa na kueleza hali halisi ya Tanzania kwa watu anaowaamini yeye.

 

Tukianza kudadavua hoja ya kwanza ya Usalama wa mwanasiasa huyo  natamani kama taifa huru na yenye heshima tutafakari mambo matatu. Kwanza, tujiulize usalama wa Lissu unakuwa mashakani tu baada ya kampeni na Uchaguzi Mkuu kumalizika?

Pili, kwa nini hakuripoti Polisi na kupewa RB ili kuweka kumbukumbu sahihi kwamba kuna hali ya kuhofia usalama wake?

Tatu, ni kwa nini iwe tu Ubelgiji ndio nchi inayoweza kulinda usalama wa Lissu wakati nchi hiyo ina msimamo hasi kwa nchi za afrika hasa kwa kurejea kwamba bado mikono ya wahusika wa kifo cha Lumumba  inanuka damu?

Hoja ya pili ya kueleza hali halisi ya Tanzania imejaa upungufu mkubwa wa weledi na uwezo wa kufikiri kwa kiongozi anayeomba ridhaa ya kuongoza nchi kama Lissu.

Kama kweli kuna tatizo Tanzania, ni nani anayeweza kushughulikia tatizo hilo huku akiwa nje ya nchi na kufanikiwa kama si geresha na kupoteza lengo?  Ni kwa nini tusiamini kwamba Lissu anashiriki kwa njia nyingine kupanga mambo ya mwaka 1961 huko Congo?

Hoja ya Kujipanga upya kisiasa kwa nini ukajipange ukiwa nje kama kweli kuna nia njema ya siasa za maendeleo ya taifa?

Tunayo mifano hai kadha wa kadha kwa wanasiasa wetu wanaowania nafasi mbalimbali na kushindwa kupenya kwa wakati wakiweka mikakati mipya lakini wakiwa ndani ya maeneo yao.

Mfano wa karibu ni Jakaya Kikwete, alipogombea urais

na kukosa katika hatua za kura za maoni. Hakutoka kwenda kujipanga nje ya nchi. Alijipanga taratibu akiwa nchini na baadaye 2005 kura zikatosha na kuongoza Tanzania kwa miaka 10 lakini hakwenda nje ya nchi kujipanga upya baada ya kushindwa.

Lissu anatufanya tuanze kuwaza mbali zaidi kuhusu hata matibabu yake kuwa ina ajenda ya siri ndani yake na hasa baada ya Rais Magufuli kuonyesha wazi msimamo wake katika kudhibiti rasilimali za taifa na kusimama kidete kuzilinda kwa vitendo bila siasa wala woga.

Lissu anatufanya tuanze kubadili mawazo na kufikiria mbali zaidi kama kweli hata ajali yake ilihusisha watu hao hao kwa lengo la kufikia malengo yao kwa kuwa majasusi wa nchi hizo wana mbinu nyingi za kufanikisha malengo yao pale wanapoona ugumu!

Wengi waliamini kwamba awali aliposema Lissu kwamba hawezi kurejea Tanzania hadi hapo Serikali itakapomuhakikishia usalama wake walidhani kuna ukweli juu ya suala hilo lakini aliporejea nchini na kuanza kampeni za urais moja kwa moja wengi wanaofikiri kwa mapana walianza kuona dalili tofauti.

Hatua hii ya kukimbia haraka haraka baada ya uchaguzi mkuu na kudai hali ya usalama na kujipanga upya inazidi kuwafanya Watanzania kumhofia Lissu.

Shime vyombo vyetu vya usalama viongeze juhudi za uchunguzi na kubaini viashiria vya vibaraka kuanza kupenya ndani ya nchi yetu kwa mbinu mbalimbali kama hizi.

TAMATI.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages