Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna (kushoto) na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Ndogo na za Kati wa NMB - Filbert Mponzi (Kulia) wakiwa wameshika alama ya uzinduzi rasmi wa akaunti ya NMB Pamoja. Katikati ni Mteja wa NMB Bi. Zaina Mikidadi, kutoka kushoto ni Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB - Benedicto Baragomwa, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa wa Serikali wa NMB Alfred Shao na Kaimu Afisa Mkuu Rasilimali wa tu- Emmanuel Akonaay.
Benki ya NMB na kampuni ya Savings
at the Frontier (SatF) leo
wamezindua huduma mahsusi kwa vikundi vya kuweka na kukopa nchini. Kwa
ushirikiano huo, NMB na SatF zinakusudia kuwafikia zaidi ya vikundi 28,000 na
wanachama wake walio nje ya mfumo rasmi na kuwaunganisha kwenye huduma za kifedha.
Mfumo huo mpya utatoa nafasi kwa vikundi vya
kuweka na kukopa pamoja na wanachama wao kutumia huduma za kidijitali za NMB
zitakazowawezesha kufungua akaunti binafsi, kufungua akaunti za vikundi na
kuweza kuzihudumia kupitia simu ya mkononi. Njia hii itawafanya wakidhi
mahitaji ya wanachama bila kulazimika kukutana au kwenda tawi la benki na hivyo
kutunza fedha kwa njia salama na ya uhakika.
Mfumo huu ni maboresho ya huduma ya ‘NMB Pamoja
Account’ ambayo ni mahsusi kwa ajili ya Vyama vya Kuweka na Kukopa
Vijijini (VSLA), Vyama vya Kijamii vya
Akiba (SILC), Benki za Kijamii Vijijini (VICOBA), Vikundi vya Kijamii vya Akiba
(CBSG), Mashirika ya Kijamii (CBO), Makundi ya Familia na Marafiki na
kuyaunganisha na benki yenye mtandao mpana zaidi nchini.
Akizungumza kwenye
uzinduzi wa NMB Pamoja Account, Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna
alisema: “Lengo
letu ni kuziba pengo lililopo kati ya taasisi za fedha na makundi yasiyo rasmi
ya kuweka akiba na kukopa kwa kuyasogezea huduma za kibenki karibu yao. Huduma
hii ambayo ni nyongeza kwenye NMB Pamoja Account, ni nafuu, inapatikana kila mahali
na wakati wowote na ni rahisi kuitumia.”
Katika kuimarisha mkakati wa Benki ya NMB
kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi, NMB Pamoja Account ni huduma kamili
iliyounganishwa na Akaunti ya Chapchap inayowaruhusu wanachama wa kikundi
kuhamisha fedha kutoka akaunti ya chama kwenda kwa mwanachama bila gharama
yoyote, huku ikitoa urahisi na uwezo wa kutoa michango, kuangalia salio, kupata
taarifa fupi na kufungua akaunti ya kikundi kwa kutumia simu ya mkononi, kwa
kupiga *150*68# bila makato yoyote
ya gharama za uendeshaji ya kila mwezi, haya yote yakiambatana na riba nzuri
inayotolewa kwenye akaunti kwa mwaka.
“SatF inafurahi kuungana na Benki ya NMB ili kutoa
suluhu ya huduma za kifedha kwa vikundi. Tunaamini ushirikiano huu utasaidia kuvifikia
vikundi yenye wanachama walio nje ya mfumo rasmi kwenye huduma za kifedha
nchini. Hii inaenda sambamba na mpango wa Benki Kuu ya Tanzania kuongeza idadi
ya wananchi wanaotumia huduma za kifedha hususan kwa wanawake,” alisema Mwakilishi
kutoka SatF, Janet Hayes
Ushirikiano wa Benki ya NMB na kampuni ya SatF
utaongeza kasi ya ufikishaji wa huduma za kifedha kwa wananchi. Ni ushirikiano
unaokusudia kuhamasisha na kuongeza uwekezaji na ushiriki wa wadau wengine
katika sekta ya huduma za fedha. Wakati Benki ya NMB ikiongoza kwa huduma bora,
zilizo karibu na wananchi na zenye tija zaidi nchini, SatF inakuja na uzoefu wa
kimataifa wa kujenga misingi ya kuboresha uwakilishwaji wa wananchi walio nje
ya mifumo rasmi ya kifedha ili kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇