LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 5, 2020

MPANGO WA DUNDULIZA KWA HUDUMA ZA NHIF KUPITIA BENKI YA NMB WAZINDULIWA JIJINI DAR ES SALAAM, LEO

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga na Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Ruth Zaipuna, wakisaini mkataba wa NHIF  na benki hiyo kuendesha huduma ya Dunduliza ambayo mfuko huo umebuni ili mwananchi aweze kulipia huduma za bima ya afya kwa kulipia fedha kidogo kidogo kupitia simu ya mkononi. Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.


CCM Blog, Dar es Salaam

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Benki ya NMB umezindua mpango unaojulikana kwa jina la 'Dunduliza' unaomwezesha mwananchi kuweka fedha kidogo kidogo za mchango wa bima ya afya na hatimaye kufanikisha kuchangia kiwango kinachotakiwa na kujiunga na huduma za bima ya afya kupitia NHIF.


Uzinduzi wa mpango huo ambao uliambatana na kusaini makubaliano kati ya NHIF na Benki ya NMB ya namna wateja watakavyoweza kuchangia au kujiwekea fedha kwa ajili ya kukamilisha mchango wa huduma anazohitaji, umefanyika jijini Dar es Salaam, leo.


Akiuelezea mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga ambaye alitia saini na Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Ruth Zaipuna, alisema ni mpango ambao umelenga kuwawezesha wananchi kujiunga na huduma ya Bima ya Afya inayotolewa NHIF kwa Vifurushi kuweka fedha kidogo kidogo kupitia Benki ya NMB kwa muda atakaochagua na atakapokamilisha kiwango husika atapatiwa kadi ya matibabu na kuanza kunufaika na huduma za matibabu kupitia mfuko huo wa NHIF.


Konga alisema utekelezaji wa Mfumo huu kwa Mwananchi anayehitaji kujiunga na huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambaye atahitaji kuweka fedha kidogo kidogo kwa muda atakaochagua ni yule anajiunga kupitia mpango wa Vifurushi ambavyo vinajulikana kwa majina ya 'Najali Afya', 'Wekeza Afya' na 'Timiza Afya' ambavyo pia vinampa fursa mwananchi anayehitaji kuchangia kuchagua huduma kulingana na mahitaji yake, umri na wanufaika anaohitaji kuwajumuisha.


Alisema mpango huo unamwezesha mwananchi kujiwekea fedha kwa ajili yake mwenyewe, au kwa ajili yake na mwenza wake au kwa ajili yake, mwenza na mtoto au watoto alionao na kufafanua namna ya kujiwekea fedha kidogo kidogo akisema ni mfumo ambao ni rahisi kuutumia kwa kuwa unahitaji mtumiaji kuwa na simu ya mkononi ambayo siyo lazima iwe ya 'kupangusa' (smartphone).


Konga alitaja  hatua za kuzingatia kwa anayehitaji huduma hiyo kuwa ni zifuatazo:-  Utabonyeza *150*68#,  Utachagua namba 2 (Kibubu),  Utachagua namba 1 (Jisajili),  Utachagua namba 1 (Kukubali),  Kisha mfumo utakutaka kuingiza namba ya NIDA na kisha utaendelea na kufuata maelekezo unayopewa kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuanza kujiwekea fedha kidogo kidogo.


"Mfumo huu haubagui mwananchi yoyote kulingana na aina ya simu aliyonayo na endapo atakwama katika hatua za kujisajili anaweza kupiga simu bila malipo kwa namba 0800110063 na utapatiwa maelezo ya namna ya kufanya", alisema Konga.


Kuhusu manufaa  ya mpango huu kwa mkulima, Konga alisema, kuwepo kwa mfumo huo kunamwondolea mwananchi mzigo wa kulipa fedha zote zinazohitajika kwa mara moja hivyo inampa fursa ya kujipanga na kulipa kidogo kidogo kulingana na muda atakaochagua.


Alisema, mfumo huo hauna gharama yoyote kwa mtumiaji hivyo unamjengea mwananchi utamaduni wa ujiwekea akiba kupitia Benki na kumwezesha kunufaika na huduma za matibabu na huduma zingine za kibenki.


Konga alisema kuwa wakati NHIF inazindua mpango wa Vifurushi Novemba mwaka jana, changamoto iliyoonekana ilikuwa ni pamoja na uwezo wa wananchi kulipa fedha zote kwa awamu moja hatua iliyoifanya Menejimenti ya Mfuko kufungua milango na kuanza kushirikiana na wadau wa taasisi za kifedha kama Benki ya NMB ambayo alisema ina wigo mpana hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuwa na ofisi kila Wilaya.


“Lengo kubwa la mpango huu ni kumuwezesha mwananchi anayehitaji kunufaika na huduma za matibabu kupitia bima ya afya ili aweze kuweka fedha kidogo kidogo na hatimaye kupatiwa kadi yake ya matibabu na kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote,” alisema Konga.


Naye Mkurungenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna alisema kuwa anafarijika kuzinduliwa kwa mpango huu ambao anaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kuwa ndani ya mpango wa Bima ya Afya lakini pia kuwajengea wananchi tabia ya kujiwekea akiba kwa matumizi yenye manufaa ya baadae kwao.


“Afya ni kila kitu na hata kwa upande wetu sisi Benki ya NMB tunahitaji sana wateja ambao wana uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote na sio wa kuchukua akiba zao benki kwenda kujitibia, niombe sana wananchi tuutumie huu mpango kuhakikisha wengi wetu tunajiwekea fedha na hatimaye kupata kadi ya matibabu,” alisema Zaipuna.

 

HABARI KATIKA PICHA👇

Afisa Mkuu Masoko na Huduma  za Wateja  wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Andrew Singu akitoa maneno ya Utangulizi wakati wa hafla hiyo
Baadhi ya Maofisa wa Mfuko wa NHIF na NMB Bank wakiwa kwenye hafla hiyo
Mkurugenzi wa Wanachama wa Mfuko wa NHIF Christopher Mapunda akizungumzia faida za huduma aya Dunduliza, wakati wa hafla hiyo
Christopher Mapunda akifafanua zaidi kuhusu huduma hiyo ya Dunduliza
Baadhi ya Maofisa wa Mfuko wa NHIF na NMB Bank wakiwa kwenye hafla hiyo
Baadhi ya Maofisa wa Mfuko wa NHIF, NMB Bank na Waandishi wa habari wakiwa kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya Maofisa wa Mfuko wa NHIF na NMB Bank wakiwa kwenye hafla hiyo
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga akizungumza wakati wa hafla hiyo
Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Ruth Zaipu, akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga na Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Ruth Zaipu, wakibadilishana hati baada ya kusaini mkataba wa NHIF  na benki hiyo kuendesha huduma ya Dunduliza ambayo mfuko huo umebuni ili mwana
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga na Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Ruth Zaipu, wakipongezana baada ya kusaini mkataba wa NHIF  na benki hiyo kuendesha huduma ya Dunduliza ambayo mfuko huo umebuni ili mwana
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga na Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Ruth Zaipu, wakionyesha hati baada ya kusaini mkataba wa NHIF  na benki hiyo kuendesha huduma ya Dunduliza ambayo mfuko huo umebuni ili mwana





No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages