LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 8, 2020

WAKULIMA WASHAURIWA KUPANDA MBEGU NA MAZAO YANAYOWEZA KUKOMAA KWA MUDA MFUPI KUTOKANA NA KUWEPO KWA KIPINDI KIFUPI CHA MVUA

 



**************************************

NA EMMANUEL MBATILO

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA imesema mvua za Vuli zinatarajia kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zitakazoambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.

Ameyasema hayo leo Mkurugenzi Mkuu TMA,Dkt. Agnes Kijazi  kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya TMA jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika Mkutano huo Dkt.Kijazi amesema Mvua za Vuli zinatarajia kuanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba mwaka huu katika maeneo ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki na ukanda wa Pwani ya Kaskazini pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.

Aidha Dkt.Kijazi amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa ushauri kwa kushirikiana na wadau katika sekta husika ili kukabiliana na athari mbalimbali zinazotarajiwa kujitokeza.

“Tunatarajia kwamba kutakuwa na Upungufu wa unyevunyevu katika udongo hivyo sekta husika inaweza kuangalia ni namna gani wanaweza kujiandaa vizuri kwaajili ya kukabiliana na visumbufu vya mazao na magonjwa mbalimbali ambayo yanajitokeza na ambayo yanatarajiwa kuongezeka.

Hata hivyo amesema wakulima wanashauriwa kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa ndani ya muda mfupi pia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi unyevunyevu na maji zinashauriwa kutumika.

Pamoja na hayo Dkt.Kijazi amesema kutokana na utabiri huo sekta ya usafirishaji inatarajiwa kunufaika hususani katika usafiri wa anga na nchi kavu.

“Sekta husika wanashauriwa kutumia muda huu kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji hasa kwa ujenzi unaohusisha maeneo yanayoathiriwa na mafuriko”. Amesema Dkt.Kijazi.



No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages