Gazeti la The New York Times limefichua kuwa Rais Donald Trump alilipa kodi ya mapato ya dola 750 tu mnamo mwaka aliochaguliwa kuingia madarakani na hakulipa hata senti moja katika miaka mingine kadhaa.
Ufichuzi huo ambao umepiga kama kimbunga yamkini utamuharibia sifa miongoni mwa wapiga kura wa kipato cha kati, na unaweza kumnufaisha mpinzani wake wa chama cha Demokcratic Joe Biden kwenye mkesha wa mdahalo wao wa kwanza kama wagombea urais wa Marekani.
Ufichuzi huu umekuja wakati mbaya kwa kampeni ya Trump, ambayo bado haijaweza kutoa jibu la kuridhisha kwa ukosoaji dhidi ya namna kiongozi huyo alivyolishughulikia janga la COVID-19. Vile vile unampa Joe Biden hatua ya kuanzia katika mashambulizi yake katika mdahalo baina yake na Trump utakaofanyika kesho Jumanne.
Tayari uchaguzi wa mapema umekwishaanza katika majimbo kadhaa ya Marekani kuelekea uchaguzi wa Novemba, na hali hii haimpi Donald Trump muda wa kutosha kujipanga upya.
Via: DW Swahili
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇