LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 7, 2020

NAWAB MULLA ANOGESHA MAHAFALI YA KIDATO CHA NNE SEKONDARI YA KAWE UKWAMANI, AAHIDI MSAA WA KOMPYUTA NA MASHINE YA PHOTOCOPY

 Na Bashir Nkoromo, CCM Blog, Kawe

Mwenyekiti wa Kampuni ya Afritea Tanzania Tea Blenders Nawab Abdulrahman Mulla, ameahidi kuisaidia kwa hali na mali Shule ya Sekondari ya Kawe Ukwamani ya jijini Dar es Salaam, ili kuifanaya shule hiyo kuendelea kuwa shule bora ambapo katika hatua ya kwanza ameahidi kutoa msaada ya komyuta na mashine ya kurudufia (Photocopy).


Mulla ambaye alikuwa miongoni mwa wana CCM waliowania kupitishwa na Chama kugombea Ubunge Jimbo la Kawe na ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Mwenyekiti wa CCM mstaafu mkoa wa Mbeya, ametoa ahadi hiyo, jana katika hafla ya Mahafali ya Kidato cha nne katika shule hiyo ambako alikuwa mgeni rasmi.


Aliahidi kutoa msaada wa vifaa hivyo wakati wa hotuba yake ambayo aliitumia pia kujibu chanagamoto zilizotajwa katika risala iliyosomwa na wawakilishi wa wanafunzi, wakati wa hafla hiyo ambapo pamoja na mambo mengine walisema shule inakabiliwa na ukosefu wa kompyuta na mashine ya kurudufia (Photocopy), vyoo kujaa maji kutokana na eneo la shule kuwa oevu na uhaba wa chakula kwa ajili ya wanafunzi hasa wanaotoka katika familia zenye kipato duni na yatima.


Kuhusu suala la chakula, Mulla alisema, atafanya mchakato wa kuratibu namna ambavyo watoto hasa wanaotoka katika familia zenye vipato duni na yatima, waweze kuwa wanasaidiwa kupata chakula huku akiwaomba wazazi wenye uwezo ambao wana wanafunzi katika shule hiyo kujaribu kutengeneza mpango wa kuchangishana fedha walau kiasi kidogo kidogo ili kuokoa hatma ya watoto hao wenye mahitaji.



"Mimi ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM mkoa wa Mbeya, na nilikuwa nagombea kuteuliwa na CCM ili nigombee Ubunge jimbo hili la Kawe, sasa mdhidhani kukosa kwangu ubunge kutanifanya niache kuyatekeleza yale yote niliyokuwa nimekusudia kuwafanyia wananchi wa Kawe kama ningeupata ubunge", alisema Mulla na kuongeza:


"Wengine mtajiuliza kama nilikuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya sasa ilikuwaje nikagombea ubunge jimbo la Kawe?, kuhusu kuja kugombea Kawe hilo msiniulize hiyo ni siri yangu mimi na CCM".


Akiwaasa wanafunzi wa Kidato cha nne wanaotarajiwa kufanya mitihani yao hivi karibuni, Mulla aliwataka wanafunzi hao pamoja na wengine katika shule hiyo kuachana na mambo yote ya hovyo na kujikita kwa dhati katika masomo muda wote.


Mulla aliwaasa wanafunzi hao kuepuka matumizi ya simu za mkononi, akisema simu hizo zimekuwa chanzo kikubwa cha kupotosha wananfunzi kwa kuwa wengi wao hupoteza muda wao wa kusoma wakitazama video za hovyo au za wanamuziki na tamthilia tu.


Aliwataka pia kuacha kutamani kuwa wanamuziki au wasanii kwa kigezo kwamba baadhi ya wasanii na wanamuziki wamepata maisha mazuri kupitia tasnia hizo, akifafanua kwamba kufanikiwa katika sanaa ni bahati tu, tofauti na elimu ambayo siyo kitu cha kubahatisha.


Mapema kabla ya Mulla kukabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo vyeti na fedha kwa wadau wa maendeleo, walimu na wanafunzi, Mkuu wa shule hiyo Safina Egha alimwambia kuwa jumla ya wahitimu watarajiwa  wa kitado cha nne wanaofanyiwa mahafali hayo ni 189 kati yao 94 wakiwa ni wasichana.


Alisema, shule imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma hata kuzipita shule kadhaa za binafsi zikiwemo zilizopo katika Kata hiyo ya Kawe na kuongeza kuwa hadi sasa shule ina Walimu wabobevu wapatao 40 waajiriwa na 15 wa kujitolea.


Hafla hiyo iliyoambatana na burudani mbalimbali ikiwemo ya sanaa ya mapigano iliyooneshwa na Vijana wa Skauti na kuwaacha midomo wazazi kwa uhodari ulioonyeshwa, ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kawe Mkaguzi Msaidizi wa Polisi David Maro, Katibu wa CCM Kata ya Kawe Fatma Awadhi na Mjumbe wa Bodi ya shule hiyo Alifakisadi Mkindi.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Afritea Tanzania Tea Blenders, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Mbeya ambaye pia alikuwa mtia nia ya Ubunge kwa tiketi ya CCM jimbo la Kawe, Nawab Abdulrahman Mulla, akimlisha keki Mkuu wa Shule ya Sekondarai ya Kawe Ukwamani ya jijini Dar es Salaam, Safina Egha, baada ya kununua kipande cha keki hiyo kwa sh. laki moja, kuchangia mfuko wa shule, wakati wa mahafali ya kidato cha Nne yaliyofanyika jana. (Picha na Bashir Nkoromo, Official CCM Blog)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages