Kongamano la
wanachama wa Klabu za Biashara ‘NMB
Business Club’ Wilaya ya Ilala limefanyika jijini Dar es Salaam, huku Benki
ya NMB ikiwaongezea muda wa marejesho ya mikopo wanachama hao, kama unavyotaka
mwongozo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akifungua
kongamano hilo lililowaleta pamoja zaidi ya wafanyabiashara 100, Mkuu wa Idara
ya Biashara wa NMB, Alex Mgeni, alisema wanatambua ugumu wa mazingira ya
biashara waliyokumbana nayo wanachama wa klabu za biashara na wateja wao na kwa
kuheshimu mwongozo wa BoT, wameamua kuwapa nafuu hiyo ya marejesho.
Hata
hivyo, Mgeni alibainisha kuwa licha ya unafuu huo walioutoa, wanashukuru kwa
sababu mtiririko wa marejesho kwa wafanyabiashara na wateja wao umeendelea kuwa
vizuri, ambako asilimia 80 ya wakopaji wamelipa katika mifumo ya kawaida, jambo
linalothibitisha uimara wa mitaji yao.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa, aliwahakikishia washiriki kuwa Benki
yake iko imara licha ya mtikisiko wa COVID-19, huku akiitaja siri ya mafanikio
hayo kuwa ni uimara wa biashara mzunguko wa fedha wa wateja wao na wanachama wa
klabu hizo kote nchini.
Vilevile, Baragomwa
aliwapongeza wanachama wa Klabu za Biashara kwa namna walivyopambana na janga
la corona, huku akiwataka kuzungumza mara kwa mara na mameneja wa matawi ya NMB
yote nchini, kujadili changamoto zinazokwaza biashara zao ili wasikwame.
Kongamano hilo,
limetumka kunadi bidhaa mpya za NMB zilizoingizwa sokoni hivi karibuni, za Kadi
za Malipo ya Kabla (NMB Pre-Paid Card) na Kadi za Mikopo (NMB Credit Card),
sambamba na huduma nyingine kama NMB Nyanyua Mjengo, NMB BancAssurance na NMB
Mkononi.
NMB Business Club ni kongamano linalolenga
kuwaongezea elimu ya fedha na kubadilishana mawazo wafanyabiashara, sambamba na
Benki hiyo kupokea maoni na ushauri wao na kuvifanyia kazi ili kuharakisha
maendeleo ya wanachama wake, lakini pia kunadi bidhaa mpya za NMB.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇