Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia) akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi Bilioni 3, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe maalumu kwa ajili ya vikundi vya wakulima na wasindikaji wa zao la muhogo wilayani Handeni, mkoani Tanga. Wengine kwenye picha ni Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justin (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa Wakulima wa zao hilo nchini, Mwantum Mahiza, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Makufwe na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Aikansia Muro.
Akizungumza
katika mkutano na wakulima hao eneo la Mkata Wilaya ya Handeni, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert
Mponzi alisema mkopo huo wenye riba nafuu utawanufaisha wakulima 421 ambao
watakuwa katika makundi 43.
“Shilingi bilioni
3 ni fedha nyingi, hivyo mzitumie vizuri ili na wengine waweze kufaidika. Huu
ni uhamasishaji wa uwekezaji katika zao la muhogo ili kuwawezesha wakulima
kujiongezea kipato na wakati huo kuendana na soko la China,” alisema Mponzi.
Mkuu wa Wilaya
ya Handeni, Godwin Gondwe aliishukuru Benki ya NMB kwa mkopo huo huku akisema
katika kutatua
changamoto ya masoko ya zao hilo, kiwanda cha kusindika kinatarajiwa kuanza
kazi miezi michache ijayo na taratibu zinaendelea ili kuweza kulipata soko la
china.
Akielezea
harakati za Wilaya katika kuhamasisha zao la muhogo, Mwenyekiti wa Umoja wa
Wazalishaji na Wasindikaji wa Muhogo Tanzania (TACAPPA), Bi Mwantumu Mahiza
alisema zao la muhogo katika wilaya ya Handeni limekuwa la kibiashara kutokana
na usafirishwaji wa muhogo mbichi kwa wingi kwenda Dar es Salaam.
Kwa miaka kadhaa,
kilimo kimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania hasa katika
upatikanaji wa chakula, biashara ya mazao nje ya nchi, kusaidia upatiakaji wa
malighafi za viwanda vya ndani na kutoa ajira kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇