Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Oktoba, 2020
ameshuhudia kampuni ya Twiga Minerals na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
likitoa gawio kwa Serikali kutokana na faida katika biashara ya madini.
Hafla ya utoaji wa
gawio hilo imefanyika katika ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano cha
Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo kampuni ya Twiga Minerals imekabidhi
Dola za Marekani Milioni 40 (sawa na takribani shilingi
Bilioni 100 za Tanzania) na STAMICO imekabidhi
shilingi Bilioni 1.1 kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Aidha, katika
hafla hiyo wachimbaji wadogo wa madini kupitia chama chao (FEMATA)
wametoa tuzo kwa Mhe. Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kulinda
maslahi ya wachimbaji wadogo na maslahi ya Watanzania katika rasilimali yao ya
madini.
Waziri wa Madini,
Mhe. Dotto Biteko amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya dhati na
mwongozo wake katika usimamizi wa madini ambao umesaidia kubadili sekta ya
madini kutoka sekta iliyofichwa na isiyo na maslahi kwa Watanzania na kuwa
sekta inayofanyika kwa uwazi na inayowanufaisha Watanzania kwa kuchangia fedha
nyingi katika pato la Taifa, kutoa ajira na kustawisha jamii.
Mhe. Waziri Biteko
ametoa mfano kuwa kati ya mwaka 2015/16 na mwaka 2019/20 mapato ya madini
yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi shilingi Bilioni 528 na kwa
sehemu kubwa shughuli za madini zinafanywa na Watanzania wenyewe badala ya
kufanywa na wageni kama ilivyokuwa zamani.
Katika hotuba
yake, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio makubwa
ambayo Tanzania imeyapata baada ya kuchukua hatua za kutunga sheria mpya ya
madini, kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini na kuanzisha masoko ya madini,
na amewataka Watanzania wote kutembea kifua mbele kwa kuwa sasa madini yao
yameanza kuwanufaisha.
Mhe. Rais Magufuli
amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na utajiri wa aina mbalimbali za madini, gesi
na mafuta hivyo ni wakati wa Watanzania kuamka na kuchangamkia fursa za
uchimbaji na uwekezaji katika rasilimali hizo bila kujali hadhi ya mtu, kampuni
ama taasisi, ilimradi hawavunji sheria na wanalinda maslahi ya Taifa kwa kulipa
kodi na tozo mbalimbali za kisheria.
Amewashangaa
Watanzania ambao walikuwa wakipinga hatua zilizochukuliwa na Serikali
kurekebisha dosari zote zilizosababisha Watanzania kutonufaika na madini yao
ikiwemo kukamata makinikia ya dhahabu, kudhibiti wizi na utoroshaji, kupitia
upya mikataba ya madini, kudai fidia na kutunga sheria zilizoiwezesha nchi kuwa
na umiliki wa asilimia 16 katika migodi ya madini na kupata mgao wa 50/50
katika faida ya biashara ya madini.
Mhe. Rais Magufuli
ameipongeza kampuni ya Barrick Gold ambayo ilikubali kuingia katika majadiliano
na Serikali na matokeo yake kuundwa kwa kampuni ya Twiga Minerals ambayo leo
imekabidhi gawio la shilingi Bilioni 100, na pia ameipongeza kamati
iliyoongozwa na Prof. Palamagamba Kabudi ambayo iliiwakilisha Serikali katika
majadiliano hayo, kwa kutekeleza jukumu hilo kwa uzalendo mkubwa licha ya
kuzingirwa na vishawishi vya rushwa na hatari za kiusalama.
Aidha, Mhe. Rais
Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania ni mahali salama pa uwekezaji na ametoa wito
kwa wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuja
kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, na kwamba Serikali
itakuwa tayari wakati wote kutoa ushirikiano utakaofanikisha uwekezaji huo
ilimradi kuwepo mazingira ya mwekezaji kupata na Serikali kupata (win-win).
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wa Dini na Watanzania wote kwa maombi na dua kwa Taifa na amewataka kuendelea kufanya hivyo kwa kuwa Taifa linalosimama na Mungu hufanikiwa, kama ambavyo Tanzania imefanikiwa katika maeneo mengi ikiwemo kuepusha ugonjwa wa Corona (Covid-19) na kusimama kidete kutetea maslahi ya Watanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea gawio la dola milioni 40,000, 106,91 la Kampuni ya Madini ya TWIGA toka kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpangowakishuhudiwa na wajumbe wa bodi hiyo wakati wa hafla ya kupokea gawio toka kwa kampuni ya Madini ya TWIGA na Shirika la Madini la Taifa STAMICO katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Julius Nyerere
jijini Dar es salaam leo Jumanne Oktoba 13, 2020
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea gawio la Sh. Bilioni Moja na Milioni Mia Moja toka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Meja Jenerali (Mstaafu) Michael Isamuhyo akishuhudiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka akati wa hafla ya kupokea gawio toka kwa kampuni ya Madini ya TWIGA na Shirika la Madini la Taifa STAMICO katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Jumanne Oktoba 13, 2020
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea tuzo maalumu toka kwa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (Femata), John Bina, na makamu wake wakati wa hafla ya kupokea gawio toka kwa kampuni ya Madini ya TWIGA na Shirika la Madini la Taifa STAMICO katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Oktoba 13, 2020
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wageni waalikwa na wadau wa madini wakati wa hafla ya kupokea gawio toka kwa kampuni ya Madini ya TWIGA na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Oktoba 13, 2020. PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇