Benki ya NMB yatangaza neema kwa wachimbaji wadogo
Benki ya NMB imetenga shilingi bilioni 32 kwa ajili ya mikopo kwa
wachimbaji wadogo nchini. Akizungumza jijini Mwanza wakati wa kongamano la wafanyabiashara
‘NMB Business Club’, Mkuu wa idara
ya Biashara wa Benki hiyo - Alex Mgeni alisema kutolewa kwa mikopo hiyo ni
matokeo ya maboresho ya sheria na sera kwenye sekta ya madini yanayofanywa na
serikali kwa lengo la kuongeza tija.
“Mikopo hiyo ambayo imeanza kutolewa tangu Januari, mwaka
huu inahusisha gharama za kununua vifaa vya uchimbaji ikiwemo mitambo na
magari ya kubebea mchanga wa madini migodini,”
alisema Alex.
Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB - Alex Mgeni,
akizungumza kwenye kongamano la biashara (NMB
Business Club) Jijini Mwanza lililoratibiwa kwa ajili ya kuwafunda
wafanyabiashara zaidi ya 200 kuhusu huduma za kifedha na faida za kutumia
huduma za benki hiyo.
Kuhusu madhara ya janga la corona kwa sekta ya biashara, Mgeni
alipongeza juhudi za Serikali zilizofanikisha kutokomezwa kwa ugonjwa huo
uliosababisha changamoto katika mfumo wa biashara na uwekezaji. Alisema
kutokana na mifumo ya biashara kupata changamoto, NMB iliwasaidia wateja wake
ambao biashara zao ziliathirika zaidi, hasa wale wa sekta ya utalii.
“Kila mfanyabiashara aliyepata changamoto na kutifikia
tulizungumza naye kutafuta namna ya kumsaidia. Wapo waliopunguziwa viwango vya
marejesho na wengine marejesho yao yalisimamishwa kwa muda, hasa wale wa sekta
ya utalii walioathirika zaidi,” alisema.
Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa - Baraka Ladislaus, akipata maelezo
kutoka kwa msindika mvinyo - Rose Stephen, kwenye kongamano la wafanyabiashara
Jijini Mwanza.
Akizungumzia NMB Business Club, Meneja wa NMB Kanda ya
Ziwa - Baraka Ladislaus alisema kongamano hilo linatoa fursa kwa benki
kusikiliza, kupokea na kufanyia kazi hoja za wateja.
“Kupitia hoja na mrejesho kutoka kwa wateja wetu wakiwemo
wafanyabiashara, NMB tunapata fursa ya kuboresha huduma na bidhaa zetu,”
alisema Ladislaus
Mfanyabiashara, Contilda Magweti wa jijini Mwanza alisema licha ya
kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara, kongamano hilo la kila mwaka katika
maeneo mbali mbali nchini pia huwapa fursa ya kukutana na kujadiliana uso kwa uso
na viongozi na watendaji wa Benki.
“Kwa kukutana pamoja tunapata fursa ya kujadiliana na kubadilishana
uzoefu kibiashara; NMB iangalie uwezekano wa kongamano hili kufanyika angalau
mara mbili kwa mwaka,” alisema Magweti
Aliwashauri wafanyabiashara na wajasiriamali wenzake kuendelea
kusaidiana maarifa ya kutafuta masoko ya bidhaa zao kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇