WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema mitambo mipya ya uzalishaji wa vitambulisho vya taifa itaanza kufanya kazi hivi karibuni baada ya wataalamu kuwasili nchini.
Mitambo hiyo ya kisasa ambayo inauwezo wa kuzalisha vitambulisho 144,000 kwa siku, ilishafungwa muda mrefu ofisini za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), na ilipaswa iwe imenza kufanya kazi tangu mwezi Aprili, mwaka huu lakini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona ilichelewa kuanza kufanya kazi kutokana na watalaamu wa mitambo hiyo kutoka Ujerumani kushindwa kuja nchini.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya na Ipela, jimboni kwake Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, leo, baada ya kupokelewa kwa shangwe kwa kumpongeza kwa kuchaguliwa kuiongoza Wizara hiyo, Simbachawene amesema Watanzania waondoe shaka kwani kupatikana kwa mitambo hiyo ambayo sasa itafanya kazi muda wowote kuanzia sasa baada ya wataalamu kutoka nchini Ujerumani kuwasha mitambo hiyo.
“Naomba nitumie mkutano huu hapa Kijijini kuwatangazia Watanzania wote sasa tatizo la kukosa vitambulisho limeisha, hakuna atakayekosa kitambulisho, kila Mtanzania mwenye sifa atapewa, tulichelewa kuwasha mitambo kwasababu ya ugonjwa wa corona uliofanya wataalam washindwe kuja nchini,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “mitambo hiyo ni ya kisasa, na inauwezo wa kuzalisha vitambulisho 144,000 kwa siku, hivyo kwa idadi hiyo ndani ya miezi michache wale wote waliosajiliwa watapewa vitambulisho vyao.”
Aidha, Waziri Simbachawene alisema kutonakana na utendaji kazi wa Rais Dkt. John Magufuli, upinzani umekufa wenyewe hivyo uchaguzi ujao chama tawala kimejingea uwezo mkubwa wa ushindi wa kishindo.
“Rais wetu na Serikali ya Chama chetu Cha Mapinduzi kimefanya kazi iliyotukuka, na upinzani unakufa wenyewe, sasa hivi hakuna upinzani, mnasikia wanavyokatika wanarudi CCM kwasababu ya kishindo cha kazi kilichofanywa na Serikali ya Awamo ya Tano,” alisema Simbachawene.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejenga na inaendelea kujenga miradi mikubwa ambayo inaifanya Tanzania kuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi ndani na nje ya nchi.
“Tumenza ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ya nchi ambayo itakua michipa mikubwa ya kiuchumi, ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, na itakamilika, na pia amenunua ndege leo hii tunajivunia, na mradi wa umeme mkubwa ambao utawezesha kutumia umeme ndani na kuuza nje ya nchi,” alisema Simbachawene.
Pia alisema kwa upande wa ujenzi wa vituo vya afya, rais Magufuli amejenga vituo zaidi ya 450 nchini, hivyo kutokana na vituo hivyo watanzania watapata matibabu katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kikao hicho, Emmanuel Kagali, alimpongeza Waziri huyo kwa utendaji wake wa kazi ndani ya Jimbo la Kibakwe, kutokana na uwepo wa umeme katika vijiji vyote, ujenzi wa zanahani na barabara.
Pia alimuomba waziri huyo kuwasaidia kupata vitambulisho vya taifa, kwani idadi kubwa ya wananchi wa Kata ya Malolo hawajapata vitambulisho.
“Mheshimiwa Waziri nimefurahi sana kupata nafasi hii ya kukupongeza na pia kukupa moyo uendele kufanya kazi, na pia tumefurahi sana kuteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi, hivyo hatutakuangusha, nawe ni tegemeo letu katika maendelo ya jimbo letu,” alisema Kagali.
Naye Mkazi wa Kata ya Ipela jimboni humo, Jeremia Kibwingu alimuomba Waziri huyo kufikisha maombi ya wananchi wa Kibakwe, ya kuongezewa muda wa kuiongoza nchi Rais Magufuli kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuanzisha miradi mikubwa nchini.
“Naomba utufikishie ujumbe huu kwa Rais Magufuli, tutaka aongoze mpaka mwisho wa maisha yake, Rais huyu si wakawaida, Watanzania naomba muelewe, huyu anapaswa aiongoze nchi hii milele,” alisema Kibwingu.
Waziri Simbachawene anaendelea na ziara yake jimboni humo kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa chama pamoja na kukagua miradi ya maendeleo jimboni humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇