Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizindua Jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na viongozi wengine eneo la Ndejengwa mkoani Dodoma leo Jumatano Julai 22, 2020
Jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi eneo la Ndejengwa mkoani Dodoma leo Jumatano Julai 22, 2020
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 22
Julai, 2020 amezindua majengo 2 ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
yaliyopo Jijini Dodoma na Chamwino.
Jengo
la NEC lenye ghorofa 8 limejengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia shirika
lake la Suma-JKT katika eneo la Njedengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 12.3
baada ya kupokea kazi hiyo kutoka kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)
waliokuwa wametumia shilingi Bilioni 4.2
Jengo
la ofisi ya TAKUKURU Chamwino ambalo ni moja ya majengo 7 yaliyojengwa katika
wilaya 7 hapa nchini, limejengwa kwa utaratibu wa ‘Force Account’ ambapo TAKUKURU imetumia shilingi Bilioni 1 sawa na
takribani shilingi Milioni 143 kujenga kila ofisi kwa kutumia wataalamu wake
yenyewe na majengo yote yamekamilika.
Akizungumza
baada ya kuzindua jengo la NEC, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza NEC akianzia na
Mwenyekiti Mstaafu wa Tume hiyo Jaji
Mstaafu Damian Lubuva aliyeokoa shilingi Bilioni 12 katika matumizi ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambazo zilielekezwa kujenga jengo hilo na
Mwenyekiti wa sasa Jaji Mstaafu
Semistocles Kaijage pamoja na Chuo Kikuu
- Ardhi kwa kusimamia kwa karibu ujenzi wa ofisi hiyo ambayo ipo tayari kuanza
kutoa huduma.
Mhe.
Rais Magufuli amewapongeza viongozi wa vyama vya siasa walioshiriki katika
uzinduzi wa jengo hilo, na ametoa wito kwao, viongozi wengine na Watanzania
wote kwa ujumla kuendela kushirikiana katika ujenzi wa Taifa na kuhakikishia
wanashiriki mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu bila kusababisha fujo,
vurugu ama vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.
“Niwaombe
viongozi wenzangu wa vyama vya siasa, uchaguzi huu uwe wa kipekee, tufanye
kampeni zetu kwa upole, tufanye kampeni zetu kwa kumtanguliza Mungu, tufanye
kampeni zetu kwa kujua sisi ni Taifa la Tanzania, tufanye kampeni zetu kwa
kujenga umoja wa Taifa letu Tanzania, tunadi sera zetu na wananchi waweze
kutupima kutokana na sera zetu” amesema Mhe. Rais
Magufuli.
Kwa
upande wao viongozi wa vyama vya siasa wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano
kwa juhudi kubwa za ujenzi wa Taifa na wameahidi kufanya siasa za kistaarabu.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa wiki 2 kwa taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zinadaiwa
shilingi Bilioni 12 na Shirika la Ulinzi la Suma Guard kulipa fedha hizo baada
ya Mkuu wa JKT Mej. Jen. Charles Mbuge kudai kutolipwa kwa madai hayo kunakwamisha
shughuli za shirika hilo.
Akizungumza
katika sherehe za kuzindua Ofisi ya TAKUKURU Chamwino, Mhe. Rais Magufuli
ameipongeza Taasisi hiyo kwa juhudi kubwa za kukabiliana na rushwa, kuokoa mali
za umma zikiwemo fedha, mashamba,
magari, majengo na viwanja.
Hata
hivyo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na gharama kubwa
zilizotumiwa na TAKUKURU kujenga nyumba 7 kwa shilingi Bilioni 1 sawa na
wastani wa shilingi Milioni 143 kwa kila nyumba, kwani majengo yaliyojengwa
yanathamani ndogo ikilinganishwa na fedha zinazotajwa kutumia.
Amemtaka
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jen Mbungo kurekebisha dosari hizo na pia
ameishangaa TAKUKURU kwa kutaka kujenga ofisi ya taasisi hiyo katika Wilaya ya
Chato kwa kuwa tayari wilaya hiyo inalo jengo la TAKUKURU alilolikabidhi yeye
mwenyewe akiwa Waziri wa Ujenzi.
Mhe.
Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya
kujenga nyumba za watumishi wa TAKUKURU lakini amekataa ombi la fedha zote
shilingi Bilioni 1 ambazo taasisi hiyo imeomba kwa ajili ya kujenga uzio katika
ofisi mpya 7zilizojengwa wilayani, na kwamba Serikali itatoa fedha zisizozidi
shilingi Milioni 500.
Sherehe
za uzinduzi wa majengo ya NEC na TAKUKURU hapa Dodoma zimehudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya
Ulinzi na Usalama, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa Dini na viongozi wa
Mkoa wa Dodoma.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇