LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 24, 2020

SERIKALI KUWEZESHA USHIRIKI JUKWAA LA MAPINDUZI YA KIJANI KIGALI

 

Washiriki wa kikao maalumu
SERIKALI imewataka Watanzania kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya jukwaa la kilimo biashara linaloandaliwa na taasisi ya Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRF), litakalofanyika Kigali Rwanda Septemba mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Profesa Siza Tumbo kwenye mkutano wa maandalizi unaochagiza uandishi dokezo kwa ajili ya kutafuta uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya Kilimo ulioandaliwa na taasisi ya mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA) jijini Dar es salaam.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Profesa Tumbo alisema kwamba jukwaa hilo ni muhimu kwa ajili ya kutafuta uwezo zaidi katika uwekezaji na hivyo kukisukuma mbele zaidi Kilimo cha Tanzania.

 Profesa Tumbo alisema Serikali inapenda watanzania wanaotaka kushiriki katika jukwaa hilo  kuwasilisha mapema maombi yao AGRA na kwamba serikali itakaa na  taasisi hiyo kuona mahitaji halisi ya kitaifa katika hilo.

Naibu katibu Mkuu Kilimo, Profesa Siza Tumbo alisema kuna mambo mengi ambayo yanatoa fursa na yameshaanikwa katika ASDP 11 sehemu  ya tatu, na yako mambo yanaweza kufanyiwa kazi nchini na yapo ambayo tunahitaji uingizaji wa teknolojia mpya.

“Ningependa tukae na AGRA tuone, kama ulivyosikia katika mkutano kuna mahitaji mengi ya fedha ambayo yanaweza kupatikana hapa nchini, ni suala la kutambua na kujiongeza tu, lakini yapo mambo ambayo nchini hayapo kama teknolojia na hii lazimka watanzania tuamke na kuliona hilo” alisema Profesa Tumbo.

Katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa PASS (THE  PRIVATE AGRICULTURAL SECTOR SUPPORT – TRUST) Nicomed Bohay alisema taasisi yake kwamba ina uwezo mkubwa wa kuwekeza na kuweka dhamana, lakini maombi mengi yanayofika kwao yanakuwa yameaandikwa ndivyo sivyo.

Hata hivyo Bohay alisema tangu taasisi hiyo kuanzishwa mwaka 2000 hadi Machi 2020 imewafaidisha  watu 1,196,871 kwa kuwapa dhamana ya mikopo inayofikia bilioni 916 sawa na dola za Marekani milioni 400.

Aidha taasisi hiyo iliyoanzishwa kwa ajili ya kusaidia kuboresha sekta ya kilimo kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa kutoa yenyewe au kuwaunganisha wakopaji na mabenki ya biashara mwaka jana pekee iliwanufaisha  watu 226,689 kwa kuwapa dhamana au kuwapa fedha katika mikoa 26 nchini.

Pia kwa mwaka huo huo (2019)  PASS  ilidhamini mipango biashara 10,666 yenye thamani ya Sh bilioni 129 iliyofikishwa katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa ajili ya mikopo.

PASS ambayo inafanyakazi kwa karibu na  Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na taasisi ya utafiti wa wanyama nchini TALIRI imesema katika mkutano huo kwamba watashiriki katika jukwaa hilo kuona taasisi ambazo zinatafuta fedha kwa ajili ya wakulima wadogo, kuangalia wawekezaji wanaotaka kuona mfumo unaofaa kwa ajili ya kuwezesha kusaidia wakulima wadogo na wale wanaotaka kutoa fedha kwa ajili ya  kusaidia ukuaji wa kilimo biashara nchini Tanzania.

Jukwaa la  AGRF  ndio  jukwaa kubwa la kilimo barani Afrika likiwakusanya wadau mbalimbali ili kuchukua hatua za kiutendaji zitakazoweza kusukuma mbele kilimo barani Afrika.

Mkurugenzi wa AGRA nchini Tanzania Vianey Rweyendela
Mkurugenzi wa AGRA nchini Tanzania Vianey Rweyendela


Jukwaa la mwaka huu litaendeshwa kwa njia ya mtandao kuanzia Septemba 18-11 kutoka Kigali Rwanda kutokana na janga la covid-19.

Watu zaidi ya 4000 wanatarajiwa kushiriki wakiwemo viongozi wa kitaifa, mawaziri, wadau mbalimbali wa kilimo na watu binafsi.

Mkurugenzi wa AGRA nchini Tanzania Vianey Rweyendela akizungumza katika mahojiano alisema kwamba anatarajia ushiriki wa Tanzania mwaka huu utakuwa mkubwa hasa ukizingatia muitiko wa mkutano wa maandalizi ambao ulikusanya wadau wengi wakiwemo viongozi wa serikali wasimamizi wa sera na waratibu, mabenki, taasisi binafsi za Kilimo na pia makampuni yanayojihusisha na Kilimo.

Aidha alisema kuwapo kwa Kituo cha Uwekezaji nchini TIC katika mkutano huo ni ishara tosha kwamba maandalizi yanakwenda vyema.

Alisema TIC ndio inayojua fursa za uwekezaji zilizopo nchini hivyo wao wanakuwa rahisi kuwaweka pamoja watanzania wote wanaotaka kushiriki  na pia wao wenyewe kueleza mataifa mengine nini kilichopo nchini na nini watakipata wakiamua kuwekeza nchini.

Awali katika mkutano huo, Mwakilishi wa TIC, Diana Ladislaus Mwamanga  alisema kwamba Tanzania ina fursa tele za uwekezaji hasa kwenye Kilimo na mifugo.

Alisema kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji ikiwamo kuondolewa kw atozo na kubadilishwa kwakanuni za uvuvi bahari kuu ni  miongoni mwa mianya inayostahili kutumika kuvutia uwekezaji.

Alisema wote watakaofanikiwa kuandika miradi wanapaswa kuelewa kubadilika kwa mazingira ya uwekezaji na vivutio lukuki vilivyowekwa kwa wanaotaka ushirika au kuwekeza moja kwa moja.

Alisema katika muda wa kufanya mauzo (Agribusiness Deal Room) ili kupata biashara mpya wawekezaji  watanzania wanapaswa kuelewa kwamba zipo sababu sita za kufanikisha mauzo hayo.

Alisema taifa ni salama lenye amani likifuata mfumo wa demokrasia ya vingi na kwamba uchumi wetu unakua na  tuko salama kutokana na  kuwa na utulivu muda wote hata wakati na baada ya uchaguzi.

Pia ukuaji wa uchumi uko vizuri  kwani mfumuko wa bei ni mdogo kuna ujazo mkubwa wa raslimali zikiwamo za utalii kama mbuga na pia  maeneo makubwa ya ardhi yanayofaa kwa ajili ya kilimo. Pia Tanzania ina gesi ya asili na ni sehemu muhimu ya kuwekeza kutokana na mazingira yake kubwa bora.

Pia Tanzania ipo kimkakati ikiwa inazungukwa na mataifa manane na bandari kuu tatu zinazohudumia nchi 6, viwanja vya ndege vya kimataifa vitatu na soko la watu milioni 177 kwa Afrika mashariki, SADC watu milioni 342, ikiwa na watu milioni 650 soko la TFTA na soko la AGOA lenye bidhaa 6000. Pia lipo soko la EBA (Ulaya).

Alisema  vyote hivyo ukichangia na msamaha wa kodi watanzania wanaweza kuzungumza kwa uhakika na wawekezaji kutoka nje kwa lengo la kuingia ubia au kuzalisha wao wenyewe bidhaa zinazoleta faida katika mnyororo wa Kilimo na ufugaji.

Naye Dk Nandonde mratibu wa ASDPll, alisema kuwa Kilimo kina nafasi kubwa ya uwekezaji na kwa sasa kipengele namba tatu pekee ina fursa za miradi ya thamani ya dola bilioni 2.5.

Alisema jukwaa lijalo likitumika vyema linaweza kuusukuma mbele utekelezaji wa ASDP ll.

Kuhusu kilio kwamba  sheria zimekuwa kikwazo katika kilimo na pia mifugo, Mkurugenzi wa sera Wizara ya Mifugo na uvuvi Dk Komba alisema kwamba ni vyema watu wakaangalia mabadiliko makubwa yaliyofanya katika kuwezesha uwekezaji na wasibaki wakikariri mambo ya zamani.

Alisema kwa serikali imefuta zaidi ya tozo 105 huku ikibadili kanuni kuwezesha uvuvi wa bahari kuu kuwa wazi kwa wenye uwezo.

 Alisema hotuba ya bajeti ya wizara ya mipango na fedha ya mwaka huu imeiainisha wazi tozo zilizofutwa na mabadiliko yaliyofanywa kuwezesha uwekezaji kuwa rafiki.

Alisema katika jukwaa ni vyema ikaangaliwa teknolojia itakayowezesha uvuvi wa kina kikuu ambao kwa sasa watanzania wengi hawamo.

Alisema mabadiliko yaliyofanywa sasa yatawezesha sekta ya Kilimo na mifugo kukua kwa kuwa nafasi zipo na fursa za uwekezaji ni rafiki zaidi.

Wazungumzaji wengine katika kikao walifafanua kwamba kuna shida sana ya upatikanaji wa chakula cha mifugo na hali hiyo inahitaji pia kuangaliwa.

Hata hivyo wapo waliozungumza kuhusu teknolojia na kusema teknolojia iliyopo sasa ya ukamuaji mafuta ya alizeti inaacha mafuta mengi katika mashudu na watu wa Kenya wanayachukua na kwenda kurekebisha kabla ya kutengeneza chakula kizuri cha mifugo.

Shida ya chakula cha mifugo ilielezwa pia na mwekezaji mkubwa Afrika Mashariki wa kuku, AKMG , Elizabeth Swai ambaye alisema  kuna ushindani mkubwa wa nafaka hasa mahindi ambapo yanahitajika kwa binadamu na pia kwa wanyama.

Aidha alisema kwamba ipo haja  kwa nchi kuongeza  Kilimo cha mahindi hasa ya njano kwa ajili ya  mifugo na poia maragawe aina ya soya, mtama na uwele.

Naye mwakilishi wa Sekta binafsi ,TPSF, Victoria Michael alihimiza sekta binafsi kutumia jukwaa kwa ajili ya kutafuta mitaji na teknolojia kwa kuwa fursa nchini ni nyingi hasa kwenye Kilimo.

Aidha Victoria aliwataka watu binafsi kuhakikisha kwamba wanaingia katika  uwasilishaji wa dokezo sabilia (pitching) yenye uhakika ili kuweza kukidhi haja na hivyo kuvutia wawekezaji.

Kwa mujibu wa Donald Mizambwa, Ofisa wa AGRA nchini Tanzania anayeshughulikia kampeni kuelekea Jukwaa Septemba mwaka huu  alisema  Jukwaa hilo lina mambo mengi ya kufanya na kujadiliana.

Aidha alivitaja vipengele vitakavyokuwepo katika jukwaa hilo kuwa pamoja kuwezesha kuwapo kwa mazungumzo ya uwekezaji: pia watakutanishwa kati ya watu wenye mitaji na watafuta mitaji kuanzia dola 500 hadi dola milioni 50. Pia kutakuwepo na mawasiliano kati ya nchi   na washirika muhimu na wafanyabiashara na pia  wakulima kuunganishwa na wafanyabiashara wa mazao yao.

Pia alisema kutakuwa katika jukwaa la majadiliano ya wataalamu katika masuala ya kitaaluma yanaohusu Kilimo biashara na uwekezaji.


-- It is my pleasure to work with you, please visit 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages