Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally akitangaza ruhusa kwa watangaza nia kujipitishapitisha kwa wanachama kuanzia Julai Mosi hadi Julai 14, 2020 |
Na Richard Mwaikenda
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ametoa ruhusa kwa watangaza nia ya kugombea udiwani na ubunge kupitia chama hicho, kujipitishapisha kwa wanachama kwa lengo la kujitambulisha.
Ruhusa hiyo ameitangaza muda mfupi baada ya kupokea fomu kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli ambaye amerejesha leo baada ya kumaliza kupata zaidi wadhamini milioni moja katika mikoa yote 32 nchini. Dk. Magufuli anaomba ridhaa ya chama hicho kupeperusha bendera ya kugombea urais Oktoba 2020.
Dk. Bashiru amesema kuanzia kesho Julai Mosi, watangaza nia wako huru kwenda hata kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuulizia taratibu za kuomba kugombea nafasi hizo.
Amesema Fursa hiyo ya kujitambulisha kwa wanachama itakoma Julai 14, 2020 watakapoanza kuchukua fomu za kuomba kugombea nafasi hizo.
Licha ya kutoa fursa hiyo, Dk. Bashiru alitoa angalizo kwa watangaza nia kuwa fursa hiyo wasije wakaigeuza kuwa kampeni, kwani wakati wa kampeni bado na atakaye kwenda kinyume atakumbana na mkono wa Kamati ya maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula.
Baada ya kutangaza hiyo viliibuka vigeregere na nderemo kutoka kwa wanachama waliofika kushuhudia mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli akirejesha fomu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇