Na Mwandishi Wetu, MWANZA
VIGOGO, Yanga SC wametoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wahamiaji, KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
VIGOGO, Yanga SC wametoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wahamiaji, KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Kwa ushindi huo, mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu, wanafikisha pointi 19 katika mchezo was aba, ingawa wanabaki nafasi ya pili, nyuma ya vinara, Azam FC waliokusanya pointi zote 21 katika mechi saba – wakati mabingwa watetezi,Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 13 za mechi sita.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramadhan Kayoko aliyekuwa anasaidiwa na Hamisi Chang’walu na Abdul Malimba wote wa Dar es Salaam KMC walitangulia kwa bao la Hassan Salum Kabunda dakika ya 27.
Kabunda, mtoto wa beki wa Yanga SC miaka ya 1990, Salum Kabunda, sasa marehemu alimtungua kipa Metacha Boniphace Mnata kwa shuti kali la umbali wa mita 22 baada ya kuwahadaa walinzi wa Yanga kufuatia kupokea pasi ya kiungo mwenzake, Kenny Ally Mwambungu.
Kiungo Tuisila Kisinda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akaisawazishia Yanga SC kwa mkwaju mzuri wa penalti dakika ya 41 akimchambua kipa mkongwe Juma Kaseja kufuatia mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kuangushwa kwenye boksi.
Kipindi cha pili, Yanga SC wakafanikiwa kupata bao la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Waziri Junior aliyemalizia kwa kichwa kona ya mtokea benchi Farid Mussa Malik dakika ya 61.
Baada ya kufunga bao hilo, Waziri, alivua jezi kuonyesha fulana iliyoandikwa “The King of CC Kirumba Stadium’, akimaanisha yeye ni Mfalme wa Uwanja huo kutokana na rekodi yake ya mabao tangu akiwa anachezea Toto Africans na Mbao FC zote za Mwanza ambazo zimeshuka Daraja.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Biashara United imeshinda 1-0 dhidi ya wenyeji, Polisi Tanzania bao pekee la Deogratius Judika Mafie dakika ya 53 Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
JKT Tanzania ikaichapa 6-1 Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga mabao ya timu ya Jeshi la Kujenga Taifa yakifungwa na Adam Adam matatu dakika ya 24, 48 na 82, Danny Lyanga dakika ya 40 na 52 na Said Luyaya dakika ya 90 na ushei, wakati la wenyeji limefungwa na Pastory Athanas dakika ya 62.
Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu, ikiwemo mabingwa watetezi, Simba SC kumenyana na Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Mtibwa Sugar na Azam FC Uwanja wa CCM Gairo, Dodoma.
Kikosi cha KMC kilikuwa; Juma Kaseja, Israel Mwenda, David Bryson, Lusajo Mwaikenda, Andrew Vincent ‘Dante’, Jean Baptiste Mugiraneza/Cliff Buyoya dk85, Abdul Hillary/Martin Kiggi dk73, Kenny Ally, Paul Peter, Emmanuel Mvuyekure na Hassan Kabunda/Relliants Lusajo dk.
Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomary, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Deus Kaseke/Farid Mussa dk59, Feisal Salum, Michael Sarpong, Waziri Junior/ Haruna Niyonzima dk82 na Tuisila Kisinda/Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dk89.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇