Katibu Mkuu Kusaya akisaini kataba wa makubaliano baina ya wizara ya kilimo
Katibu Mkuu Kusaya akitoa maelezo namna ambavyo wizara itatekeleza makubaliano hayoKatibu
Mkuu wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akiwa pamoja na Mkurugenzi wa
World Vegetable Center wakionesha mkataba huo baada ya kusaini.
*********************************
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya leo (tarehe 20/07/2020 ) amesaini mkataba wa
makubaliano kati ya Wizara ya Kilimo na World Vegetable Center ili
kuboresha utafiti na uendelezaji wa mazao ya mboga mboga ili kusaidia
kuboresha lishe na kuongeza usalama wa chakula.
Mkataba wa makubaliano umesainiwa
Jijini kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya kwa niaba ya
serikali na Dkt.Gabriel Rugalema Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki
na Kusini (avrd-World Vegetable Center).
Makubaliano hayo yapo katika
maeneo makuu matatu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji, uchakataji na
utunzaji wa mbegu za mazao ya mboga mboga kwa ajili ya matumizi ya
kisayansi kwa sasa na vizazi vijavyo.
Eneo la pili la makubaliano ni
utafiti wa mbegu bora zenye kuhimili ukinzani wa magonjwa, wadudu, na
hali ya hewa kama vile ukame, mafuriko na mabadiliko ya tabia nchi kwa
ujumla na tatu kujenga weledi wa wana sayansi, maafisa ugani kilimo,
wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya kilimo na wakulima kuhusu mbinu bora za
kilimo.
Teknolojia mpya na kilimo biashara kufuatana na matakwa ya
Serikali na wadau wengine.
Aidha, Kusaya amesema kuwa
makubaliano ya ushirikiano huu ni mwendelezo wa makubaliano ya
ushirikiano kati ya serikali kupitia Wizara ya Kilimo na AVRDC- World
Vegetable Center iliyoanza mwaka 1992 ambapo kwa wakati huo Serikali
ilikubali kuanzisha kituo cha utafiti wa mboga mboga Tengeru mkoani
Arusha kwa niaba ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC).
“Kupitia makubaliano haya,tutaweza
kutumia fursa hii kuimarisha utafiti wa mazao ya mboga mboga na
kuongeza ujuzi na weledi wa wataalam wetu ikiwa ni pamoja na wanafunzi
wa vyuo vyetu vya kilimo ili sekta ya mboga mboga ichangie ipasavyo
katika uongezaji tija na kuchangia pato la Taifa” alisema Kusaya.
Kusaya amesema Wizara yake ina
vyuo vya mafunzo ya Kilimo 14,taasisi za utafiti wa Kilimo 17 na vituo
mahususi 18 ambavyo kupitia ushirikianao huu vitaweza kutumika kuzalisha
mbegu bora za mazao ya horticulture na kuwafikia wakulima kote nchini.
Hata hivyo Kusaya ametoa wito kwa
wakurugenzi wa Wizara ya Kilimo kusimamia yale yaliyoko kwenye mkataba
na kuhakikisha yanatekelezwa ipasavyo.
“Ili hili lifanyike ningependa
kuwepo kamati ndogo ndogo hapa Wizarani itakayofuatilia utekelezaji wa
makubaliano haya na makubaliano mingine ya aina hii, ninawataka idara
zinazohusika kushirikiana na TARI na TPRI kuandaa mpango kazi wa
utekelezaji” alisema Katibu Mkuu Kusaya.
Naye Mkurugenzi wa World Vegetable
Center Dr. Gabriel Rugalema amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1997
hadi 2018 wameweza kuzalisha aina 18 za mbegu bora za mazao tofauti (nyanya,ngogwe,mchicha,mnafu,figiri au loshuu)
“ Mbegu za nyanya tu zinakadiriwa
kuchangia Dola za Kimarekani milioni 250 katika uchumi wa Tanzania kwa
miaka mitano iliyopita pamoja na kuongeza ajira na pato la familia”
alisema Dkt.Rugalema.
Aliongeza kusema jumla ya wataalam
400 kutoka nje ya nchi waliopata mafunzo kati ya mwaka 1998 na 2018 na
wataalam zaidi ya 2000 kutoka ndani ya nchi wamepatiwa mafunzo kati ya
mwaka 1994 hadi sasa.
AVRDC kupitia kituo chake cha
World Vegetable Center kilichopo Tengeru Arusha kimefanikiwa pia
kufundisha zaidi ya wakulima 200,000 Tanzania Bara na Visiwani elimu juu
ya mazao ya mboga mboga ili kuinua uzalishaji wake na kuongeza kipato
cha wakulima.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇