LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 14, 2020

RAIS DK. MAGUFULI AHUTUBIA MKUTANO MKUU WA KANISA LA TAG, AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUWAHIMIZA WAUMINI KUSHIRIKI KATIKA UCHAGUZI MKUU KWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA

Rais Dk. John Magufuli akizungumza kwenye Kilele cha Mkutano Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) katika Ukumbi wa Chuo cha Biblia Miyuji, jijini Dodoma leo. (Picha na Ikulu)


Ikulu, Dodoma

Rais Dk. John Magufuli amewaomba viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini kuwahimiza waumini na Wananchi kwa jumla kushiriki katika uchaguzi Mkuu hasa kwa kupiga kura kwa amani na utulivu, na kuwataka viongozi wa vyama vya Siasa kutotumia matusi au kusababisha vurugu wakati wa uchaguzi mkuu huo.


"Kwa bahati nzuri uchaguzi hautafanyika Ijumapili wala Jumamosi wala Ijumaa, utafanyika siku ya kazi (Jumatano), kwa hiyo nina waumini wa madhehebu yote hamtazuiwa na kufanya ibada hivyo nawaombeni sana mjitokeze kupiga kura ili tuweze kupata viongozi watakaotufaa katika taifa letu", Alisema Rais Dk. Magufuli.


Amewataka pia pamoja na kushiriki katika uchaguzi huo kumuomba Mungu ili aweze kuwapatia viongozi wenye maono, wachapa kazi na wazalendo kwa Taifa ili wasiangukie kwa viongozi wabadhilifu, wabinafsi au vibaraka kwa kuwa kazi yao itakuwa ni kubomoa badala ya kujenga.


Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo alipokuwa akizungumza katika Mkutano Mkuu na Baraza Kuu la Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililojumuisha Maaskofu na Wachungaji wa Kanisa hilo wa nchi nzima, waliokutana katika ukumbi wa Chuo cha Biblia Miyuji Jijini Dodoma na kulipongeza Kanisa hilo kwa huduma nzuri ya kiroho linayoitoa kwa Waumini wake na kwa mchango wake katika utoaji wa huduma za kijamii kwa Watanzania bila kubagua.


Pamoja na kulipongeza Kanisa la TAG, Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu ambao upo kwa mujibu wa Katiba na itaendelea kutoa ushirikiano katika juhudi mbalimbali za kanisa hilo kuhudumia jamii ikiwemo ujenzi wa Chuo Kikuu Jijini Dodoma ambapo amemuagiza Mkuu wa Mkoa Dk. Binilith Mahenge kuhakikisha mpango huo unafanikiwa na uwekezaji mwingine wowote ambao Kanisa hilo litaona inafaa kuufanya.


Ameelezea kufurahishwa na kusanyiko la Maaskofu na Wachungaji takribani 4,000 waliohudhuria mkutano huo uliodhihirisha uwepo wa Mungu na amewashukuru viongozi hao kwa kazi kubwa wanayoifanya kuliombea Taifa na kutoa huduma za kijamii kupitia shule na vyuo, vituo vya watoto yatima na watoto wa mitaani, miradi ya maendeleo na visima vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.


Rais Magufuli amemshukuru Askofu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la TAG ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Assemblies of God Barani Afrika, Dk. Barnabas Mtokambali na Waumini wa Kanisa hilo kwa kumpa Ngao ya Tuzo ya Uongozi thabiti wa kumtanguliza Munguwakati wa mapambano thidi ya Ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona huku akisema kuwa Tuzo hiyo inamstahili Mwenyezi Mungu ambaye amesikiliza maombi ya Watanzania na kuepusha madhara ya janga la Corona ambalo limeleta taharuki kubwa duniani.


Rais Magufuli amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuibariki Tanzania ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ameweza kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa ajili ya Watanzania ikiwemo kuboresha huduma za jamii kama Afya, Maji na Elimu na kujenga miundombinu  ya barabara, madaraja, umeme, reli na majengo.


Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway – SGR) ya Dar es Salaam – Morogoro – Makutupora, kufufua reli ya Kaskazini ya Dar es Salaam – Tanga – Moshi – Arusha, mradi wa ujenzi wa Bwawa la Nyerere kwa ajili ya kuzalisha megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji, usambazji wa umeme vijijini ambao umefikia asilimia 85 na jukumu zito la kuhamisha makao makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.


Mapema katika mkutano huo Askofu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la TAG ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Assemblies of God Barani Afrika, Dk. Mtokambali alimkabidhi Rais Magufuli tuzo ya TAG ya kutambua namna alivyoliongoza Taifa kumtegemea Mungu katika kipindi kigumu cha janga la ugonjwa wa Corona (Covid-19).


Pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kumuomba Mungu badala ya kuwafungia watu majumbani, Baba Askofu Mkuu Dk. Mtokambali amesema muongozo wa Rais Magufuli wakati wa janga la Corona pia umesaidia kuokoa madhara katika uchumi kutokana na kuwahimiza wananchi kufanya kazi na kuongeza uzalishaji.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages