Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza alipokuwa akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo. jijini Dodoma leo. Kwa uelewa zaidi isome hotuba yake hii.
HOTUBA YA MHESHIMIWA MGENI RASMI
KATIKA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA WADAU WA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO KATIKA
UKUMBI WA PSSSF JIJINI DODOMA TAREHE 10 DESEMBA, 2020.
Dkt. Leonard Akwilapo, Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;
Mheshimiwa, Mwakilishi wa Swisscontact Shirika la Swiss Contact la Switzerland nchini Tanzania;
Bi. Winifrida Rutaindulwa, Mwenyekiti
wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE);
DKt.
Adolf B. Rutayuga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
(NACTE);
Wakuu wa Taasisi na Mashirika
mbalimbali;
Wajumbe wa Baraza la NACTE
Wenyeviti wa Bodi za Masomo wa Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE);
Viongozi wa Serikali katika ngazi
mbalimbali;
Wakuu wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi na
Mafunzo nchini;
Wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE);
Waandishi wa Habari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hii leo katika tukio hili muhimu
tukiwa salama na afya njema. Nifuraha yangu kuwa pamoja nanyi katika Ufunguzi
wa Mkutano huu wa Kimataifa wa Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo. Aidha,
nawashukuru na kuwapongeza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa
kuandaa na kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi
wa Mkutano huu, ambao unawakutanisha wataalam waliobobea katika masuala ya
Elimu ya Ufundi na Mafunzo.
Nafahamu
kuwa Mkutano huu umeandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Swiss-Contact chini ya
Ubalozi wa Switzerland nchini Tanzania. Napenda nitumie nafasi hii kwa niaba ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwashukuru sana Swiss-Contact kwa kufadhili
Kongamano hili. Tunashukuru sana kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali
ya Switzerland na Tanzania. Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi ya
Switzerland kwa lengo la kuleta maendeleo ya watu wetu baina ya nchi hizi
mbili.
Aidha,
nichukue nafasi hii kuwakaribisha wageni wote katika Jiji letu la Dodoma ambalo
ndiyo makao makuu ya Serikali nchini Tanzania. Kwa wageni kutoka nje mjisikie kuwa
mko Tanzania nchi ya amani na utulivu. Nimefurahi
pia kupata nafasi hii ya kushiriki nanyi katika Kongamano hili ambayo inanipa fursa ya kuzungumza nanyi
kuhusu umuhimu wa Elimu ya Ufundi na
Mafunzo hasa wakati ambapo azma ya nchi yetu ni kujenga nchi ya Uchumi wa Viwanda. (Mtakumbuka kuwa Mheshimiwa Raisi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dkt
John Joseph Pombe Magufuli, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri alisisitiza
kwamba ndani ya kipindi cha miaka 5 ijayo ajira zipatazo milioni 8 ziwe
zimetengenezwa).
Mabibi
na Mabwana,
Kauli
mbiu ya Mkutano huu ni “Enhancing
Triple Helix in Technical Education and Training” yaani “Kukuza
Ushikiano wa Makundi Matatu ya Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo”.
Wadau hao ni Serikali, Taasisi zinazotoa Elimu ya Ufundi na Mafunzo, na
Waajiri. Hakika kauli mbiu hii ina maana
kubwa sana na imekuja kwa wakati muafaka kabisa. Kauli mbiu hii inachochea
ushirikiano wa wadau wote katika Utoaji wa Elimu ya Ufundi na mafunzo hapa
nchini. Elimu ya Ufundi na Mafunzo ina mchango mkubwa sana katika Maendeleo ya
sekta zote za kiuchumi hapa nchini.
Aidha,
ulimwenguni kote Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi imejulikana kuwa ndiyo
inayotoa mchango mkubwa sana katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Viwanda na
pia maendeleo na ustwi wa jamii. Mashirika ya kimataifa ya UNESCO na ILO
wanaelezea Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa lugha ya kiingereza kama ifuatavyo: “TVET is an aspect of Education process
involving in addition to general Education, the study of technologies and
related sciences, and acquisition of practical skills, attitude, understanding
and knowledge relating to occupants in various sectors of economic and social
life”. Kwa hiyo Mkutano huu ni
jukwaa nzuri la washiriki wa Mkutano kuweza kutafakari wajibu wao katika utoaji
wa elimu bora ya Ufundi na Mafunzo kwa maendeleo endelevu katika nchi yetu. Elimu ya Ufundi ni nguzo muhimu ya kufikia
ajenda ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda. Tunatambua kuwa, kutoa Elimu ya Ufundi iliyobora
ni mkakati muhimu sana utakao saidia kubadili fikra na mitazamo ya raia walioelimika na kuwa mahiri katika stadi na maarifa
ya kutosha kusaidia kukabili changamoto za maendeleo ya nchi yetu. Nimefarijika
kusikia kuwa wadau mbalimbali wameitikia
na kujitokeza kwa wingi kwenye Kongamano hili.
Kuhudhuria kwenu, kujadili na kufikia maazimio yanayotekelezeka ndivyo vitakavyofanya dhima ya Kongamano hili iwe na
maana iliyokusudiwa. Nawapongeza sana wadau wote wakiwemo
waajiri waliotambua umuhimu wa Kongamano hili na hivyo kuweza kuhudhuria.
Mabibi
na Mabwana,
Kama mjuavyo, Tanzania tayari iko katika
uchumi wa chini wa kati, ili
Ili kuweza kuendelea na kupanda na kufikia uchumi wa juu
kunahitajika kuwa na mfumo rasmi wa kuwandaa vijana wetu katika viwango vya juu
vya maarifa na ujuzi wa stadi za kutenda.
Ili kuzalisha na kuendeleza rasilimali watu iliyo bora katika kada ya
kati ni lazima kuwepo kwa mahusiano mema na ya dhati kabisa baina ya taasisi
zinazotoa mafunzo na waajiri. Mahusiano hayo ndiyo yatazalisha wataalam bora
kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Kwa hiyo Kongamano hili linatoa fursa
adhimu ya kukutana, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati Kwa hiyo, Baraza linawajibu
wa kuhakikisha kuwa watoa Mafunzo na Waajiri (Industry) wanashirikiana wakati
wa maandalizi na wakati wa utoaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ili kubaini mahitaji ya soko la ajira na stadi
stahiki kwa wakati husika.
Mabibi na Mabwana,..
Kwa
mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, usimamizi wa tuzo za mafunzo
na upimaji wa kitaifa kwa lengo la kuweka uwiano katika taasisi za mafunzo ili kufikia viwango
vinavyohitajika ni wajibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Ni wazi
kwamba, Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi ni chombo muhimu sana kilichowekwa kisheria ili kusimamia jukumu
hilo. Kwa hiyo Baraza ni lazima
kuhakikisha kuwa linatekeleza wajibu huo kikamilifu kwa kutumia mamlaka lililopewa
ili kuendeleza na kuzalisha mtaji wa rasilimali watu wenye sifa kwa maendeleo
ya taifa.
Mabibi na Mabwana,
Taarifa
ya utafiti pia inaonesha kuwa ni wahitimu 95,771 kutoka katika vyuo mbalimbali
vya Elimu ya Ufundi wameingia katika soko la ajira kuanzia mwaka wa masomo
2014/2015. Hii namba ni ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji ya soko.
Inakadiriwa kuwa nafasi katika soko la ajira kwa ajili ya kukuza uchumi wa
Tanzania zitaongezeka hadi milioni 15 ifikapo mwaka 2030. Repoti inaonesha pia
kuwa sekta zote 6 zinakabiliwa na pengo la ujuzi (skills gaps), na waajiriwa
kufanya kazi zisizoendana na ujuzi walionao (skills mismatches).
Hali
hii inapelekea uzalishaji kuwa hafifu na kuzorotesha maendeleo ya uchumi
nchini. Kwa hiyo upo umuhimu mkubwa sana wa kukuza ushirikiano kati ya taasisi
za mafunzo, waajiri na na Serikali ili tuweze kuwa na wahitimu wanaokidhi
mahitaji ya soko la ajira. Ni matumaini yangu kuwa Kongamano hili litajadili
kwa kina na kutoka na maazimio ya namna gani tutaboresha utoaji wa mafunzo kwa
vijana wetu.
Mabibi na Mabwana,
Nina
taarifa kuwa kwa sasa tuna jumla ya vyuo 418 vinavyotoa Elimu ya Ufundi na
Mafunzo vilivyosajiliwa na NACTE ambavyo kwa ujumla wake vina wanafunzi wapatao 160, 000 kwa ngazi ya Astashahada na
Stashahada. Hali hii inaonesha kuwa kwa kipindi kilichosalia kufikia mwaka 2030
ambapo mahitaji yatafikia milioni 15, bado tunachangamoto kubwa kufikia malengo
hayo. Inahitajika jitihada za maksudi za kuhakikisha tunaendeleza kwa haraka
stadi za kuwajengea uwezo watu wetu. Kwa hali hiyo ni lazima kuangalia upya
uwekezaji wetu katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo. Ili kuhakikisha tunaiendeleza
na kuiimarisha sekta hii, ni muhimu
kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi
katika uwekezaji huu. Ni ukweli pia kuwa ili kufikia Tanzania ya Viwanda tunahitaji wataalam wengi zaidi wanaohitimu
kutoka katika vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyotoa stadi na ujuzi wa kutenda kwa
ufanisi.
Mabibi na Mabwana,
Wajibu
wa wadau wote wa elimu ni kushirikiana ili kuhakikisha elimuna mafunzo
yanayotolewa ni bora kuwawezesha wahitimu kuwa mahiri na walio na uwezo wa
kutosha kutatua changamoto zinazolikabili Taifa letu.
Elimu
na Mafunzo ya Ufundi lazima iwaandae vijana kuwa watengenezaji wa ajira badala
ya kuwa watafutaji wa ajira tu. Hili litawezekana tu pale taasisi na vyuo vya Elimu
ya Ufundi vikishirikiana na wadau mbalimbali na hasa waajiri, Serikali iko
tayari kupokea ushauri na kutuao ushirikiano katika kukuza ujuzi na umahiri.
Mabibi
na Mabwana,
Naomba
nihitimishe hotuba yangu kwa kusisitiza kuwa utoaji wa Elimu ya Ufundi inayojibu
matatizo ya jamii, inayoandaa vijana wenye umahiri wa kuweza kupambana na
changamoto za maendeleo katika ulimwengu wa sasa wa Sayansi na Technolojia ni
jambo la muhimu sana. Ili kufikia adhma
ya Serikali ya Awamu ya Tano inayongozwa na Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Uchumi wa Viwanda, Pamoja na mambo mengine,
tunahitajika kwa pamoja kuunganisha nguvu ili kuwekeza kiasi cha kutosha katika
Elimu ya Ufundi. Ni matarajio yangu kuwa Kongamano hili litatoka na maazimio na
ufumbuzi wa namna ya kukabiliana na changamoto za utoaji wa Elimu ya Ufundi
hapa nchini na kuishauri Serikali ipasavyo juu ya hatua za kuchukua ili elimu
itolewayo iendane na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadae.
Mabibi
na Mabwana,
Baada
ya kusema maneno hayo, nawatakia kila heri na mafanikio mema katika Kongamano hili. Na sasa napenda kutamka kwamba, Kongamano
la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo limefunguliwa rasmi.
Asanteni
kwa kunisikiliza.
Katibu Mtendaji wa Bataza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE),DKt. Adolf B. Rutayuga,
akizungumza maneno ya utangulizi
kuhusu utendaji wa Nacte wakati wa
ufunguzi wa kongamano hilo. Hii hapa chini ni hotuba yake.
Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Dkt. Leonard Akwilapo Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; kwa
kukubali mwaliko wetu wa kuja kufungua Kongamano hili la Wadau wa Elimu ya
Ufundi na Mafunzo hapa nchini. Vilevile napenda kutoa shukrani zangu za dhati
kwako Mgeni Rasmi kwa kukubali kufanyika kwa Kongamano hili, kutuunga mkono na
kwa maelekezo yako wakati wa maandalizi ya Kongamano hili.
Aidha, napenda kuwapongeza Vyuo vya Elimu ya Ufundi na
Mafunzo, Taasisi mbalimbali, Waajiri na Viongozi wa Serikali kwa kuitikia wito
wa kushiriki kwenye Kongamano hili la kwanza la aina yake lililo ratibiwa na Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE. Mafanikio
ya Kongamano hili ni matokeo ya ushirikiano baina Vyuo, Baraza la Taifa la
Elimu ya Ufundi na wadau wengine wakiwemo Ubalozi wa Switzerland nchini
Tanzania. Vilevile nachukua nafasi hii kuwakaribisha washiriki wote kwenye
Kongamano hili muhimu kwa maendeleo na ustawi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo
hapa nchini.
Ndugu Mgeni Rasmi,
Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayongozwa na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
ya kujenga Uchumi wa viwanda. Nchi
nyingi duniani zinatambua kuwa Elimu ya
Ufundi ni nyenzo muhimu sana katika kuchochea Maendeleo ya Viwanda. Ili elimu ya Ufundi iweze kuwa kichocheo kizuri katika kuchangia ujenzi
wa Uchumi wa Viwanda inapaswa iwe elimu inayozingatia umahiri wa kutenda na
mahitaji halisi ya Soko la ajira kwa wahitimu. Kongamano hili lina lengo la
kutoa fursa kwa Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo kujadili na kubaini njia bora zaidi zinazoweza
kuimarisha ushirikiano kati ya Vyuo vya mafunzo na Wadau wengine katika utoaji
wa mafunzo. Wadau ambao kwa sehemu kubwa wapo katika makundi matatu ambayo ni Vyuo vya Elimu ya Ufundi, Waajiri na Serikali. Lengo la Kongamano hili ni kubainisha njia bora za
kuimarisha ushirikiano wa makundi haya matatu katika utoaji wa mafunzo (“Enhancing
Triple Helix in Technical Education and Training”) kama dhima ya Kongamano
inavyosema.
Ndugu Mgeni Rasmi,
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi ni chombo
kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Sura ya 129, kwa lengo la kusimamia na
kuratibu taaluma zinazotolewa na taasisi na vyuo vya elimu ya ufundi
nchini. Jukumu kubwa la Baraza ni
kuendeleza na kuinua ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo kwa kusimamia
kikamilifu shughuli za usajili na ithibati, mitaala na upimaji ili tuzo
zinazotolewa ziwe na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Ndugu
Mgeni Rasmi,
Baraza linajukumu la kuweka sera, kanuni na taratibu
zinazotumika kusimamia viwango vya ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo nchini.
Aidha, kuvisaidia vyuo vya ufundi kukuza na kudumisha ubora wa viwango vya
elimu itolewayo na kuishauri Serikali katika kupanga mikakati ya kuendeleza
elimu ya ufundi na mafunzo nchini. Ili
kufikia adhima hii, Baraza limekuwa likitekeleza majukumu mbalimbali yakiwemo:
(a)
Kuratibu na kusimamia taaluma
zitolewazo katika elimu ya ufundi nchini, ili kuhakikisha kuwa kila mmiliki wa
chuo au taasisi ya mafunzo ya ufundi anazingatia viwango na vigezo vilivyowekwa
na Baraza;
(b)
Kuweka mfumo wa tuzo za kitaifa za
elimu ya ufundi zitakazo wawezesha wahitimu kutambuliwa kitaifa na kimataifa;
(c)
Kuratibu, kusimamia, kukagua na kutoa
ushauri kwa taasisi na vyuo vya ufundi, kuhusu ubora wa viwango vya elimu na
mafunzo ya ufundi yatolewayo kwa lengo la kuviwezesha kujiendesha vyenyewe na
kuhakikisha kuwa ubora wa elimu itolewayo unazingatiwa katika kipindi chote cha
mafunzo; na
(d)
Kuweka kanuni, taratibu na miongozo ya
usajili na uthibiti wa vyuo na taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi nchini.
Ndugu
Mgeni Rasmi,
Hivi sasa Baraza limesajili jumla Vyuo 418 vya Elimu
ya Ufundi hapa nchini. Vyuo hivi vinatoa
fani mbalimbali zikiwemo fani za Afya na Sayansi Shirikishi vyuo 174, fani za Biashara, Mipango na Utalii vyuo 155
na Fani za Sayansi na Teknolojia Shirikishi vyuo 89. Kati ya vyuo hivyo 418 vilivyosajiliwa na
Baraza, vyuo 182 ni vya Serikali na vyuo 236 visivyo vya Serikali
(sekta binafsi). Vyuo hivi vyote vinatoa
mafunzo kwa Mitaala inayozingatia Umahiri yaani (Competence Based Education Training- CBET). Pamoja
na mafanikio hayo, katika kutekeleza majukumu yake, zipo changamoto katika
utoaji wa mafunzo hayo zikiwemo za:-
·
Uhaba wa vifaa
vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vingi vya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi,
·
Ukosefu wa maeneo
ya kutosha ya mafunzo kwa Vitendo,
·
Kukosekana kwa
takwimu sahihi za mahitaji ya wataalam katika kila fani husika,
·
Vyuo kujielekeza
kutoa mafunzo katika fani ya aina moja,
·
Kuwepo
kwa uhusiano dhaifu kati ya taasisi za mafunzo na soko la ajira (Weak linkage
between institutions and industry);
n.k
Ndugu
Mgeni Rasmi,
Nimatarijio yetu kuwa kupitia Kongamano hili kutasaidia sana
kubaini ni kwa namna gani tunaweza kutoa Elimu ya Ufundi inayojibu matatizo ya
kiuchumi katika jamii yetu. Lakini pia kupitia Kongamano hili vyuo vitapata
nafasi ya kuzungumzia changamoto mbalimbali wanazozipata katika utoaji wa
mafunzo. Kwa upande mwingine waajiri nao pia wataweza kueleza ni changamoto
gani zinazotokea kwa kuwaajiri wahitimu kutoka katika vyuo na taasisi zetu za
mafunzo. Na nini kifanyike ili kukuza mashirikiano baina ya vyuo vyenyewe
lakini pia baina Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo na waajiri au Soko la
ajira.
Aidha, ni
matumaini ya Baraza kwamba, Kongamano
hili litatoa fursa ya vyuo kujifunza masuala
mbalimbali kutoka chuo kimoja na kingine na hivyo kuchochea ukuaji ushirikiano wa vyuo katika utoaji wa Elimu bora
inayokusudiwa na jamii. Kongamano pia litasaidia
pia kubaini maeneo ya uwekezaji ili kuzalisha wataalam wenye vipaji na mahiri
kwa fani zinazohitajika badala ya ilivyo hivi sasa vyuo vingi kujielekeza kutoa
fani za aina moja bila kuzingatia mahitaji halisi katika jamii.
Ni matumaini ya Baraza pia, mwishoni mwa kongamano hili taasisi na vyuo vya mafunzo
na waajiri/viwanda ushirikiano utaimarishwa ili kuifanya elimu ya ufundi
iendane sambamba na mahitaji ya soko la ajira.
Ndugu
Mgeni Rasmi,
Kwa dhati kabisa
ninapenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa usimamizi endelevu, kupitia
Wizara yetu, ya Elimu Sayansi na Technolojia kwa kusisitiza nyanja za uwekezaji na kuhimiza uboreshwaji wa
elimu ya ufundi na mafunzo. Kwa matokeo
na jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda,
Baraza litaendelea kuhakikisha linasimamia na kuratibu kikamilifu utoaji wa
Elimu ya Ufundi na Mafunzo ili wahitimu kutoka vyuo vilivyosajiliwa na Baraza
waweze kufanya vizuri katika soko la ajira
kwa kuwa na taaluma, ujuzi na umahiri unaohitajika kuipeleka Tanzania kuwa ya
Uchumi wa Viwanda. Nia na malengo yetu
katika kuimarisha mahusiano ya Taasisi
za Mafunzo, Waajiri na Serikali ni ili
kuweka mipango mikakati iliyo bora ya kuandaa rasilimali watu watakao ipeleka nchi
yetu kwenye Uchumi wa Viwanda na kuendelea kuupaisha uchumi kufikia Uchumi wa
kati wa juu hadi Uchumi wa juu.
Ndugu
Mgeni Rasmi,
Naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Ubalozi wa Switzerland kwa kufadhili
Kongamano hili, Tunawashukuru sana uwezeshwaji huu. Aidha, niishukuru Serikali na Sekta
Binafsi, taasisi na vyuo vya ufundi,
wadau wa elimu ya ufundi na mafunzo, na
wote ambao kwa namna moja au nyingine wamefanikisha kwa hali na mali kufanyika
kwa Kongamano hili. Kwa namna ya pekee ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Satano Mahenge na Sekretaiati yake ya Mkoa
na viongozi katika ngazi mbalimbali za Mkoa ushirikiano mzuri mliotupatia wakati wote wa
maandalizi wa Kongamano hili.
Ndugu
Mgeni Rasmi,
Naomba nimalizie hotuba yangu fupi ya Ukaribisho kwa
kurudia kumshukuru Mgeni Rasmi kuwepo nasi hapa leo tunajisikia faraja sana.
Aidha, ninawashukuru sana washiriki wa
Kongamano na kwa mawazo na michango mbalimbali mtakayoitoa kupitia kongamano
hili.
Asanteni Wote kwa Kunisikiliza!!!
Sehemu ya washiriki wakisikiliza kwa makini
Kwanza kabisa napenda kutumia
fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia wote uhai na kutuwezesha
kufikia siku hii ya leo. Pili naomba niungane na wenzangu waliotangulia, kutoa
shukrani zangu za dhati kwako Mgeni Rasmi
Dkt. Leonard Akwilapo Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutenga muda wako adhimu katika
ratiba yako na kuja kuwa Mgeni wetu Rasmi katika ufunguzi wa Kongamano
hili la wadau wa Elimu ya Ufundi na
Mafunzo hapa nchini. Pamoja na majukumu mengi uliyonayo, na hasa ikizingatiwa
kuwa hiki ni kipindi cha Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu
kumalizika, nidhahiri kama Katibu Mkuu unayo majukumu mengi sana ndani ya
Wizara. Lakini hata hivyo, bado umeweza kutenga muda katika ratiba yako na kuja
kujumuika pamoja nasi katika Kongamano hili. Hii inadhihirisha jinsi unavyoiweka
kipaumbele cha juu sekta hii ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo. Tumefarijika sana
kuwa nawe hapa katika ufunguzi wa Kongamano hili ambalo limeandaliwa na Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi kwa kushirikiana na Washiriki wetu wa maendeleo kutoka
Ubalozi wa Switzerland nchini Tanzania. Ndugu Mgeni Rasmi tunakushukuru
sana kwa ujio wako.
Ndugu Mgeni Rasmi;
Elimu ya Ufundi, ni elimu ambayo
inatilia mkazo mafunzo kwa vitendo na kufanya wahitimu kuwa nguzo muhimu sana
katika azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kujenga Uchumi wa
Viwanda. Katika azma hiyo ya Serikali, Wizara yako ndiyo yenye jukumu kubwa
sana la kuandaa rasilimaliwatu wenye stadi stahiki, umahiri na ujuzi wa kuweza
kutoa msukumo mkubwa katika ujenzi wa Uchumi wa Viwanda. Kama Baraza la Uongozi tuliona upo umuhimu wa
kuwakutanisha Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ili tukae pamoja tujadili na
kuweka maazimio yatakayotusaidia kuweka Mikakati Bora na Endelevu katika Utoaji
wa Elimu ya Ufundi.
Ndugu
Mgeni Rasmi;
Sisi wana-NACTE tunajisikia
fahari kubwa kuwa nawe ukiwa Katibu Mkuu kwenye Wizara yenye dhamana ya Sekta
hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Tunakushukuru kwa kutuamini kuwa
wasimamizi na waratibu wa utoaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo hapa nchini.
Mafunzo ya Elimu ya Ufundi katika fani mbalimbali kwa sasa yanatolewa katika
Vyuo 418. Kama Vyuo hivi vyote vingeleta wawakilishi wao ukumbi
huu usingetosha kabisa. Itoshe tu kusema kwamba waliopo ni wawakilishi wa
wenzao wengi ambao hawakufika hapa. Tunapenda
kukuhakikishia kuwa NACTE kwa kushirikiana na vyuo, taasisi za Elimu ya Ufundi
na Mafunzo na wadau wengine tutaendelea kwa juhudi kubwa kusimia utoaji wa
mafunzo na kuhakikisha kuwa Elimu ya Ufundi na Mafunzo inatolewa kwa ubora
unaotakiwa ili iweze kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje ya
nchi.
Ndugu
Mgeni Rasmi;
Tunaelewa kuwa tumepewa
dhamana kubwa ya kulisimamia Baraza lenye wajibu mkubwa katika Taifa hili. Taarifa
ya Katibu Mtendaji wa Baraza imeainisha mafanikio ya Baraza na changamoto
zinazo likabili. Hivyo tunaelewa jukumu lililo mbele yetu ni kubwa linalohitaji
ushirikiano na mshikamano wa hali ya juu ili kuweza kutatua changamoto hizo. Tunakuomba
usituchoke pale tutakapokuja kukusumbua mara kwa mara kukuomba ushauri na
maelekezo kuhusu maendeleo na mustakabali wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
na Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa ujumla. Aidha, tuko tayari kupokea maelekezo
yako utakayotupatia leo katika Kongamano hili na kwamba tutayafanyia kazi.
Ndugu Mgeni Rasmi;
Ili nchi yetu iweze kufikia azma
ya Tanzania ya Uchumi wa viwanda ni lazima kama nchi tuone ni kwa jinsi gani
tunawekeza na kuendesha Elimu ya Ufundi. Tunaomba kuishauri Serikali ichukue hatua
madhubuti katika kuelekeza rasilimali zake katika kuwekeza kwenye Elimu ya Ufundi na
Mafunzo na hasa katika mafunzo ya Sayansi na Teknolojia. Hivi sasa Baraza limesajili
jumla ya Vyuo 418 kati ya hivyo, vyuo vya Sayansi na Teknolojia Shirikishi ni
89 tu. Kati ya vyuo hivyo vya
Sayansi na Teknolojia Shirikishi vyuo 57
ni vya Serikali na vyuo 32
tu ni vya binafsi. Hii inaonesha kuwa uwekezaji
wa Sekta binafsi katika vyuo vya Sayansi na Teknolojia Shirikishi ni mdogo sana
ikilinganishwa na uwekezaji unaofanywa na Sekta hiyo katika vyuo vya fani za
Biashara, Utalii na Mipango na fani za Afya. Hii inatokana na gharama kubwa za
uwekezaji katika uanzishwaji wa vyuo vya aina hiyo.
Ndugu Mgeni Rasmi
Sote tuna fahamu kuwa, Miradi
mikubwa inayojengwa hapa nchini kama ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa, Bomba la
Mafuta na Mradi wa Kufua Umeme inahitaji sana wataalamu wenye fani za Sayansi
na Teknolojia Shirikishi. Hata hivyo, Vyuo vya Serikali vinavyotoa mafunzo hayo
havitoshelezi mahitaji. Aidha, vingi kati ya hivyo vinakabiliwa na changamoto
mbalimbali zikiwemo za miundombinu chakavu, uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia
na uhaba wa wakufunzi. Tunaomba kuishauri Serikali ione ni kwa jinsi gani itaelekeza
nguvu zake katika uwekezaji kwa Vyuo vya Sayansi na Teknolojia ili kuhakikisha
kuwa azma ya Uchumi wa Viwanda na nchi kufikia Uchumi wa Kati wa juu inafikiwa.
Ndugu Mgeni Rasmi;
Hadhara hii ni yako, tuliopo hapa tunayo shauku kubwa ya
kukusikiliza. Baada ya maneno machache haya, kwa heshima naomba sasa
nikukaribishe ili uweze kuongea na hadhara hii na kisha utufungulie Kongamano
hili la Wadau wa Elimu ya Ufundi na
Mafunzo ya Mwaka la Mwaka 2020.
Ndugu Mgeni Rasmi, Karibu sana.
Baadhi ya washiriki wakiwa makini kusikiliza hotuba hizo.PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇