Dar es Salaam, Tanzania
WENYEJI, Tanzania ‘Taifa Stars’ wakicheza pungufu kwa dakika 12 wamechapwa 1-0 na Burundi ‘Int’hamba Murugaba’ katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Kiungo wa Simba SC, Jonas Mkude alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 78 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kufuatia kumvaa na kumkunja Saidi Ntibazonkiza baada ya wawili hao kuchezeana rafu.
Ni kiungo huyo huyo wa FK Kaisar Kyzylorda ya Kazakhstan, Ntibazonkiza aliyeifungia Burundi bao hilo pekee dakika ya 86 akimalizia pasi nzuri ya mkongwe Cedric Amissi wa Al Taawon ya Saudi Arabia.
Ushindi huo kwa Burundi ni sawa na kulipa kisasi kwa Taifa Stars baada ya kutolewa katika mechi za kuwania tiketi ya fainali za Kombe ka Dunia Septemba 8, mwaka jana kwa mikwaju ya penalti 3-0 kufuatia sare ya jumla ya 2-2, timu hizo zikifungana 1-1 mara mbili Bujumbura na Dar es Salaam.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; David Mapigano, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdallah Kheri/Thomas Ulimwengu dk90+1, Bakari Mwamnyeto, Jonas Mkude, Said Ndemla/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk59, Feisal Salum/Muzamil Yassin dk76, Mbwana Samatta/Ally Msengi dk80 na Iddi Suleiman ‘Nado’/Ditram Nchimbi dk66.
Burundi; Onesime Rukundo, Eric Ndizeye, Frederick Nsabiyumva, Steve Nzigamasabo/ Cedric Dany Urasenga dk62, Said Ntibaronkiza, Saido Berahino/ Bonfilscaleb Bimenyimana dk72, Philip Nzeyimana, Nimubona Emery, Ndayishimiye Youssuf, Cedric Amissi na Mohammed Amissi/Bigirimana Blaise dk62.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇