Na Mwandishi wetu✍🏽
Kwa mujibu wa Wakristu, Mtume Paulo akimwandikia waraka wa kwanza mwanafunzi wake Timotheo, kuhusu namna ya kutekeleza utumishi wake kwa watu ili uwe na manufaa kwa makundi mbali mbali ya watu anaowaongoza alimuasa kwamba;
“Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake…Dhambi za watu wengine huonekana waziwazi nazo zawatangulia kwenye hukumu; lakini dhambi za wengine huonekana tu baadaye. Vivyo hivyo matendo mema huonekana waziwazi, na hata yale ambayo si dhahiri hayawezi kufichika.”
Ujumbe bayana wa Paulo hapa ni kwamba, matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno. Ukiwatendea watu jambo jema wanatambua na wanaliona, na bila shaka watakushukuru na kukuheshimu kwa ajili hiyo. Vivyo hivyo ukiwatendea ndivyo sivyo, watafahamu ulivyowakosea na hawatasahau, ndiyo kusema ili mtu adumu kuwa mwema machoni pa watu wake, ajitahidi kutenda wema kwa kadiri ya uwezo wake na mahitaji ya watu hao.
Licha ya kwamba ujumbe huu umepo katika minajili ya kuimarisha imani za waumini kidini, lakini inasawiri pia hadi katika maisha ya kawaida ya mwanadamu kwa kuwa ina mafundisho makubwa pia ya kimaisha kwa binadamu yakifanyiwa tafakuri kwa hekima na busara
Kusudi la kutumia aya hiyo ya waraka wa Paulo kwa Timotheo ni kutaka kueleza japo kwa kifupi mantiki ya nini hasa kiini cha ushindi mkubwa alioupata Rais John Magufuli, katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliomalizika majuzi, Lakini kwa kutotazama walikojikwaa na badala yake wakatazama awalikoangukia, baadhi ya waliokuwa wagombea wa vyama vya upinzani na baadhi ya wafuasi wao wakajaribu kutilia shaka ushindi huo kiasi cha kutamani kufanya vitendo vinavyoweza kuisababishia nchi taharuki.
Tatizo la watu hao hawakutaka kuzishughulisha akili zao zintambue kuwa Rais Magufuli chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliingia nao katika uchaguzi akiwa ameshafanya kazi kubwa iliyowafanya Watanzania kuwa na imani.
Kazi hii ya kuwajengea imani Watanzania aliifanya kwa maarifa makubwa na kujituma kwa ari na moyo wake wote tangu alipoingia madarakani kutumikia kiti cha Urais katika awamu yake ya kwanza mwaka 2015.
Kwa ufupi na bila kuyataja aliyofanya kwa kuwa kila mtu anayajua kwa kuwa kama hakuyaona mubashara atakuwa ameyaona kwa macho au kuyasikia kwa masikio. Naam, tangu Dk. Magufuli aingie madarakani kazi zake alizofanya na kusimamia kwa nguvu zote, zimegusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwenye kila sekta.
Haya yote yanaonekana bayana machoni na mioyoni mwa wananchi, hawa wapiga kura vijana, wanawake kwa wanaume, wazee na kila mtu kwa namna yake ameguswa kwa karibu sana na juhudi za Rais Magufuli moja kwa moja, wangeshindwaje kumpa kura zilizojaa pomoni na kuibuka na ushindi mnono aliopata?
Kupangua hoja hizi na kuwashawishi wapiga kura wasiichague CCM na Rais Magufuli, ilihitaji hoja makini zilizoshiba, ili kuwafanya wananchi wafikirie upya.
Lakini pengine kwa kukosa hoja, wao wakaja na nyepesi nyepesi kama zile za kupuuza ujenzi wa miundo mbinu kwamba ni maendeleo ya vitu siyo ya watu kana kwamba zahanati ndiyo zinazosafiri barabarani, au reli ndiyo inatibiwa kwenye hospitali zilizojengwa, ulikuwa aina fulani ya mzaha ambao wapinzani waliamua kujiburudisha nao ili kalenda isogee, wasingeweza kumshawishi yeyote kwa hoja duni vile zaidi ya kujidhalilisha na kufunua udhaifu wao mbele ya wapiga kura.
Ni bahati mbaya kwa wapinzani kuwa katika mazingira ya utendaji kazi usiokuwa na mfano wa Rais Magufuli, hawakutaka kusoma alama za nyakati, hawakuwa na agenda mahsusi ambayo ingeweza kuwashawishi wananchi, waliendelea na masihara na mzaha wao waliozoea bila kubainia kuwa hali ya mambo imebadilika.
Mtu ambaye amepata huduma ya kituo cha afya katika kata yake, amepata umeme kijijini kwake, amefutiwa kero nyingi za kodi ya mazao na serikali Rais Magufuli angewezaje kumchagua Lissu, ambaye hata hana uhakika angefanya nini na kumwacha mtu aliyetimiza ilani na ahadi kwa vitendo?
Ni muhimu kutambua kwamba mwananchi anapopiga kura, na hasa wapiga kura makini, anaangalia kura yake itampa nini, anachagua manufaa na maendeleo ya maisha yake na hatma yake.
Ushindi wa Rais Magufuli ulikuwa dhahiri tangu alipoingia madarakani, uongozi wake umegusa maisha ya watu moja kwa moja, amekuwa kiongozi wa watu, ametatua shida zao kwa kiwango cha mtu binafsi mpaka taifa, ushindi huu wa kishindo kwa hakika ulitarajiwa na ni haki yake kwa kuangalia rekodi ya utendaji wa miaka mitano iliyopita.
Kelele zitapigwa nyingi, maneno ya wasioitakia Tanzania mema yatakuwa mengi, wenye wivu lakini ambao hawataki kujinyonga hawatanyamaza, lakini hayo yote hayatabadili ukweli kwamba Rais John Magufuli amefanya kazi kubwa sana, ambayo watanzania wameiona, wameikubali na wanaiheshimu. Ndiyo maana wakaamua kumtendea kama Paulo anavyosema; “mtenda kazi astahili ujira wake”.
Rais Magufuli ametenda kazi ya kutukuka, kitu pekee alichostahili ni kutendewa sawasawa na matendo yake, kipimo kile kile cha heshima na maendeleo alichowapimia watanzania, vivyo hivyo wamempimia kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hadi kuwangika cha kura nyingi za kishindo cha tufani. Hakika alistahili. CIAO
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇