Akitangaza udhamini huo wenye thamani ya Shilingi
Milioni 40, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Klabu ya Gofu Lugalo, Mkuu
wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa NMB, Omary Mtiga alisema udhamini wao
unatokana na kutambua thamani ya michezo ikiwemo gofu.
Alisema ya kuwa, NMB kama taasisi kinara ya
kifedha nchini, inafurahishwa na aina ya ushirikiano uliopo kati yao na Klabu
ya Gofu Lugalo inayoandaa michuano hiyo na kwamba udhamini wao huo ni wa sita mfululizo
tangia mwaka 2014 na unaakisi nafasi ya Benki hiyo katika maendeleo ya michezo
Tanzania.
“Tunafurahishwa na aina hii ya ushirikiano
baina yetu na waandaaji, ambao hauishii tu katika kudhamini CDF Cup, bali pia
unaoifanya NMB kuwa na nyota wengi wa gofu wanaounda timu yetu, ambayo nayo
itashiriki michuano hiyo,” alisema Mtiga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu
Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo, aliishukuru NMB kwa namna
inavyojitoa katika kusaidia ukuaji wa michezo nchini, hasa CDF Cup
inayoratibiwa na kuendeshwa na klabu yake. Alisema
wanatarajia kuwa na washiriki wengi mwaka huu, kutokana na mwitikio aliouona,
kwani hadi wanakabidhiwa hundi ya udhamini na NMB, kuna jumla ya washiriki 110
waliojiandikisha, ikiwa imesalia wiki moja kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.
“Tayari washiriki 110 wamejisajili hadi sasa
kutoka klabu mbalimbali nchini, zikiwemo Lugalo, Dar Gymkhana, Arusha Gymkhana,
Zanzibar Gymkhana, NMB na nyinginezo, na tunatoa wito washiriki wajitokeze
zaidi na wazazi wawalete watoto wao kushiriki,” alisema Luwongo.
Naye nahodha wa Klabu ya Gofu ya NMB, Michael
Misabo, alisema kuwa nyota wa timu yake wako tayari kushindania na hatimaye
kutwaa ubingwa wa CDF Trophy, kwani wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha
wanafanya vyema katika kinyang’anyiro hicho.
“Katika CDF Cup 2020, NMB sio tu wadhamini
wakuu wa mashindano, bali pia ni washiriki tuliojiandaa kuchuana na tunaingia
tukiwa na uhakika wa kufanya makubwa na kutwaa ubingwa wa jumla,” alisema
Misabo mbele ya wanahabari waliohudhuria hafla hiyo.
Kwa upande wake, nahodha wa Klabu ya Gofu
Lugalo, Japhet Masai, alisema kama timu wamejiandaa vya kutosha na kwamba
maandalizi ya jumla ya michuano yanaendelea vyema na kwamba Ijumaa Septemba 18
kutafanyika utangulizi kwa nyota wa kulipwa kuchuana.
“Nyota wa kulipwa watatangulia kuchuana Ijumaa
ya Septemba 18, kisha ufunguzi rasmi Jumamosi na kuhitimisha michuano Jumapili
kwa nyota wa ngazi mbalimbal kutoana jasho katika Divisheni za A, B na C kwa
watoto, wanaume na wanawake, pamoja na nyota wa ridhaa,” alifafanua.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇