Baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya wa mwaka wa 2017, kulikuwepo na uhasama kati ya washindani na wafuasi kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.
Kwa upande mmoja, kwa sababu matokeo ya uchaguzi yalikuwa yamefutiliwa mbali na mahakama ya juu nchini Kenya na uchaguzi uliorudiwa ulisusiwa na Raila Odinga, kiongozi wa upinzani nchini Kenya. Baadaye, Rais Uhuru kuapishwa na kuingia ofisini, mahasimu wakuu wa kisiasa, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga waliamua kuzika tofauti zao na kukutana mnamo Machi 9, 2018 na kuorodhesha ajenda tisa kwa minajili ya kuboresha Kenya na siasa zake.
Hatua hiyo ilimaliza wasiwasi wa miezi kadhaa kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata, ambao mara kwa mara husababisha migawanyiko na kusababisha ghasia nchini Kenya.Kuundwa kwa Jopo la BBI
Viongozi hawa wawili walikubaliana kuunda kamati iliyolenga njia ya kumaliza hali hiyo ya ukosefu wa uthabiti.
Jopo hilo lililojulikana kama Building Bridges Initiative (BBI) lilipaswa kuangazia masuala tisa ikiwemo ukabila, ufisadi na ugatuzi - ikiwa ni miongoni mwa changamoto kuu tangu taifa kupata Uhuru mwaka wa 1963.
Ajenda za kuundwa kwa Jopo la Maridhiano(BBI) zilikuwa pamoja na jinsi ya kumaliza migawanyiko ya kikabila, kuwashirikisha watu wote kuhusu masuala ya utawala na siasa za Kenya, jinsi ya kushughulikia suala la kumaliza uhasama wa kisiasa unaotokea wakati wa uchaguzi mkuu, kuimarisha amani na usalama, kukabiliana na janga la ufisadi, kukabiliana na ukosefu wa maadili ya kitaifa, masuala ya majukumu na haki za raia, kuwajibika kwa pamoja na jinsi ya kuendeleza serikali za ugatuzi.
Jopo hilo ilikusanya maoni kutoka kwa Wakenya elfu saba na kuandaa ripoti ambayo ilizinduliwa na baadaye kuwasilishwa kwa Wakenya kwa mjadala zaidi ili kuiboresha, zao la ripoti ya sasa.
Ikiwa Wakenya watakubaliana na yaliyomo kwenye ripoti hiyo, huenda kura ya maoni ikaitishwa na kubadili katiba ya mwaka wa 2010 ambayo itasababisha mabadiliko katika muundo wa serikali.
Jambo hili ndilo limekuwa likiwatia kiwewe baadhi ya wanasiasa wa Kenya waking'ang'ania kuwa mchakato wa BBI na ripoti yenyewe ni mpango wa kisiri wa kumnyima naibu rais William Ruto kuwania na kushinda urais katika kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa 2022.
Ripoti ya jopo la maridhiano ina masuala na sifa kadhaa ambazo huenda zikabadilisha siasa na mfumo wa serikali nchini Kenya iwapo ripoti hiyo itaidhinishwa na Wakenya kwenye kura ya maamuzi.
Kupanuliwa kwa SerikaliRipoti iliyofanyiwa marekebisho ya BBI inapendekeza kupanuliwa kwa serikali ili kuhakikisha kuwa kila Mkenya anajumuishwa serikalini na kuondoa mtindo wa awali ambapo mshindi wa kiti cha urais anatwaa mamlaka yote.
Ripoti hiyo inapendekeza kubuniwa kwa afisi ya waziri mkuu na manaibu wake wawili. Aidha, inapendekeza kuwa mawaziri wanaweza kuteuliwa kutoka bunge la taifa pamoja na wataalam wengine kutoka nje ya bunge hilo.
Ripoti hiyo pia inapendekeza kurekebishwa kwa sura ya nane ya katiba kuhusu mfumo wa bunge na kuwarejesha maafisa wakuu wa serikali bungeni wakiwemo waziri mkuu, manaibu wake wawili, mawaziri, mkuu wa sheria na kiongozi mkuu wa upinzani.
Waziri mkuu anayependekezwa kwenye ripoti ya BBI atateuliwa na rais kutoka kwa chama au muungano wa vyama ambao una wabunge wengi zaidi katika bunge la Kenya. Ripoti hiyo pia inapendekeza kuongezwa kwa nyadhifa za uongozi katika ngazi ya kitaifa ili kuhakikisha kuwa jamii zaidi zinawakilishwa katika utawala wa nchi.
Suala la UwakilishiSiasa za migawanyiko ambazo zimekuwa kama desturi nchini Kenya wakati wa kipindi cha uchaguzi, huenda zikapungua iwapo mapendekezo ya ripoti iliyofanyiwa marekebisho ya jopo la mairidhiano, BBI yataidhinishwa na Wakenya.
Jopo hilo linataka sura ya saba ya katiba kuhusu uwakilishi kurekebishwa, ili kuhakikisha kuna uwazi na usawa katika mfumo wa uchaguzi, na pia kurekebishwa kwa mfumo wa usimamizi wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini, IEBC.
Aidha, jopo hilo linapendekeza mashindano ya kisiasa kuandaliwa kwa misingi ya sera, madili na utu, na wala sio chuki kama jinsi imekuwa mtindo wakati wa uchaguzi nchini Kenya.
Swala la uwakilishi wa kijinsia wa thuluthi mbili, ambalo limepiga chenga bunge kwa miaka kadhaa, pia limeangaziwa kwenye ripoti hiyo, kwa kutoa mapendekezo kadhaa. Swala hilo ni moja ya maswala tano muhimu ambayo jopo hilo limependekeza yafanyiwe marekebisho.
Uwajibikaji kwenye Idara ya Mahakama
Ripoti ya jopo la BBI ina baadhi ya mapendekezo kadhaa ambayo yatahitaji kushughulikiwa kupitia bunge. Jopo hilo katika kutayarisha miswada ya kurekebisha sheria husika, limeangazia maoni yaliyopewa kipa umbele wakati wa mchakato wa uhalalishaji wa ripoti hiyo.
Sura ya kumi inapendekeza kuwekwa mikakati ya kuhakikisha idara ya mahakama inawajibika kwa Wakenya. Hii inamaanisha kwamba ingawaje uhuru wa idara ya mahakama unalindwa, sharti iwajibikie Wakenya katika utekelezaji wa majukumu yake.
Hivyo basi, jopo hilo limependekeza kubuniwa kwa ofisi ya kusikiliza malalamiko ya umma kuhusu idara ya mahakama, ofisi ambayo itakuwa na mwakilishi katika tume ya huduma za idara ya mahakama(JSC).Hazina ya kustawisha wadi.
Ripoti ya BBI imetoa mapendekezo ambayo yanahitaji kuhusishwa kwa bunge hasa kuhusu wodi zote nchini Kenya. Kamati tekelezi ilizingatia maoni iliyokusanya na kuratibu miswada kadhaa muhimu ya marekebisho.
Miongoni mwa miswada hiyo ni mswada wa hazina ya kustawisha wodi mbalimbali katika kaunti wa mwaka wa 2020.
Malengo ya mswada huo uliopendekezwa ni kutoa mkakati wa kisheria wa utekelezaji wa hazina ya kustawisha wodi ambayo inalenga kuanzishwa kupitia marekebisho ya katiba. Muhimu ni kuwa ripoti hiyo pia inapendekeza nyongeza ya pesa kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi angalau asilimia 35, kutokana na akaunti za mwisho zilizokaguliwa na kuhakikisha kuwa wanaangazia utoaji wa huduma hasa watu wanaoishi katika mipaka ya mbali ya kaunti.
Kama njia ya kupigana dhidi ya ufisadi, ripoti ya BBI inapiga marufuku wafanyikazi wa serikali dhidi ya kufanya biashara na serikali na kupendekeza utekelezaji wa ripoti mbali mbali zilizotayarishwa miaka ya nyuma, hasa kuhusu ardhi. Pia, ripoti hiyo inapendekeza kusawazishwa kwa mishahara katika idara zote za serikali, mahakama, bunge na serikali pamoja na mashirika yote ya serikali na tume. Ili kuwezesha uchumi, ripoti hiyo inapendekeza mpango wa miaka 50 ambao utalenga viwanda na kilimo.
Ili kufikia haya, kuna haja ya kutekeleza sera ambazo zinawezesha kuanzishwa kwa biashara mpya na kuziendesha pamoja na kupunguza ushuru.
Kwenye mfumo wa utawala, ripoti hiyo inapendekeza Rais kumchagua Waziri Mkuu kutoka kwa chama chenye viti vingi bungeni ama muungano mkubwa bungeni ambaye atachukua nafasi hiyo baada ya kuidhinishwa na bunge.
Rais mwenyewe atachaguliwa na wananchi kwa kipindi cha miaka mitano(kisichozidi awamu mbili) na lazima apate asilimia 50 za kura na zaidi na asilimia 25 katika zaidi ya nusu ya kaunti 47 za Kenya.
Rais atasalia kuwa mkuu wa nchi, serikali na majeshi yote, huku waziri mkuu akipata nguvu za utendakazi kutoka bungeni na kusimamia shughuli za kila siku za serikali.
"Ndani ya siku fulani baada ya kuitwa kwa kikao cha bunge baada ya uchaguzi, Rais atamteua waziri mkuu mbunge wa bunge la kitaifa kutoka kwa chama cha kisiasa ambacho kina wabunge wengi zaidi, au kama hakuna chama kilicho na wabunge wengi zaidi, yule mbunge ambaye anaonekana kuwa na uungwaji mkono ya wabunge wengi kwenye bunge hilo," ripoti inapendekeza.
Aidha, baraza la mawaziri litajumuisha naibu rais, waziri mkuu huku mawaziri wakijumuisha wabunge na wataalam ambao, wengine watateuliwa kutoka nje ya bunge.
Waziri mkuu atakuwa kiongozi wa shughuli za bunge katika bunge la kitaifa.
Bunge la kitaifa litakuwa na wabunge 360 ikilinganishwa na 290 ilivyo sasa; huku wengine 70 zaidi wakichaguliwa kwa kufuata mfumo wa wingi wa idadi ya wapiga kura katika baadhi ya maeneo bunge huku seneti ikiwa na wabunge 94.
Pia, pendekezo jipya linamaanisha kwamba mabunge yote mawili hayatakuwa na wabunge wateule kama ilivyo sasa.
Ili kufidia zaidi sheria na uwakilishi mzuri wa kijinsia kwenye serikali, ripoti hiyo inapendekeza kwamba magavana na manaibu wao watawania viti wakiwa wa jinsia tofauti.
"Gavana atawania kiti akiwa peke yake bila naibu wake lakini ni lazima amteue naibu wake baada ya uchaguzi ambaye atakuwa wa jinsia tofauti naye," ripoti inapendekeza.
Kilicho wazi kwa sasa ni kwamba kiongozi wa upinzani Raila Odinga na naibu Rais William Ruto wako pande mbili tofauti kuhusiana na suala BBI. Kwa Raila, ripoti ya BBI inampa nafasi nzuri ya kurudi kwa shughuli za kisiasa baada ya kushindwa mara nne katika chaguzi za awali pamoja na uchaguzi wa mwaka 2017, matokeo ambayo aliyapinga mahakamani. Kwa upande mwingine, ni wakati mzuri kwa William Ruto kuondoka kwenye upande wa serikali na kurudia alichokifanya kwenye kura ya maamuzi ya mwaka wa 2010, ambapo alijijengea jina kwa kupinga katiba ya mwaka wa 2010.
Kati ya wanasiasa hawa wawili walio na ushawishi nchini Kenya, moja wao atapata mshtuko wa kisiasa.
Kimsingi, kampeini za BBI zinatoa nafasi mwafaka kati ya wanasiasa wawili wenye ushawishi nchini Kenya kuonyesha ni nani mwenye ushawishi zaidi na ni nani mwenye hafifu kisiasa. Ripoti ya BBI itasaidia pande zote mbili-upande wa Rais Uhuru Kenyatta na Raila na upande wa Ruto- kujipima kuhusiana na uchaguzi wa mwaka wa 2022.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇