Mratibu wa Kongamano la Mtandao wa Wanawake Kunyanyuana Kiuchumi Mkoa wa Iringa, |
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Theresia Mtewele akiongoza kongamano la wanawake Mkoa wa Iringa lililoandaliwa na Mbunge Mteule wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Dk. Ritta Kabati (wa tatu kulia).
Na Mwandishi wetu, Iringa.
Wanawake wa mkoa wa Iringa wameweka azimio la kumchagua Rais Mteule anayetokana na Chama Cha Mapinduzi, Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na namna alivyowasaidia wanawake wa Iringa na Tanzania kwa ujumla katika sekta tofauti tofauti.
Wakizungumza katika kongamano lililoandaliwa na mbunge mteule wa viti maalum mkoa wa Iringa, Dkt. Ritta Kabati, Wanawake kutoka katika maeneo tofauti wamesema kwa sasa wanayohaja ya kuhakikisha wanamchagua Rais Magufuli kwa sababu amewasaidia kuboresha sekta ya afya, barabara,elimu na hata kuwainua kiuchumi kwa kuhakikisha halmashauri zote za mkoa wa Iringa zinatoa mikopo kwa kinamama, vijana na walemavu.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mratibu wa kongamano, Dkt. Ritta Kabati amesema miradi yote iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya tano ya Dkt. Magufuli inamchango mkubwa kwa maendeleo ya mwanamke huku akitolea mfano ujenzi wa barabara katika maeneo mengi mkoani Iringa zinazorahisha wanawake kufika hosptali kwa haraka na hata kufanya biashara kando kando mwa barabara hizo.
Dkt. Kabati amesema uamuzi wake wa kuandaa kongamano hilo lililokutanisha wanawake wote bila kujali vyama vya kisiasa wala dini ni pamoja na kuhakikisha wanawake wa mkoa wa Iringa wanatengeneza mtandao wa kunyanyuana kiuchumi na kifikra.
Nae mgeni rasmi katika kongamano hilo. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Theresia Mtewele amewataka wanawake wote kujitokeza katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu kwa kuwa ni haki yao kikatiba kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Bi. Mtewele amesema wanawake wa Iringa wanapaswa kujivunia uwepo wa Rais Dkt. Magufuli kwa kuwa amewaletea fedha za kujengea hosptali, vituo vya afya, pamoja na kutekeleza miradi mingine mingi mikubwa ya maji iliyoondoa adha ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Iringa.
Bi. Mtewele amewaomba wanawake wa Iringa kuhakikisha wanawachagua viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ambao ni rahisi zaidi kuwasiliana na Rais Dkt. Magufuli kuliko wagombea wa vyama vya upinzani ambao wamejikita katika harakati za Kitaifa na kuwaacha majimboni wakihudumiwa na wengine.
Kwa upande wake mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, amesema mwanamke ni nguzo kubwa katika amani ya jamii kwa kuwa mara zote amekuwa akijishusha katika mambo mbalimbali na hivyo kuleta amani.
Msambatavangu amesema wanawake wa Iringa wanakila sababu ya kuwachagua viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwa sababu katika kipindi cha miaka 5 iliyopita kimewahudumia vizuri na pia kimeonesha kutaka kuwahudumia vizuri kutokana na ilani ya chama hicho ya mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇