Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Temeke Ramadhan Ndwatah akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo.
…………………………………………………………..
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa
Temeke imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni 79, 540, 500
kutokana na kufanya uchunguzi sehemu mbalimbali ikiwemo fedha za SACOSS,
Mfuko wa Jimbo pamoja na risiti zilizoghushiwa.
fedha hizo zimeokolewa katika kipindi cha cha mwezi April hadi
Juni mwaka huu wakati TAKUKURU ikiendelea na majukumu yake ya kuzuia na
Kupambana na Rushwa kwa mujibu wa sheria namba 11 ya mwaka 2007.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Temeke Ramadhan Ndwatah, amesema kuwa wakati
wanatekeleza majukumu wamepokea taarifa 103 zinazohusu vitendo vya
rushwa.
Ndwatah ameeleza kuwa katika kipindi hicho Manispaa ya Temeke
pamoja na taasisi binafsi zinaongoza kwa kulalamikiwa na kufanikiwa
kufunguliwa majalada mapya ya uchunguzi yaliyofunguliwa na kufikia hatua
za uchunguzi wa kina yapo 15, huku majalada mengine yanaendelea na
uchunguzi katika hatua mbalimbali.
Amefafanua kuwa katika kesi ya kwanza inamhusu Bw. Elias
Mtarawanje ni Diwani wa Kata ya Kijichi ambaye alifikishwa mahakamani
kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 1,000,000 ili amsaidie mtu
aliyetakiwa kulipwa fidia ya kiwanja, kinyume na kifungu cha 15 (1) (a)
cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kesi ya pili Bw. Ally Mtiga ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Tambukareli
alifikishwa mahakamani kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya
utanganyifu kwa mwananchi ili aweze kumsaidia kupata leseni ya makazi.
kesi ya tatu Sophia Milanzi ni Afisa Mtendaji Mtaa wa Kizinga
alifikishwa Mahakamani kwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 50,000 kutoka
kwa mwananchi ili ampatie huduma ya kubadili jina kwenye rejesta ya
makazi.
Kesi ya nne Moris Sendi ni Afisa Mtendaji Mtaa wa Rangi Tatu
alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa Sh. 70,000
kwa ajili ya kumsaidia mwananchi aendelee kufanya biashara eneo la
Rangitatu.
“TAKUKURU inaendelea na kujumu la kuelimisha umma kupitia njia
mbalimbali, lengo ni kuhakikisha wananchi wanashiriki kwa vitendo katika
mapambano dhidi ya rishwa” amesema Bw. Ndwatah.
Katika hatua nyengine Bw. Ndwatah amesema kuwa katika kuelekea
uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, wamejipanga kwa
kuendelea kuelimisha umma kupitia njia mbalimbali ikiwemo kufanya
mikutano ya hadhara, semina kwa wagombea pamoja mawakala ili kudhibiti
vitendo vya rushwa katika kipindi cha uchaguzi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇