JAJI Mkuu wa Tanzania Mhe Profesa Ibrahim Hamis Juma akimuapisha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli leo 5/11/2020, katika uwanja wa Jamuhuri Jijini Dodoma, baada ya kushinda uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika mwaka huu Oktoba 28,2020.(Picha na Ikulu)
Ikulu, Dodoma
Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, leo tarehe 05 Novemba, 2020 ameapishwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili cha miaka 5 baada ya
kipindi cha kwanza cha miaka mitano kumalizika.
Mhe. Dkt. Magufuli
ameapishwa kushika wadhifa huo baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu
uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 ambapo alipata jumla ya kura 12,516,252 sawa
na asilimia 84.4 ya kura zote zilizopigwa kwa wagombea 15 waliokuwa wanawania
kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Dkt. Magufuli
ameapishwa pamoja na Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameapishwa kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sherehe za kiapo
hicho zimefanyika kwa mara ya kwanza katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma
ambako ni Makao Makuu ya Tanzania na zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Marais
Wastaafu, Makamu wa Rais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Mabalozi,
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya za Kikanda, viongozi wakuu wa vyombo
vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa kikiwemo
chama tawala nchini Tanzania (Chama Cha Mapinduzi – CCM)
na viongozi wa sekta binafsi.
Viongozi Wakuu wa
Nchi waliohudhuria sherehe hizo ni Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri
Kaguta Museveni, Rais wa Umoja wa Visiwa vya Komoro Mhe. Azali Assoumani, Rais
wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emerson Mnangagwa na pia Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Botswana Mhe. Slumber Tsogwane ambaye amemwakilisha Rais wa nchi hiyo Mhe.
Mokgweetsi Masisi, Waziri Mkuu wa Msumbiji Mhe. Carlos Agostinho Rosario ambaye
amemwakilisha Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi na Naibu Waziri Mkuu wa Qatar Sultan
bin Saad Al Muraikhi aliyemwakilisha Mtawala wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad
Al-Than.
Aidha, Marais na
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kenya, Afrika Kusini, DRC, Malawi, Misri, Zambia,
Kuwait, Namibia, Rwanda, Umoja wa Ulaya na Ethiopia wamewakilishwa
naWaheshimiwa Mawaziri na Mabalozi wa nchi hizo.
Akizungumza baada
ya kuapishwa kwake, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote waliohudhuria
sherehe za kuapishwa kwake wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali
hapa nchini na amewahakikishia kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na
uhusiano mzuri uliopo kati yake na nchi hizo.
Mhe. Rais Magufuli
amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wote wa Tanzania
kwa kuhakikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unafanyika na kukamilika kwa amani na
utulivu, jambo ambalo limeendelea kudhihirisha kuwa Tanzania sio tu kisiwa cha
amani bali pia ni kitovu cha demokrasia.
Mhe. Rais Magufuli
amesema uchaguzi umekwisha na kwamba jukumu lililo mbele ya Watanzania ni
kuchapa kazi na kuleta maendeleo. Hivyo ameahidi kutekeleza Ilani ya Uchaguzi
Mkuu ya CCM ya mwaka 2020/25 huku akitilia mkazo katika ujenzi wa miradi ya
maendeleo, kutunza rasilimali za Taifa, kuzalisha ajira, kushughulikia kero za
wananchi na kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa.
Amekishukuru chama
chake cha CCM kwa kufanya kampeni nzuri zilizowezesha kupata ushindi mkubwa
katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao sasa wanakwenda kubeba
jukumu la kuwahudumia wananchi wa Tanzania kama walivyoahidi.
Katika sherehe
hizo Wakuu wa Nchi wamepata nafasi ya kutoa salamu ambapo Mhe. Rais Museveni
pamoja na kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuchaguliwa na kuapishwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka Watanzania hasa vijana kurejea
madhumuni ya uhuru uliopiganiwa na waasisi akiwemo Hayati Mwl. Julius Kambarage
Nyerere huku akiwataka kujiepusha kuwa vibaraka wa mabeberu na kufanya kazi ili
kujitegemea na kujenga ustawi wa jamii.
Kwa upande wake,
Mhe. Rais Mnangagwa wa Zimbabwe ameishukuru Tanzania ambayo amesema Zimbabwe
inaiona kama Baba na Mama huku akitambua juhudi za kuanzia Hayati Mwl. Nyerere
hadi Mhe. Rais Magufuli ambao wamekuwa mstari wa mbele kuipigania Zimbabwe bila
kuchoka.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
05 Novemba,
2020
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇