Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea cheti cha ushindi wa Ubunge wa Jimbo la Ruangwa kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Frank Chonya (kushoto) kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Oktoba 29, 2020. Kulia ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe, Mary wakitazama cheti cha ushindi wa Ubunge wa Jimbo la Ruangwa baada ya kukipokea kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Frank Chonya kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Oktoba 29, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
****************************************
MBUNGE mteule wa jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amepokea cheti cha kumtambulisha rasmi kuwa mbunge mteule wa jimbo hilo.
Amepokea cheti hicho leo (Alhamisi, Oktoba 29, 2020) kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Ruangwa, Bw. Frank Chonya katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Akizungumza mara baada ya kupokea cheti hicho, Mheshimiwa Majaliwa amesema anamshukuru Mungu kwa kuwezesha yote na kuwafikisha hapo na kuwavusha salama kipindi cha kampeni kwa karibu miezi miwili.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa, alisema kipekee anashukuru vyama vya siasa wilayani humo kwa kumuamini na kuthamini maendeleo. “Sisiti kusema vyama vya siasa vimeendelea kuthamini maendeleo ya wilaya yetu. Lakini katika hili, niseme kwamba tumeliweka mbele sana suala la maendeleo ya wilaya yetu. Ninawashukuru sana.”
Amesema kupatiwa cheti cha kumtambua rasmi kuwa mbunge mteule hadi atakapoapishwa, kumetokana na imani yao kubwa waliyoionesha kwake na kuamua apite bila kupingwa.
“Leo niko hapa mbele yenu, nimemaliza muda wangu wa 2015-2020, mmenivumilia, mmenipa ushirikiano na mmenisaidia kuifanya kazi yangu vizuri. Ninawashukuru viongozi wote na wananchi wa Ruangwa kwa mchango wenu uliowezesha Ruangwa ipige hatua ya maendeleo. Mimi, mke wangu na watoto tunawashukuru sana.”
Amesema katika miaka mitano iliyopita, yako mambo mengi waliyofanya na katika kipindi hiki yako mambo yaliyobakia kama kupeleka umeme na maji vijijini. “Ninawaahidi kushirikiana nanyi ili kufikia malengo yaliyowekwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.”
Aliwapongeza madiwani wote walioshinda katika kata zote 22 na kuwaahidi kuwa yuko pamoja nao kuijenga Ruangwa.
Mapema, akizungumza kabla ya kumkabidhi cheti chake, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Ruangwa, Bw. Frank Chonya alisema jimbo hilo lenye kata 22, lilikuwa na watu waliojiandikisha kupiga kura 106,043 na lilikuwa na vituo 311 vya kupigia kura.
Alisema vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo ni CCM, ACT Wazalendo, CUF na CHADEMA. “Kabla ya uchaguzi, kata saba, wagombea wake kutoka Chama cha Mapinduzi walipita bila kupingwa. Jana baada ya uchaguzi, CCM imeshinda kata 12, ACT kata mbili na CUF kata moja.”
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇