LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 19, 2020

DK. BASHIRU: KIONGOZI WA KUCHAGULIWA WA CCM ALIYEPATA UONGOZI WA DOLA KATIKA UCHAGUZI MKUU ULIOPITA AACHIE NAFASI YA KICHAMA

Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally akizungumza leo, jijini Dodoma

Makao Makuu ya CCM, Dodoma

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ally  amesema kiongozi wa ngazi yoyote wa kuchaguliwa ndani ya CCM ambaye amepata nafasi ya uongozi kwenye Dola katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka huu, aachie nafasi na Chama kitatoa utaratibu nchi nzima wa namna ya kujaza nafasi kwa njia ya uchaguzi.


"Principle ipo palepale, hatuwazuii viongozi wa Chama kugombea, waliokosa warudi kwenye nafasi zao, waliopata wawaachie wenzao nafasi hizo za chama." amesema Dk. Bashiru wakati akitoa ufafanuzi kwa viongozi wa Chama walioshinda na walioshindwa katika uchaguzi wa Dola uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.


Dk. Bashiru amesema hayo leo wakati  akiendesha kikao cha siku moja cha majadiliano na Sekretarieti za CCM za wilaya zote za Mkoa wa Dodoma, ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa NEC, Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma.


Katika kikao hicho Dk. Bashiru pia ametoa maelekezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwadhibiti na kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi na watumishi wa Chama au Serikali wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiwatapeli watu ili kupatiwa rushwa kwa kuwahadaa kuwa  watu hao watapandishwa cheo, kupewa ajira au kupata uteuzi.


Amesema hakuna rushwa inayopokelewa Makao Makuu ya CCM kwa ajili ya uamuzi wowote hivyo ametoa rai kwa wanachama na wananchi kuacha kutapeliwa na kutoa hongo yoyote kwa ahadi ya kupewa ajira, uteuzi au huduma yoyote kinyume cha utaratibu.


"Watu watakaotapeliwa kwa kisingizio kwamba kuna mgao unaletwa makao makuu, ama kuhusu ajira, kupandishwa cheo au uteuzi, hao wametapeliwa wao wenyewe, hakuna mtu katika uongozi wa sasa anayeweza akaleta hela hapa makao makuu, hayupo." amesema Katibu Mkuu Dk. Bashiru.


Dk. Bashiru ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko mbalimbali ya wananchi na wanachama waliodai kutapeliwa na viongozi na watumishi wasio waaminifu kwa kisingizio cha kupandishwa cheo, ajira au kupata uteuzi.


Kikao hicho, kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Rodrick Mpogolo, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Dk. Hawasi Haule, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Godwin Mkanwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Mkoa wa Dodoma Ismail Jama.

1 comment:

  1. Safi sana, ccm ndio chama chenye dira na kuonyesha njia Tanzania.

    ReplyDelete

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages