KWA HALI ILIVYO CCM MNAPASWA KUWA NA FOMU MOJA TU YA MGOMBEA URAIS, TENA IWE YA JPM
Na Saidi Mwinshehe (Pichani)
LAZIMA tukubaliane kabisa na wewe ambaye umeamua kwa hiyari yako kusoma hiki ambacho nakiandika. Tukubaliane tu utasoma kuanzia mwanzo hadi mwisho.Ndio lazima iwe hivyo.
Ujue katika maisha haya kuna watu vichwa ngumu kidogo, yaani hata wewe fikiria unatumia muda mwingi kuandika kitu, alafu anatokea msomaji anasoma hapo juu na kisha anaacha.Sio vizuri jamani...tukubaliane tu leo tenga muda wako angalau usome hadi mwisho.
Kwa kuwa tumekubaliana sasa naomba nianze kwa kueleza hivi, huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu nchini kwetu Tanzania. Ni mwaka ambao tutachagua kiongozi kwa ngazi ya Diwani, Mbunge na nafasi ya Rais. Ni mwaka huu ambao tutashuhudia wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa nchini wakipita tena kuomba kura baada ya kufanya hivyo 2015.
Tunakumbuka katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 wagombea wa karibu vyama vyote walipita, wakajinadi na kisha tukawachagua.Uchaguzi ni uchaguzi tu na sote tunafahamu vema aina ya wanasiasa wetu.Tunakumbuka kwani katika uchaguzi mkuu uliopita, tuliwasikiliza na kisha tukawapa nafasi.
Hivyo tunarudi tena kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu 2020.Utakuwa uchaguzi wa aina yake katika nchi yetu.Watanzania wamebadilika sana. Watanzania wa leo wanajua kuchuja na kupata kiongozi sahihi.Ni uchaguzi ambao nina hakika watakaochaguliwa watakuwa wamepita kwenye mchujo wa hali ya juu.
Ndio! Watanzania safari hii hawatakuwa na mzaha.Wamechoka kuwa na madiwani ambao hawajui kutimiza wajibu wao.Wamechoka kuwa na wabunge vilaza, wabunge ambao wanawaza yao badala ya kuwaza ya wananchi.
Watanzania wamechoka kuwa na wabunge ambao kazi yao ni kupinga kila kitu.Wanapinga hata uwepo wa barabara za juu katika jiji la Dar es Salaam na ukiwauliza sababu ya kupinga kwao hawana majibu zaidi atakwambia anapinga kwasababu Serikali ya CCM itajidai.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ,Watanzania hawapo tayari kuendelea na wabunge ambao walipewa nafasi ya kwenda kuwawakilisha Bungeni lakini walipofika huko wakaanza kujiwakilisha wao na familia zao.Uchaguzi wa mwaka huu wagombea wa ngazi zote mjipange.Tena mjipange haswaaa.
Watanzania wanataka maendeleo tena kwa kasi , maendeleo ambayo yatakuwa chachu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.Kwa maana hiyo lazima tupate wabunge ambao watakwenda na kasi hiyo.
Bahati nzuri wabunge wengi ambao wanamaliza muda wao wa ubunge watakuja tena majimboni kuomba ridhaa ya kupewa tena nafasi.
Nieleze tu kama wewe ni Mbunge na unahitaji tena kurudi bungeni, uwe na sababu za msingi ambazo tutazielewa.Uwe na hoja ambazo tutajiridhisha wananchi kuwa unastahili kurudi.
Wale wabunge wenzangu na mimi ushauri wangu kwenu msijisumbue.Wale wabunge ambao kazi yao ni kuingia bungeni na kisha kusubiri posho ya kikao na mshahara safari hii hamna nafasi.
Hakuna anayeweza kuchagua mbunge kilaza. Wakazi gani? Niwaombe, tena sio kuwaomba niwatake tu wabunge ambao mnataka kurudi majimboni kwenu ni vema mkatenga muda na kisha mkajifikiria kama mnatosha au laa? Jipimeni maana wapiga kura tayari tumeshawapima.Oktoba 25 hatutaangalia jina la mgombea wala Chama anachotoka.
Tutachagua wachapakazi.Tunawajua vizuri.Hivi mimi ninayeishi Dar es Salaam nashindwaje kuwajua wabunge wangu.Ukweli wananchi wanajua uwezo wa kila mbunge na wanajua hata wale ambao wanataka kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo kwenye eneo la udiwani na ubunge ndilo ambalo angalau Watanzania watahitaji kuwa na muda wa kuchuja nani awe diwani, nani awe mbunge.Najua kwenye nafasi hizo wagombea watakuwa wengi na viwango tofauti vya maarifa, elimu, akili na uelewa.Ukweli ni kwamba Watanzania wanafahamu vilivyo sifa za diwani wanayemtaka, sifa za mbunge wanayemhitaji.
Ngoja nikunong'oneze hapa kidogo.Sogeza sikio maana sitaki aliyekuwa karibu asikie nachotaka kukwambia.Sogea tena.Iko hivi ndugu kwenye nafasi ya urais mwenzio sioni mwenye ubavu wa kupambana na Rais Dk.John Magufuli ambaye atasimama kwa niaba ya CCM.
Hebu jiulize hata wewe tu bila mwingine kujua.Nani unamuona anaweza kupambana na Dk. Magufuli kwenye uchaguzi Mkuu mwaka huu.Hakuna, kweli hakuna wa kupambana na Dk.Magufuli.
Hivi anayetaka kupambana na Rais Magufuli kwenye uchaguzi wa mwaka huu atakuwa na hoja gani. Anakwenda kuwaambia nini Watanzania? Hivi anayetaka kupambana na Rais Magufuli katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu atakuwa na sifa zipi ambazo zitashinda sifa alizonazo Dk.Magufuli.
Ukweli hakuna.Ndio hakuna.Nakwambia hakuna.Niamini mimi hakuna wa kupambana na Rais Magufuli. Kwa yanayofanywa na Rais Magufuli hivi sasa Watanzania wamekuwa na imani kubwa sana na kazi nzuri ambayo inafanywa na Rais pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza.
Kwa Dk. Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu hana sababu ya kutumia nguvu kubwa ya kujieleza.Hana sababu ya kujipigia debe. Hana sababu ya kutolala usingizi kisa uchaguzi Mkuu.Kazi ambazo amefanya kwenye nchi yetu zinatosha kabisa tena kwa asilimia 100 ya kuwa sababu ya kupita kiulaini kabisaa.
Rais Dk. Magufuli amefanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi. Sote tunaona yaliyofanywa na Rais Magufuli.Hata hapa sitataka kutumia muda mwingi kuelezea ambayo Rais ameyafanya.Hivi nani hajui ambayo yamefanyika ndani ya nchi yetu. Sitaki kuzungumzia elimu bure maana hata mtoto mdogo anajua hayo.
Sitaki kuzungumzia ujenzi wa Ikulu ya Dodoma, sitaki kuzungumzia ujenzi wa barabara za juu katika Jiji la Dar es Salaam, sitaki kuzungumzia ujenzi wa madaraja kwenye Ziwa Victoria, sitaki kuzungumzia ujenzi wa meli mpya na vivuko katika maziwa yanayotuzunguka nchini kwetu.
Rais Magufuli amefanya mambo makubwa ya maendeleo katika nchi yetu ndani ya kipindi kifupi.Ndio kuna mengi yamefanyika. Sitaki kuzungumzia ununuzi wa ndege mpya nane tena za kisasa.Sitaki kuzungumzia mabadiliko makubwa ambayo yamefanyika katika sekta mbalimbali na leo hii tunaona matunda yake.
Sipo hapa kwa ajili ya kuzungumzia ujenzi wa reli ya kisasa, sitaki kuzungumzia ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Nyerere kule Rufiji.Sitaki kuzungumzia namna ambavyo Rais Magufuli ameweka utaratibu mzuri wa Watanzania kunufaika na rasilimali za nchi yao.
Leo hii watanzania tumeona hata michanga ya madini kumbe ilikuwa na mabilioni ya fedha.Kwa mara ya kwanza tumepata fedha kwenye michanga ya madini (Makinikia). Mungu atupe nini tena.
Sioni wa kupambana na Rais Magufuli.Nikiri kwenye uchaguzi kila Mtanzania anayo haki ya kujitokeza na kugombea. Sitashangaa kuona watanzania wengine wakichukua fomu kwenye nafasi hiyo ya urais.Ni haki yao ingawa hawana nafasi ya kushinda.
Kwa kuwa kila Mtanzania anayo haki ya kugombea nafasi yoyote, nishauri kwa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu mwaka huu kwenye mchakato wenu ndani ya Chama hamna sababu ya kuwa na mafomu mengi ya kugawa kwa wanaotaka kugombea urais.
Fomu ya kugombea urais ndani ya CCM iwe moja tu, fomu hiyo tena iwe ya Rais Dk.John Magufuli. Nafahamu kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu , Rais anatakiwa kukaa kwenye urais kwa awamu mbili na kila awamu ina miaka mitano.
Dk. Magufuli ameshakaa kwa awamu ya kwanza na sasa anarudi tena kwa ajili ya awamu ya pili ambayo itakuwa ya miaka mitano mingine. Nafahamu ukubwa wa CCM na jinsi ambavyo wamekuwa na demokrasia pana katika mambo ya uchaguzi.
Katiba yao iko wazi kabisa, mwenye sifa anakaribishwa kuchukua fomu.Hata hivyo kwa mwaka huu sioni sababu ya CCM kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kuwa na mafomu mengi ya kugawa kwa wanaotaka kuwania nafasi hiyo ndani ya CCM.Fomu ya mgombea urais ndani ya CCM iwe moja, tena iwe ya Dk. Magufuli.
Kuna mambo ya kushangaza sana, hiki nilichoandika najua wapo ambao watakereka sana. Wapo watakaosema jamaa huyu anajipendekeza.
Wengine watasema nimetumwa.Hivi jamani kutoa maoni yako ni dhambi. Kama ni dhambi basi niko tayari kuipokea.Mungu aliyeniumba kwa mfano wake atanisamehe. Kwa Rais huyu tuliyenaye mwenye hofu ya Mungu na mwenye kumtanguliza Mungu kila wakati, sioni mahali ambapo nitahukumiwa kwa kueleza ukweli kuhusu Dk. Magufuli.
Tunakumbuka hapa kati kati Dunia ambavyo ilikuwa imekumbwa na taharuki baada ya kuwepo kwa janga la Corona. Ni Rais mmoja tu anaitwa Dk. John Magufuli kutoka Tanzania ndio amethibitisha anao uwezo wa kukabiliana na majanga madogo na makubwa.Tunamuhitaji Rais Magufuli tena .
Nihitimishe kwa kuwaomba CCM ni kweli huenda sina akili za kutosha za kueleza jambo.Huenda sijui cha kuzungumza kuhusu CCM na uchaguzi Mkuu lakini niombe safari hii kwenye CCM yenu muwe na fomu moja tu ya mgombea urais.Iwe ni fomu kwa ajili ya Rais Magufuli.Uliyesoma kuanzia kule juu hadi hapa chini nakushukuru kwa kutekeleza makubaliano yetu.
Basi isiwe tabu... tuwasiliane 0713833822
Your Ad Spot
Jun 14, 2020
HOJA MTAMBUKA YA SAID MWINSHEHE
Tags
featured#
makala#
Share This
About Bashir Nkoromo
makala
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇