LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 11, 2020

RAIS MAGUFULI AMUAPISHA PROF. MANYA, AAGIZA MISHAHARA YA WALIOHAMIA WIZARA YA MADINI KUTOKEA TMA IPUNGUZWE

Rais Dk. John Magufuli akimuapisha Prof. Shukrani Manya kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Madini, Ikulu jijini Dodoma, leo.


Ikulu, Chamwino, Dodoma

Dk. John Magufuli ameagiza waliokuwa wafanyakazi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMA) ambao walihamishiwa Wizara ya Madini mishahara yao ipunguzwe ili iendane na viwango vya mishahara vya watumishi wa Wizara hiyo.


Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo, Ikulu Jijini Dodoma, baada ya kumuapisha Prof. Shukrani Manya kuwa Naibu Waziri Madini, katika Wizara ya Madini.


Rais Magufuli amesema, wafanyakazi hao hawawezi kuendelea kulipwa mishahara mikubwa kuwazidi viongozi wao wa Wizara hasa baada ya ofisi waliyokuwa wameajiriwa kuvunjwa kutokana na utendaji usioridhisha.


“Nataka wafanyakazi wote wa iliyokuwa TMA wapunguziwe mishahara, na ambaye ataona mshahara hautoshi aondoke” amesisitiza Rais Magufuli


Rais Magufuli amemtaka Prof. Manya kutumia taaluma yake vizuri katika kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali yao ya madini badala ya kuacha rasilimali hiyo ikihujumiwa kwa utoroshaji, wizi, ukwepaji kodi na kuingia mikataba isiyofaa.


Amemtaka kwenda kushirikiana na viongozi wenzake wakiwemo Waziri, Katibu Mkuu na Wataalamu wa Wizara kuhakikisha wanafanya uamuzi na kukwamua masuala ambayo yalikuwa yamekwama kwa muda mrefu ili sekta ya madini ambayo imefanikiwa kuongeza mapato kutoka sh. Bilioni 168 mwaka 2015 hadi kufikia sh. Bilioni 527 iongeze mapato zaidi.


Rais Magufuli ametoa mwito kwa Wizara ya Madini kujadiliana na wadau ili madini yaliyopo nchini yatumike kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo chuma badala ya kutegema vyuma chakavu ambavyo baadhi huibwa kutoka kwenye miradi ya ujenzi wa reli au kuingizwa nchini kutoka nchi za nje, na kuzalisha umeme kwa kutumia urani na makaa ya mawe.


Rais Magufuli amewataka Watanzania wote waendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuitikia maombi yao ya kuliepusha Taifa dhidi ya ugonjwa wa Korona (Covid–19) ambao unaendelea kuangamiza maisha ya maelfu ya watu katika nchi mbalimbali duniani ilihali Tanzania ikiwa shwari.


Hafla ya kuapishwa kwa Prof. Manya imehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Job Yustino Ndugai, Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wafanyakazi wa Wizara ya Madini.


Prof. Manya pia amekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Latifa Mansour.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages