Juni mwaka jana kupitia Jarida la Forbes msanii kutokea Marekani Shawn Carter maarufu kama Jay Z alitangazwa kuwa msanii wa kwanza wa Hip Hop kuwa Bilionea, akiwa na utajiri wa US Dollar Bilioni 1.
Kwa mujibu wa Jarida hilo, vyanzo vya mapato vya Jay Z ni kuwa na hisa za Dollar Milioni 70 kwenye kampuni ya usafiri ya Uber, Dollar Milioni 70 kwenye masuala ya sanaa, Dollar Milioni 50 kwenye umiliki wa majumba ya kupangisha na muziki.
Pia umiliki wa Kampuni ya Roc Nation na Tidal inayouza nyimbo mtandaoni. Hivi ndivyo vimechochea kwa kiasi kikubwa utajiri wa Rapa huyo ambaye pia ni baba wa watoto watatu aliowapata na mkewe Beyonce.
Jay Z anafikia kiwango hicho kikubwa cha mafaikio kuwahi kutokea mara baada ya kuutumia muziki kwa takribani miaka 23. Ni safari iliyohitaji ushujaa, ubunifu na kujituma ili kuweza kufikia kilele chake.
Kwa hapa Tanzania msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Juma maarufu kama Diamond Platnumz anatajwa kwa msanii mwenye mafanikio zaidi.
Ingawa ni vigumu kutaja utajiri wake kwenye namba, ila ukubwa wa muziki wake, kampuni anazomiliki, matangazo, miradi mbalimbali ya kwake na ya kampuni nyingine ambayo amekuwa akifanya nazo kazi, inatosha kabisa kumtaja kama msanii aliyefanikiwa.
Huyu ni msanii anayemiliki lebo kubwa ya muziki Afrika Mashariki, Wasafi Classic Baby (WCB) ikiwa na wasanii watano (Rayvanny, Mbosso, Lava Lava, Zuchu na Queen Darleen) na wote wanafanya vizuri kimuziki na katika mauzo ya kile wanachozalisha.
Pia Diamond ana umiliki wa Wasafi Media na kampuni ya kutengeneza video za muziki, Zoom Extra. Huku akiweza kufanya kazi na kampuni kubwa duniani kama Coca Cola, Pepsi, Belaire, Universal Music Group na nyinginezo.
Hata hivyo wasanii wote wawili hadi kufikia kiwango hicho cha mafanikio haikuwa rahisi katika hali yoyote ile. Kuna magumu mengi waliyopitia ila walijivisha moyo wa ushupavu ili kuona ndoto zao zinatimia na kuweza kuwa msaada kwa wengine.
Jay Z alizaliwa Disemba 4, 1969 Brookly, Marekani, alipitia changomoto nyingi akiwa mdogo hasa pale Baba yake, Adnis Reeves alipoachana na mama yake, Gloria Carter.
Hata hivyo, Jay Z alikuja tena kukutana na Baba yake baada ya kufanikiwa kwenye muziki na kurejesha uhusiano wao kabla ya kufariki mwaka 2003.
Kutokana na ugumu wa maisha rapa huyo awali alijiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya na ndipo alipopata fedha za kurekodi albamu yake ya kwanza, Reasonable Doubt iliyotoka mwaka 1996 ikiwa na nyimbo zipatazo 15.
Kwa mujibu wa CBS News nyumba za Marcy Project ambazo familia masikini zilikuwa zikiishi ndani ya Brooklyn, Marekani alipozaliwa Jay Z zilikuwa kwenye maeneo hatari na yenye uhalifu sana.
Licha ya hayo yote Jay Z alipambana huku na kule hadi kufanya kazi kwenye mgahawa wa chakula na kufanikiwa hutoa albamu yake hiyo (Reasonable Doubt) ambayo kwenye wiki yake ya kwanza sokoni iliweza kuuza nakala 500,000, huku wimbo wake uitwao Ain't No Nigga (Like the One I Got) ukiingia kwenye chati za Billboard na ukawa mwanzo wa mafinikio yake.
Wakati Jay Z anafikisha umri wa miaka 20 ndipo Diamond Platnumz alizaliwa. Muimbaji huyo kutokea Tandale alizaliwa Oktoba 2, 1989 katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.
Yaliyotokea kati ya Adnis Reeves na mkewe, Gloria Carter yalibuka kwenye familia ya muimbaji huyo. Akiwa mdogo wazazi wake (Abdul Juma na Sanura Kassim) walitengana, huku yakiwepo madai kuwa alitelekezwa na baba yake bila msaada.
Baada ya kuhitimu elimu yake ya Secondary mwaka 2006, alijikita rasmi katika muziki ili kujaribu kutimiza ndoto zake. Ili kuhakikisha anafikia ndoto yake alifanya kazi mbalimbali ikiwepo kuuza mitumba, petrol station, kupiga picha na nyinginezo ili kupata fedha za kurekodi.
Mwaka 2009 alitoa wimbo uitwao Kamwambie ambao ndio ulimtangaza zaidi na kuweza kutoka kimuziki, baada hapo zilifuatia nyimbo nyingine kama Mbagala na Nitarejea. Mwaka 2010 alipata ziara (tour) ya kwanza kwenda Uingereza na ndio ukawa mwanzo wa mafanikio yake kimuziki.
Kwa sasa Diamond anautambua muziki kama biashara ya kwanza kuanza kumlipa vizuri na kumuwezesha kuwekeza katika miradi mingine kama nilivyotangulia kueleza hapo awali, hata kwa upande wa Jay Z.
UBAHILI WA JAY Z
Wasanii wengi duniani hutumia matamasha kama sehemu ya kukutana na mashabiki wao na kuwapatia burudani. Kukutana kwa makundi haya mawili sio bure bali kuna biashara inafanyika hapo katikati.
Juni 17, 2018 msanii Harmonize (kabla ya kujitoa WCB) aliandaa show yake aliyoipa jina la Kus Night katika uwanja wa Dar Live na kusindikizwa na wasanii wengine kama Ben Pol, Queen Darleen, Chin Bees, Nyandu Tozzy, Country Boy na Mrisho Mpoto.
Wakati Harmonize akielekea kumaliza kutumbuiza majira ya saa 10 alfajiri, Diamond aliibuka kwenye show hiyo akitokea ukumbi wa Next Door Arena ambapo Davido alikuwa na show yake pia siku hiyo.
Diamond alipanda jukwaani na kuanza kutumbuiza na Harmonize wimbo wao uitwao Bado, kisha ule wa Kwangaru. Ni Show iliyokuwa na msisimko wa aina yake kwa upande wa mashabiki na wasanii wenyewe.
Wakati wakitumbuiza wimbo, Bado, Harmonize alishindwa kujizuia na kuanza kulia. Sababu ya kufanya hivyo ni kwamba kwa mara ya kwanza alikutana na Diamond kwenye eneo hilo (Dar Live).
Pindi Diamond alipokaribia kumaliza shughuli yake jukwaani alivua tisheti aliyokuwa amevaa na kuwarushia mashabiki wake kitu kilicholeta purukushani kutokana kila mmoja alitamani kuondoka na nguo hiyo.
Kitendo cha kuwarushia mashabiki wake tisheti yake ndipo nikagundua Jay Z anaweza kuwa mbahili kuliko Diamond. Kivipi?, sikiliza nikuambie kitu.
Januari Mosi 2009 Jay Z alitumbuiza kwenye Tamasha la siku ya UKIMWI (World AIDS Day Concert) kwa kuhadhimisha miaka 30 ya mfuko wa Healthcare Foundation (AHF). Tamasha hili ni maalum na limekuwa na mfululizo wa matukio duniani kote kuwapa watu ufahamu kuhusu ugonjwa wa UKIMWI.
Kabla ya kupanda jukwaani Jay Z, muimbaji mwenye sauti ya aina yake, Alicia Keys alitangulia na kuanza kuwapa mashabiki burudani kwa kipiga kinanda pekee yake na kuimba mubashara (live).
Baada ya dakika 4:23 Jay Z alijumuika na Alicia Keys na kuanza kutumbuiza pamoja wimbo wao unaokwenda kwa jina la Empire State of Mind.
Mara baada ya Jay Z kumaliza kuimba vesi zake mbili za wimbo huo, alivua koti lake na kumkabidhi mtu aliyekuwa pale jukwaani, hakuwarushia mashabiki wake kama alivyofanya Diamond.
Kuna uwezekano aliyepokea koti hilo alikuwa mtu wake wa karibu au watu waliokuwa wanahusika na usalama pale jukwaani. Mara baada ya kumaliza kutazama tukio hilo, ghafla nikasikia sauti ndani yangu ikisema inawezekana Jay Z akawa bahili kuliko Diamond, kwani ingemgharimu nini kuwapa mashabiki hilo koti?.
Imeandikwa na Peter Akaro-July 2019.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇