Awali sikutaka kuandika chochote kufuatia makubaliano yenye faida za pande mbili kati ya Serikali yetu ya Tanzania chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli na Kampuni ya Madini ya Barrick.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza mahojiano ya BBC kuhusu tathimini ya kilichokubaliwa kulinganisha na kilichotarajiwa, sanjari na maoni ya baadhi ya Watanzania nimeona nichangie mjadala huu kwa mafungu 12;
# Kwanza ninaamini Watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi yao watakubaliana na mimi kuwa hatua zote alizochokua JPM kuikaba sekta ya madini ni kwa maslahi ya nchi na hivyo alichokuwa anafanya ilipaswa kuungwa mkono na kila aliyeamini kwamba tulikuwa hatupati ilivyostahiki.
#Hivyo haikuwa vita ya JPM na kampuni za madini bali Watanzania na kampuni za madini..
# Pili, Ninaamini kwamba tathimini ya kupima kushindwa au kushinda vita ya kibiashara ni kuangalia kama hatua zilizochukuliwa kwa ujumla wake zimeleta nyongeza ya tunachopata, tumebaki palepale au tumeshuka hata tulichokuwa tukipata awali.
#.Kifupi ningeweza kusema niishie hapa kwasababu wote tunakubaliana kwamba tunapata zaidi sasa kulinganisha na kabla. Ambacho ndio msingi wa kusema tumeshinda vita hii kwani hoja ya kwamba tulichotaka hatukupata kwa asilimia 100% haina msingi kabisa katika Sayansi ya majadiliano au mabishano ya kibiashara duniani.Ushindi ni kupata zaidi ya ulichokuwa nacho kabla ya majadiliano.
# Kwa mfano, Serikali kuanza kuendesha kwa ubia migodi ya Barrick Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga, Ni USHINDI! Kwasababu kabla ya JPM haikuwezekana!
# Serikali kuanza kumiliki hisa asilimia 16% za migodi ya Barrick nchini ni USHINDI. kwasababu kabla ya JPM haikuwezekana.
# Serikali kupata asilimia 50% ya faida za kiuchumi zitokanazo na uwekezaji wa Barrick ni USHINDI, kwasababu kabla ya JPM haikuwepo!
# Makubaliano ya kutenga $6 kwa kila 'ounce' ya dhahabu itakayouzwa kuwekwa mfuko wa maendeleo kwajili ya maeneo inakochimbwa dhahabu ni USHINDI, kwani kabla ya JPM haikuwezekana.
# Barrick kutenga dola milioni5 kuanza taratibu za kutengeneza kiwanda cha kuchenjua makanikia ili kitakapokamilika uchenjuaji wote ufanyike nchini ni USHINDI kwani kabla ya JPM hatukufika hapo!
# Kuongeza ukaguzi kwa sasa kuhusu makanikia yanayosafirishwa nje kwenye kipindi cha mpito kabla ya ujenzi wa Smelter ni hatua, ni USHINDI! kwani kabla ilikuwa holela!
# Tatu, Wapo wanaokosoa kwanini makanikia yaruhusiwe sasa kabla ya smelter kupatikana.Niwakumbushe tu sababu mojawapo ya kuzuia usafirishaji makanikia ilikuwa kukabili usiri na udanganyifu kuhusu kiasi cha madini, kitu ambacho sasa kinadhibitiwa na ukweli kwamba shughuli zote zinafanywa na kampuni ya TWIGA ambayo ni ubia kati ya Serikali na Barrick.
#Nne, Serikali kuwa sehemu ya mmiliki na msimamizi wa biashara yote inapunguza nguvu ya baadhi ya masharti likiwemo la kutumia bank za ndani kwajili ya kudhibiti usiri. Sharti la kutumika bank za ndani inabaki zaidi kwajili ya kuongeza biashara kwa Benk zetu na hivyo kupanua kufungamanisha biashara ya madini na sekta zingine kama bank.
#Tano, Malipo ya dola milioni 300 ambayo ilipangwa awali yalipwe kwa mkupuo lakin sasa yatalipwa kwa awamu sio kushindwa. Ni USHINDI bado kwani kabla ya JPM hatukustahili kulipwa chochote. Zaidi uamuzi wa Barrick kuanza kulipa dola 100m ( au zaidi ya shilingu 230bn ) ina mantiki kubwa kwasababu hatukuwa tunawadai kitu kabla ya JPM.
#Sita ; Hoja kwamba Serikali kupewa hisa asilimia 16% sio USHINDI kwakuwa kuna baadhi ya migodi Serikali inamiliki zaidi ya asilimia hizo haina msingi kwasababu kabla ya JPM ilijulikana tunamiliki hisa hizo katika migodi hiyo lakn haikusababisha Barrick ikubali kutupa hisa hata asilimia1%kwenye migodi inayomiliki .
#Zaidi ieleweke kwamba, umiliki wa Serikali wa hisa hizo kwenye kampuni za Mwadui, TanzaniteOne na Ngaka ni maamuzi yaliyofanywa na Serikali tangu mwanzo wa mkataba na sio kudai hisa kwa mkataba uliokwishaingiwa na kuanza kutekelezwa kwa miaka mingi kama ilivyo migodi ya Barrick nchini. Kifupi JPM ndio Rais wa kwanza kuishinikiza kampuni yenye mkataba na Serikali kwa miaka mingi kuachia sehemu ya hisa zake kwa Serikali.
# Saba :Kusema kwamba uamuzi wa Serikali kuruhusu Barrick isiorodheshwe soko la mitaji la ndani (DSE) ni kuwanyima watanzania umiliki wa asilimia 30% wanazopaswa kumiliki kwa mujibu wa sheria ya sasa ni hoja isiyo na nguvu sana kwasababu; Kwanza sheria haijasema watanzania tungemiliki hisa hizo bure bali kununua, kitu ambacho tangu sheria iruhusu mwaka 2017 kabla ya makubaliano haya imekuwa ngumu kwa watanzania kununua hisa hizo kutokana na uchanga wa sekta binafsi..
#Wakosoaji hawasemi tangu Waziri wa madini atunge kanuni za kutaka migodi iuze hisa asilimia 30% pale DSE ni watanzania wangapi wamejitokeza kununua wawe sehemu ya umiliki wa migodi hii.
# Msingi wa kutaka asilimia 30% ya hisa za migodi hii kuuzwa soko la mitaji ilikuwa ni pamoja na kutaka uwazi ktk gharama, mapato na faida ya uzalishaji ili kuwa na hakika ya kodi ya faida.
#Kwa makubaliano yalivyo sasa ambapo Serikali ni sehemu ya umiliki na uendeshaji kupitia kampuni ya TWIGA, ni wazi kusudi la uwazi linajibiwa kwani Serikali ni sehemu ya Bodi na nisehemu ya uendeshaji kupitia kampuni ya TWIGA na zaidi hata kusudi la umiliki wa Umma linajibiwa kwani Umma unakuwa sehemu ya wamiliki kupitia Serikali.
# Nikumbushe tu watanzania kwamba, ingawa Sheria ya madini ya 2010 ilitaka migodi kuuza hisa asilimia30% kwa Umma kupitia soko la mitaji la ndani (DSE), ukweli ni kwamba pamoja na uwepo wa sheria hiyo, kanuni kufanya sheria hiyo itekelezwe hazikutungwa na hivyo haikuweza kutekelezeka mpaka alipoingia JPM ambaye ndani ya mwaka mmoja ilitungwa kanuni kutekeleza.
# Hali ni hiyo hata kwenye sheria ya Posta na mawasiliano ya mwaka2010, ambayo ilitaka kampuni za simu ziuze hisa soko la mitaji la ndani ( DSE)ili watanzania wawe sehemu ya umiliki na kuongeza uwazi wa hesabu za kampuni za simu kudhibiti ukwepaji kodi. Sheria hiyo ya mawasiliano ya 2010 kama ilivyokuwa sheria ya madini ya 2010 nayo haikutekelezwa kwasababu Serikali alishindwa kutengeneza kanuni kutekeleza sheria hiyo.
#JPM alipoingia tu sheria na kanuni zikawekwa sawa ndani ya mwaka mmoja na kampuni za simu kama ilivyo kwa migodi zikatakiwa kuuza hisa asilimia 25% soko la ndani!
#Nane; Hoja ya inawezekanaje kuwepo makubaliano ya mgawo sawa wa faida za kiuchumi ( 50/50) katika makubaliano ya Barrick na Serikali ilhali Serikali inamiliki asilimia 16%. Nadhan ndio msingi wa kuitwa makubaliano kwani hata hisa za asilimia 16% Serikali imepewa bila kuchangia mtaji tofauti na kawaida. Ndio msingi wa makubaliano.
# Mgawanyo wa 50/50 faida za kiuchumi unahusisha hisa pamoja na vitu vingine kama ushiriki wa Serikali katika kulipwa madeni yaliyolimbikizwa ili kupunguza faida ya makampuni ya madini na kodi.
# Pia Serikali kupewa haki ya kuteua wajumbe wawili katika kila bodi ya wakurugenzi ya makampuni husika na pia kuteua Watanzania katika nafasi za juu katika menejimenti ya kila kampuni ni mambo ambayo ni vigumu kubeza kwamba haisaidii kudhibiti udanganyifu. Huu ni USHINDI. Kabla ya JPM hatukuwa na fursa zote hizi ambazo zinafanya Serikali kuwa sehemu ya kila kitu kuhusu uendeshaji wa migodi hii.
#Tisa ; Nirudie kusema kwamba " JPM is the Perfect President of our time "...tumuunge mkono hasa anaposimamia mabadiliko haya makubwa ambayo kwa tunaojua dunia inaendeleaje tunathubutu kusema anatoa kafara ya uhai wake kwa maisha ya Taifa hili.
#Nani asiyejua hatari ya vita hii ya rasilimali? Aliyekuwa Rais wa Irani Mohamed Mossadeq , alipinduliwa madarakani kwa njama za Shirika la Ujasusi la Marekani CIA baada ya kuchukua hatua kali dhidi ya Kampuni za mafuta mwaka 1951.
# Nisisitize tena na tena kwamba Dhamira ya JPM katika vita dhidi ya Ufisadi ni mtaji kwa Taifa hili. Wanaojua nchi hii na bara hili lilivyotafunwa wanaelewa ninachosisitiza.Bara hili kuna nchi wanahangaika na Viongozi wakuu wezi..Nani amesahau sakata la aliyekuwa Rais wa Nigeria, Abbacha kukutwa na fedha dola bilioni 3 alizopewa na kampuni za uporaji mafuta Nigeria? ( msome Ayittery 2016)
# Kumi; Niseme kwamba kazi ya ulinzi wa rasilimali inahitaji mkakati wa kivita.Ndicho alichofanya JPM ikiwemo kutunga sheria zile, ziliongeza msukumo na kuifanya Barrick waone kwamba wasingeweza kumaliza mgogoro ule kwa kupiga maneno tu. Lazma walegeze msimamo. Kampuni za kimataifa za madini, gesi na mafuta, kuna wakati wanaziyumbisha Serikali hata kwa kujifanya zinajitoa kwenye biashara ili Serikali ilainike na kujirahisi zaidi. Hivyo Serikali inaweza kutumia mbinu za kutunga baadhi ya Sheria kuongeza nguvu ya makubaliano ( bargaining power) ili kupata inachokitakata hata isipopata kwa asilimia100%.
# Kumi na moja, hoja ya kukubaliana mashauri ya migogoro baina ya kampuni na Serikali kuamuliwa na Baraza la kimataifa usuluhishi wa migogoro ya kiuwekezaji (International Arbitrations) badala ya mahakama za ndani sioni tatizo kubwa hasa kwa uzoefu niliopata kuona kwenye kesi ya IPTL na Tanesco, kwenye uamuzi wa mwaka 2014, ambapo Baraza la usuluhishi( International Centre For Settlement Of Investment Dispute- ICSID) lilifanya maamuzi wa kwa faida ya Tanzania lakini Mahakama Kuu ya Tanzania ilikuwa imeshafanya maamuzi kuumiza Tanzania kwa kwa jambo hilohilo Sept. 5,2013.
# Zaidi nafasi ya Barrick kushindwana na Serikali inapunguzwa na Serikali kuwa sehemu ya umiliki na uendeshaji kupitia kampuni ya TWIGA tofauti na mfumo wa awali.
#Kumi na mbili: Kimsingi uamuzi wa kuendesha kwa pamoja biashara za migodi hii kupitia kampuni ya TWIGA, Pamoja na mambo mengine ,inapunguza kwa kiasi fulani uzito wa hoja ya mikataba kupelekwa bungeni kulinganisha na hapo kabla kwani madai haya msingi wake mkubwa ilikuwa usiri na kutosimamiwa vema maslahi ya nchi kwenye mikataba husika.
# Hata hivyo, bado kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Mbunge yeyote anayo haki kupatiwa mkataba kwa mujibu wa kanuni za Bunge na anaweza kuwasilisha hoja bungeni kuhusu mkataba husika na ukaletwa bungeni kujadiliwa.
# Nilipata kutumia njia hiyo kupewa mikataba miwili, ule wa mwadui na wa kiwanda cha Chumvi Uvinza katika Bunge la10..
#Nidokeze pia kwamba Kumekuwepo mjadala mpana wa kisheria kwamba wabunge wakiwa sehemu ya kupitisha mikataba watapoteza nguvu yao ya kuisimamia Serikali mambo yakienda kombo katika mikataba waliyoshiriki.
#Ndio maana mabunge mengi duniani yamebaki na mamlaka ya kuhoji mkataba uliosaniwa lakin sio kuwa sehemu ya kupitisha au kuingia mikataba. Bunge kuwa sehemu ya kupitisha mikataba ni kujifunga. Kwani sio kweli kwamba Bunge litakuwa sahihi siku zote na kwa mambo yote. Hivyo ikitokea Bunge limekosea na kisha Serikali kusaini basi Bunge halitakuwa na uhalali wa kutumia mamlaka yake kikatiba kuiwajibisha Serikali katika jambo hilo..
# Nihitimishe kwa kusema kwamba kibano walichopata Barrick kwenye sakata hili hata biashara kusimama kwa takribani miaka miwili ni ushahidi wa ujasiri na uzalendo wa JPM kuhakikisha nchi inapata stahiki yake hata kama mikataba ilikuwa imeshafungwa. Kusimamisha Barrick miaka miwili kwa wanaoijua Barrick wanajua sio mchezo! Ziliundwa Tume nyingi huko nyuma na Barrick hawakuwahi kutikiswa kiwango hiki. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni! Tulichokipata ni USHINDI.
Ndio maana hata ukisoma ilani za ACT na CHADEMA, huoni ahadi na misimamo mikali dhidi ya wawekezaji sekta ya madini kwasababu vyama hivi vinajua haviwezi kuvuka alipoishia JPM!
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇