Wananchi wakinyoosha mikono juu kukubaliana kumpigia kura Dk Magufuli na wagombea wengine wa CCM.
Okash akizungumza katika mkutano huo kwa kuwahimiza wananchi kuwahi vituoni Oktoba 28 kuwapigia kura wagombea wa CCM.
Na Mwandishi Wetu, Kondoa.
MGOMBEA Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Halima Okash amewasihi wananchi kumpigia kura nyingi Mgombea Urais Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli kutokana na wema aliowatendea.
Akizungumza wakati wa kampeni za lala salama katika Kata ya Kingale, Jimbo la Kondoa Mji, Okash aliwahimiza wanaKondoa na Watanzania kwa ujumla, kesho kutwa Oktoba 28, kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Dk. Magufuli na wagombea wote wa CCM.
Akitolea mfano wa wema wa Dk. Magufuli, alisema kuwa licha ya 2015 wanaKondoa kutompatia kura nyingi, lakini hakulipiza kisasi alitumia wema na busara zake kutowabagua kuwaletea maendeleo, hivyo wanastahili nao kumlipa kwa kumpigia kura nyingi.
"Nawasihi wanakondoa wenzangu tumlipe wema JPM maana 2015 hatukumpa kura nyingi lakini hakutususa alitupa maendeleo, ni Rais asiyebagua wala kuwa na kinyongo, wema aliotuonesha tumlipe kwa kumpigia kura nyingi kesho kutwa Oktoba 28,"alisisitiza Okash huku akipigiwa makofi ikiwa ni ishara kwamba wamekubaliana naye.
Okash alisema tatizo hilo halikutokea Kondoa tu, bali hata baadhi ya maeneo ya nchi, lakini kutokana na tabia yake ya kutokuwa na visasi wala kinyongo amewapelekea maendeleo, sasa wamekubali kulipa wema aliowafanyia kwa kuahidi kumpigia kura keshokutwa.
Alisema ndiyo maana kila kwenye mikutano yake ya kampeni mnashuhudia mafuriko ya watu wanaojitokeza kwenda kumsikiliza akimwaga sera za chama, akitangaza mafanikio ambayo serikali yake ya awamu ya Tano ilivyotekeleza na kuahidi kufanya maajabu mengine ya maendeleo kwa miaka mitano mingine endapo mtampatia ridhaa kwa kumpigia kura nyingi ashinde kwa kishindo.
Aliwakumbusha mambo makubwa yaliyofanywa katika kipindi cha miaka mitano cha Dk.Magufuli kwa mkoa wa Dodoma kuwa ni;Dodoma kutangazwa kuwa Jiji, kuwa makao makuu ya nchi, Rais kuhamia Ikulu ya Chamwino, serikali nzima kuhamia, Ujenzi wa Stendi ya Kisasa na Soko la Kisasa la Job Ndugai na Kondoa kunufaika na barabara ya lami ya Dodoma - Manyara.
Miradi mingine ni;Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR Dar- Dodoma, kuanza kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na kuanza ujenzi wa barabara za pete (Ringroads) kulizunguka jiji la Dodoma na hivi karibuni JPM ametangaza kujenga Uwanja Mkubwa wa Kisasa wa michezo.
Katika mkutano huo ambao aliutimia kuwanadi Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk Magufuli,Mgombea Ubunge wa Kondoa Mji, Ally Makoa na wagombea udiwani wa CCM, aliwahimiza wananchi siku hiyo ya Uchaguzi Mkuu kuwahi mapema kuwapigia kura wagombea hao na kurejea majumbani kwao.
Pia aliwaasa kutokuwa chanzo cha kusababisha vurugu kwani hata wasipokuwepo kwenye vituo, ulinzi wa uhakika wa kura zao upo kutokana na mfumo mzuri uliowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ushirikiano na serikali.
Pia alitumia wasaa huo kutoa elimu kidogo ya jinsi ya kupiga kura za Mgombea Urais wa CCM, wabunge na madiwani wa chma hicho, kwa kutia vizuri kwenye kiboksi alama ya vema na kwa wasiojua kusoma kuangalia alama ya CCM ya jembe na nyundo sambamba na picha za wagombea wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇