LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 20, 2020

DK. MAGUFULI KUCHANGIA MILIONI KUMI UJENZI WA KITUO CHA AFYA KAZURAMIMBA, KIGOMA, MIEZI MITATU BAADA YA UCHAGUZI MKUU


Mgombea Urais wa CCM Dk. John Magufuli

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Magufuli amesema baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu atachangia Sh. Milioni 10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kazuramimba mkoani Kigoma.


Dk.Magufuli ameahidi kutoa kiasi hicho cha fedha baada ya kufurahishwa na jitihada za wananchi wa Kazuramimba kuanza kukijenga kwa nguvu zao na kwamba ndani ya miezi mitatu baada ya kumalizika uchaguzi Mkuu Oktoba 28 , 2020 kitakuwa kimekamilika.


"Najua nitashinda Urais , hivyo katika kipindi cha miezi mitatu tutakuwa tumekamilisha ujenzi. Hiki ni kipindi cha kampeni hivyo nikitoa hizi hela ambazo nataka kuchangia watasema natoa rushwa, ndio maana nasema nitatoa baada uchaguzi kwisha.


Wananchi wa Kazuramimba umeonesha mfano mzuri sana kwa kuamua kuanza ujenzi kwa nguvu zenu, na wanasema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.Nami niwaahidi wananchi wa hapa nitachangia ujenzi wa kituo hiki cha afya," amesema Dk.Magufuli wakati akizungumza na wananchi hao wa Kazuramimba, leo Septemba 20, mwaka 2020.


Amesema mbali ya kukamilisha ujenzi, atapeleka dawa na vifaa tiba pamoja na watalaam ili kituo kianze kutoa huduma za matibabu na kwamba kiwe kinatoa na huduma za upasuaji."Tunataka hiki kituo cha afya kiwe kinafanya na operesheni."


Dk. Magufuli amesema kutokana na umuhimu wa kituo hicho, Waziri wa Afya ambaye atamteua kazi yake ya kwanza itakuwa ni kushughulikia kituo hicho ili kianze kazi ya kutoa huduma kwa wananchi hao.


Wakati huo huo Dk. Magufuli ameendelea kuzungumzia mkakati uliopo wa kuboresha miundombinu ya barabara ambapo amesema anataka mtu atoke Kazuramimba hadi Dar es Salaam na Kazuramimba hadi Tunduma bila kukanyaga changarawe.


Hata hivyo amewaambia wananchi hao kuwa miaka mitano aliwaomba kura na walimchagua yeye, mbunge na madiwani wa CCM na katika kipindi chote hicho wamefanya waliyoweza na wataendelea kutekeleza mengine yaliyobakia kwani maendeleo ni changamoto na changamoto zinatatuliwa moja baada ya nyingine.


"Wakati tuaomba kura hapa Kazuramimba hata umeme ulikuwa hakuna, leo upo.Hakukuwa na majengo lakini leo majengo yameongezeka na hata idadi ya watu imekuwa kubwa.Kazuramimba kuna wakazi zaidi ya 65000, mji ni mkubwa, mengine niachieni mimi.


Naomba mniamini,mnipe kura, najua katika mikakati ya kugombea ndani ya CCM walikuwepo wagombea wengi, hata aliyekuwa mbunge wa hapa naye alikuwepo wakati wa mchakato wa kura za maoni na yuko hapa leo ameniombea kura mimi,amemuombea kura mgombea ubunge Nashon, amewaombea kura madiwani wetu wa CCM," amesema.

Chanzo: Saidi Mwinshehe/Michuzi Blog/Tv Kigoma

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages