Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari, Dkt Jim Yonazi akizungumza katika kikao cha kamati ya
kujadili na kupitisha mpango mkakati wa kuipeleka jamii ya Tanzania katika
mfumo wa dijitali, katika ukumbi wa Wizara hiyo Mji wa Serikali Mtumba jijini
Dodoma Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula.
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mulembwa Munaku (aliyesimama) akiwasilisha Mkakati wa Kuipeleka jamii ya Tanzania kidijitali kwa wajumbe wa kamati ya mkakati huo katika ukumbi wa Wizara hiyo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma
Na Faraja Mpina WMTH
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari (WMTH) ameratibu Mpango mkakati wa pamoja wa kuipeleka
jamii ya Tanzania katika mfumo wa dijitali kwa kuanza na Sekta ya Elimu na
Sekta ya Afya ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja.
Dkt Chaula ameendesha kikao cha kamati ya utekelezaji wa mkakati huo
katika ukumbi wa Wizara hiyo mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kwa lengo
la kujipanga na kuuridhia mkakati huo ili kuhakikisha kunakuwa na uratibu
mahsusi unaokidhi malengo yaliyokusudiwa.
Kamati hiyo inayojumuisha taasisi za Serikali ina
mpango wa kuwashirikisha wadau mbalimbali wanaopeleka intaneti katika shule za
umma, hospitali na vituo vya Afya ili kuhakikisha kinachotolewa na wadau
kinakidhi mahitaji na vigezo vilivyokusudiwa vya kuipeleka jamii ya kitanzania
katika mfumo wa dijitali, Aliongeza Dkt chaula
“Sisi kama Wizara tuna malengo na matamanio
yetu, kupitia Sera ya TEHAMA ya Wizara ya mwaka 2016 na Sera ya Elimu ya TEHAMA
ya mwaka 2014 ili kwa pamoja kama Serikali tujipange, turidhie na tushirikishe wadau
wote wanaotuwezesha katika eneo hili ili kurahisisha ukusanyaji wa takwimu na
kujua maeneo yaliyofikiwa”, alisisitiza Dkt Chaula
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Jim
Yonazi amesema kuwa Serikali imejenga miundombinu mbalimbali katika Sekta ya
Afya na Elimu na kuongeza idadi ya shule, hospitali, Vituo vya Afya, barabara pamoja
na ufikishaji wa umeme vijijini kupitia REA na kusababisha kuongezeka kwa
mahitaji ya upelekaji wa huduma za intaneti katika maeneo hayo.
Aliongeza kuwa wananchi wanaofikiwa na hizi
huduma wanatakiwa kushiriki katika uchumi wa dijitali na Wizara ina jukumu la
kuhakikisha huduma za mawasiliano na data zinawafikia
Wananchi kwa kushirikiana na wadau ili juhudi
za Serikali ziwe na matokeo chanya katika utoaji wa huduma bora katika Sekta ya
Elimu na Afya.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara
hiyo Mulembwa Munaku amesema kuwa mkakati huo una lengo la kuhakikisha
miundombinu ya TEHAMA na huduma za mawasiliano zinatumika katika Sekta ya Afya
na Elimu na kutimiza lengo la Serikali kupitia Wizara hii iliyopewa dhamana la
kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 asilimia 80 ya wananchi wamefikiwa na huduma za
intaneti.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Ofisi ya Rais Tawala na
Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Erick Kitali amesema kuwa mkakati huo utasaidia
utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kwa gharama nafuu kama vile vituo cha
kutolea huduma jumuishi ‘one stop centre’ na huduma za tiba mtandao
ambapo mpaka sasa ni vituo 12 tu ndio vimeunganishwa na huduma hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu
wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba amesema kuwa UCSAF ina
jukumu la kuhakikisha TEHAMA inaleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi, na mpaka
sasa wamekwishapeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 711, intaneti katika shule
481 pamoja na kuwezesha Tiba Mtandao.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe kutoka
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wakuu wa taasisi zilizo chini
yake, Wizara ya Fedha na Mipango, TAMISEMI
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini,
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇