Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli akizungumza katika Mkutano wake wa Kampeni za CCM uliofanyika leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
CCM Blog, Dar es Salaam
Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayetetea kiti hicho ili aendelee na awamu ya pili ya miaka mingine mitano, Rais Dk. John Magufuli ameunguruma leo katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa michezo wa Benjamin Mkapa na kutoa ahadi zenye neema tupu ikiwemo kuifanya Dar es Salaam, kuwa kama Ulaya.
"Mwaka 2015 nilipokuwa nikiwaomba mnichague, niliwaahidi kuwa nitajenga barabara za juu kwenye makutano ili kupunguza msongamano wa magari katika jiji hili la Dar es Salaam, wapo mliojiuliza kwamba hivi kweli itawezekana? Sasa baada ya miaka yangu mitano wenyewe mmeona imewekana, barabara hizo tumezijenga", alisema Dk. Magufuli katika mkutano huo ambao ulifurika maelfu kwa maelfu ya wananchi.
Aliongeza " Dar es Salaam ni mji muhimu sana, awamu inayofuata mkinichagaua tutajenga barabara nyingi za juu, tutajenga kila kwenye makutano ya barabadara kubwa na pia tutaongeza barabara za mwendo kasi katika maeneo mengi ikiwemo Mbagala. Tunataka Dar es Salaam hii iwe kama ulaya hata wakija wageni kutoka Ulaya wakifika wadhani bado wapo huko kwao".
"Nilimsikia mwanasiasa mmoja (siyo wa CCM), akisema eti barabara ile ya njia nane tunayojenga kutokea Ubungo eti ni pana sana. Sasa huyu majibu yake ni haya mawili tu.Tanzania kuwepo barabara pana sana siyo jambo la ajabu, kuna nchi huko ulaya ipo barabara yenye njia 40, lakini pia sisi tukiwa na barabara ambayo ni pana kuliko zilizopo kwingine kuna ubaya gani? Mbona Binadamu wa kwanza hakuzaliwa Tanzania, au mbona sisi tuna mlima Kilimanajro ambao haupo kwingine, na pia Tuna Tanzanite ambayo haipo kwingine Duniani mbona huyo hashangai?", alisema Dk. Magufuli akimjibu mwanasiasa ambaye hakumtaja, aliyetoa madai kwamba barabara ya njia nane inayojengwa kutoka Ubungo hadi Kibaha ni pana mno.
Akiomba kura kwa Wagombea wa Ubunge baada ya kuomba za kwake, Dk. Magufuli aliwataka wananchi wakiwemo wa vyama vyote kuwachagua wagombea hao wa ubunge na wa udiwani wa CCM ili kuja kurahisisha utendaji wake tofauti na kumchanganyia na wagombea wa Ubunge na Udiwani wa vyama vingine.
"Safari hii Wagombea hawa tuliowateua wote ni mahiri kabisa, ni wachapakazi, Halmashauri Kuu na Kamati Kuu tumehakikisha tunapitisha wale tunaowaona kuwa ni wachapakazi kweli kweli kwa hiyo nileteeni hawa", alisema Dk. Magufuli.
Akithibitisha jinsi CCM iliyokuwa imepania kuteua wagombea bora, wakati akimtambulisha mgombea Ubunge wa CCM katika Jimbo la Kawe, Akofu Josephat Gwajima alisema, " Huyu Gwajima alikuwa wapili kwenye kura za maoni lakini kwa kutambua kuwa ni mchapakazi na mkwel, nilimkata mtoto wa dada yangu ambaye ndiyo alikuwa ameongoza kwa kura, lakini nikaona uwezo wake haushindi wa Gwajima.
Mapema Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally alisema, mkutano huo wa leo ulikuwa wa kuzindua awamu ya tano ya Kampeni za CCM na kueleza matumaini yake kwamba baada ya uzinduzi huo kampeni zitazidi kuwa motomoto zaidi.
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli akizungumza katika Mkutano wake wa Kampeni za CCM uliofanyika leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇