👈Na Joe Nakajumo
"NILETEENI huyu……nileteeni
hawa na mimi naomba kura zenu", hii ni kauli iliyotolewa na mgombea
urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Magufuli katika mikutano yake yote ya kampeni ya uchaguzi
mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika hivi karibuni.
Kauli mbiu hiyo imesaidia pamoja na mikakati mingine ya
kampeni za uwazi za CCM kuwawezesha Dk. Magufuli, wagombea ubunge na madiwani
wa CCM kuibuka washindi kwa kupata kura nyingi katika uchaguzi uliomalizika.
Dk. Magufli alitangazwa Oktoba 30, 2020 na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) kuwa mshindi kwa kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia
84.4.
Alipogombea mara ya kwanza Urais mwaka 2015 alipata
zaidi ya kura milioni nane zikiwa ni sawa na asilimia 58.
Uchaguzi wa mwaka huu ambao ni wa sita chini ya mfumo wa
vyama vingi ulifanyika Oktoba 28, mwaka huu ambapo kampeni zilianza Agosti 26
na kumalizika Oktoba 27.
Katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili, wagombea
urais, ubunge na madiwani walikuwa katika kampeni za kunadi sera za vyama vyao
mbele ya wananchi ili kuomba wachaguliwe na kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka
mitano yaani 2020 hadi 2025.
WANACCM WAPOKEZANA KIJITI CHA URAIS
Tanzania iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi 1992 na
uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo huo ulifanyika 1995 Wana CCM wamekuwa
wakipokezana kijiti cha mbio za kuwania Urais na kushinda.
Mshindi wa kwanza kiti cha Rais kwa tiketi ya CCM alikuwa
hayati Benjamin Mkapa.
Tangu wakati huo kwa mfululizo CCM imeshinda kiti cha
Urais ambapo hayati Mkapa aliyefariki Julai mwaka huu alitetea kiti chake,
mwaka 2005 ulipofanyika uchaguzi na Dk.Jakaya Kikwete alishinda kuwa Rais miaka
10 kuanzia 2005 hadi mwaka 2015.
Baada ya Rais Kikwete kuondoka, Dk.Magufuli alipokea
kijiti na kushinda uchaguzi wa mwaka huo Oktoba 2015.
Mwaka huu matokeo yaliyotangazwa yanamwezesha kumalizia kipindi cha pili cha
miaka mitano hadi 2025.
Mgombea wa CCM, Dk. Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM
,alikuwa ni miongoni mwa wagombea kutoka vyama 15 walioshiriki kuwania nafasi
ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tofauti na wagombea wenzake 14 wakiwemo wanawake wawili,
Dk. Magufuli ambaye kwa mara ya kwanza alishinda Urais mwaka 2015,alipitishwa
na Mkutano Mkuu wa Chama kugombea urais kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Katika mikutano yake ya kujinadi kwa Watanzania akiomba
ridhaa yao ili wamchague kumalizia ngwe ya pili ya miaka mitano ijayo, Dk. Magufuli
alikuwa akisisitiza sana umoja, mshikamano na kudumisha amani.
USHINDI NA
UKAMILISHAJI WA MIRADI.
Suala lingine alilokuwa akiwaeleza wananchi ni mafanikio
ya utendaji wa serikali yake katika kipindi cha miaka mitano aliyomaliza.
Aliwatajia wananchi mafanikio yaliyopatikana katika
sekta zote za jamii zikiwemo afya,maji,miundombinu na elimu.
Aidha alikuwa akiwaeleza mambo ambayo serikali yake
itatekeleza kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano
ijayo iwapo Chama chake kitapata ridhaa ya wananchi kuongozi nchi.
Lakini pia alikuwa akiwakumbusha wananchi jinsi serikali yake ilivyoibua na
kuanza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na kuwaomba ridhaa wamchague ili
aweze kukamilisha miradi aliyoianzisha maana hakuna uhakika wa miradi hiyo
kukamilishwa endapo hatachaguliwa.
Miradi hiyo ni ujenzi wa reli ya kisasa itakayotumia
umeme kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma.
Awamu ya kwanza ya mradi wa reli ya kisasa ’STANDARD
GAUGE RAILWAY SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro unakaribia kukamilika
kwani umefikia asilimia 95.
Treni ya umeme itakayosafiri katika reli hiyo itakuwa na
kasi ya kilomita 160 kwa saa.
Dk.Magufuli alitaja miradi mingine inayotekelezwa ni
ujenzi wa bwawa la Nyerere kufua umeme katika mto Rufiji ambapo litakapokamilika
mwaka 2022 litazalisha umeme wa kilovoti 2,115.
Pia mara tu baada
ya serikali yake kuingia madarakani
mwaka 2015,ilishanunua ndege mpya 11, na tayari ndege nane zinafanya
kazi serikali ikiwa imezikodisha ndege hizo kwa
Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Mgombea wa CCM anasema Ilani ya Uchaguzi wa CCM yenye
kurasa 303 ina kipengele cha ununuzi wa ndege nyingine mpya tano moja ikiwa ya
mizigo.
AING’ARISHA DODOMA NA IKULU YA CHAMWINO
Uamuzi mwingine wa kihistoria ambao Dk. Magufuli aliuchukua
mara baada ya kuingia madarakani ni serikali yote kuhamia makuu Dodoma.
Hatua hii aliichukua baada ya kipindi cha zaidi ya miaka
40 tangu serikali ya awamu ya kwanza iliyoongozwa na hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere, kuamua makao makuu ya serikali yahamia Dodoma kutoka
Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamia
Dodoma ulipitishwa na Mkutano Mkuu wa TANU Oktoba, mwaka 1973.
Hivi sasa serikali nzima ipo Dodoma Rais Dk.Magufuli ameenda
mbele zaidi kwa kupanua eneo la Ikulu Chamwino kwa kuongeza majengo mapya na
kuweka bustani ya wanyamapori ndani ya eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 8,473 ambalo limezungushiwa ukuta wa
kilomita 27.
Ikulu ya Dar es Salaam na barabara zake ina eneo la
kilomita 41.8. Dodoma mji wa serikali upo eneo la Itumba ambako kuna wizara
zote.
ALIWABEBA WAGOMBEA WA CCM
Kwenye mikutano ya kampeni, Dk. Magufuli alikuwa na kazi
ya ziada na katika majimbo mengine kazi
ya kuwaombea wabunge na madiwani kura ilikuwa ngumu kutokana na fununu
alizokuwa nazo kwamba mgombea aliyepitishwa na Chama hakubaliki na hivyo kusababisha
wasiwasi wa Chama kushinda katika jimbo husika.
Lakini kwa ujasiri mkubwa alizisawazisha kasoro hizo
mbele ya halaiki ya wananchi waliohudhuria mikutano yake.
Mtindo wake wa kuwaombea kura wagombea ubunge na udiwani umesaidia sana kuiwezesha
CCM kupata ushindi wa kishindo na wa kihistoria katika uchaguzi mkuu wa mwaka
huu wa 2020.
Alikuwa anawasimamisha wabunge mmoja mmoja kuomba kura
na madiwani wote wa jimbo husika walisimama katika msitari mmoja mbele ya umati
wa watu na kuwaombea kura.
‘Nileteeni huyu…… kwa maana mbunge na nileteeni hawa kwa
maana ya madiwani Na alimalizia kwa kuwaomba wananchi kwamba ‘na mimi naomba
kura,wangapi watanipigia, aliwauliza wananchi nao waliitika kwa umoja wao
wakisema ‘umepita baba, umepata baba’.
Jambo lingine ambalo alilifanya kwa wagombea udiwani wa
CCM ni yeye kuwaapisha mbele ya wananchi kwa kuwataka warudie maneno aliyokuwa
akiyatamka kwa mfano’,nitajitahidi kusikiliza kero za wananchi na kutafuta
namna ya kuzitatua,sitaomba rushwa.’
‘Mkinichanganyia kazi yangu itakuwa mgumu,lakini
mkiniletea hawa wa CCM, ni rahisi kuwadhibiti kwa sababu mimi ndio Mwenyekiti
wao,madiwani ndio wanaosimamia shughuli za Halmashauri na halmashauri inapokea
fedha nyingi kutoka serikali kuu,
kwa hiyo hawa wana majukumu makubwa ya kusimamia miradi
ya maendeleo katika maeneo yao,’ aliwaeleza
wananchi katika mikutano yake.
ATALIPA DENI KWA KUCHAPA USIKU NA MCHANA
Hatimaye Dk. Magufuli aliyezindua kampeni kwa Chama chake cha Mapinduzi Agosti 29 mkoani Dodoma na alihitimisha hapo hapo Dodoma Oktoba 27 kwa kuzungumza na
wazee mjini Dodoma.
Kutokana na wananchi wengi kujitokeza kwa wingi katika
mikutano yake ya kampeni, Dk. Magufuli alikuwa akiwaeleza wazi kwamba alikuwa
na deni kwao.
Siku ya Novemba Mosi,2020,katika ukumbi wa Tume UCHAGUZI HOUSE Dodoma alipokabidhiwa
cheti cha ushindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rais Mteule Dk. Magufuli katika
hotuba yake fupi ya kuwashukuru wananchi alisema;’kwangu mimi nina deni kubwa sana
kwa Watanzania kwa imani yao na mimi nitatimiza
kwa kufanya kazi usiku na mchana.’
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2020 wananchi 12,516,252 wamemkubali Dk. Magufuli
na kumpa ridhaa ya kuongoza kipindi kingine cha miaka mitano ambacho ni cha
mwisho kwake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wagombea wengine wa Urais walikuwa Tundu Lissuwa Chadema
aliyepata kura 1,933,271,Bernard Membe wa ACT Wazalendokura 81,129,Profesa Mahona
Lucas wa NRA kura 80,787, Ibrahim
Lipumba CUF kura 72,885,
John Shibuda wa ADA TADEA kura 33,086 Mutamwega Mugahywa
wa SAU 14,922,Cecilia Mmanga Demokrasia Makini kura 14,556,Maganja Jeremiah
NCCR Mageuzi kura 19,969,.
Philipo Fumbo wa DP kura 8,283,Queen Sendiga ADC kura 7,627,Twalib Kadege wa UPDP kura
6,194,Hashim Rungwe wa CHAUMA kura 32,878 na Mazrui Khalfan Mohamed wa UMD kura
3,721 na Seif Maalim Seif wa AAFP kura 4,635.
#Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwenye simu namba 0784291434 email nakajumoj@gmail.com
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇