Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Godwin Mollel (Kushotoa) akiwa na Mwenyekiti wa wahitimu hao Dk. John Lupimo wakati wa hafla ya wahitimu wa mafunzo ya uboreshaji wa utoaji huduma za tiba asili iliyofanyika Jijini Dodoma, jana.
DODOMA, Tanzania
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amepiga marufuku tabia za Waganga wa tiba asili kupiga ramli chonganishi kwa lengo la kuwasaidia wananchi jambo ambalo ni kinyume na taratibu na miongozo ya Serikali.
Dk. Mollel ameyasema hayo leo, wakati wa hafla fupi ya wahitimu wa mafunzo ya uboreshaji wa utoaji huduma za tiba asili iliyohudhuriwa na baadhi ya wawakilishi kutoka Wizara ya Afya na baadhi ya wanafunzi wa taaluma ya uuguzi Mirembe Jijini Dodoma.
"Mambo ya ramli chonganishi, hayatakiwi kabisa katika nchi yetu, kitu tunachosisitiza ni tiba kwa kutumia mimea yetu ambayo Mungu alipomuumba mwanadamu aliumba akaweka mimea ya chakula, mimea ya matunda na mimea dawa, mimea dawa hiyo ndio tunataka wakaibue huko walete itusaidie kutibu watu wetu" alisema
Dkt. Mollel aliendelea kukemea tabia za baadhi ya Waganga kutumia Imani potofu katika taaluma ya tiba asili, huku akisisitiza kuwa, Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na Waganga wa tiba asili nchini wanaofuata taratibu na miongozo ya Wizara ya Afya katika kuwahudumia wananchi.
"Hatutegemei mtu atuambie jiwe litutawale, hizo Imani ambazo mtu anatawaliwa na jiwe, mtu anatawaliwa na ilizi, sisi ndio tulipewa tuvitawale vitu vyote na Mungu, kwahiyo sisi tunataka tiba ambayo sisi binadamu tutatawala vitu vyote na Imani potofu isisogelee kabisa kwenye utaratibu wetu wa tiba asili " alisema
Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwa, Serikali inawatambua na itaendelea kushirikiana na Wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala nchini kutokana na kuwa na mchango chanya katika kuwahudumia wananchi hasa katika kipindi hiki ambacho nchi na Dunia kwa ujumla imepitia changamoto ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo ya uboreshaji wa tiba asili, Mwenyekiti wa wahitimu Dkt. John Kabadi Lupimo mesema, wamepata mafanikio mengi ikiwemo, kufungua viwanda vidogo vya kuchakata dawa asili, basdhi kusajiliwa kama Waganga wa tiba asili, kusajili dawa mbali mbali na kujua Sheria ya Afya ya tiba asili.
Mbali na hayo, Dkt. John Kabadi Lupimo ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa mafunzo hayo, huku akisisitiza wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuikuza taaluma ya tiba asili ambayo inaendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi hususan katika kipindi hiki ambacho Dunia imekumbwa na mlipuko wa virusi vya Corona.
Your Ad Spot
Jun 14, 2020
SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UPIGAJI RAMLI CHONGANISHI
Tags
featured#
Kitaifa#
Share This
About Bashir Nkoromo
Kitaifa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇