LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 16, 2020

BABA WA UZAO: RAIS DK. MAGUFULI HANA HISTORIA YA KUSHINDWA KATIKA UTENDAJI WAKE

TEGETA, Dar es Salaam
Kanisa Halisi la Mungu Baba lililopo Tegeta jijini Dar es Salaam, limesema, Rais Dk. John Magufuli, hana historia ya kushindwa katika utendaji wake kwa kuwa amebarikiwa na Mungu Baba, hivyo kila atakayemwinua na kumuombea mema kama lilivyofanya kanisa hilo atapata baraka tena za halali kabisa.

Hayo yamesemwa jana na Kiongozi wa Kanisa hilo anayejulikana  kwa jina la Baba wa Uzao, wakati wa kuhitimisha ibada ya siku tisa ya kumuomba Mungu amfiche Rais Dk. Magufuli waovu wasimdhuru ili aendelee kuitumikia Tanzania kwa hekima, maarifa na busara alizonazo.


Akiendesha ibada hiyo, Baba wa Uzao, alitumia vifungu mbalimbali vya maadiko matakatibu, katika kuelezea imani ya Kanisa hilo katika kuonyesha faida na thawabu waliyopata kwa ibada waliyofanya kumuombea Rais kwa Mungu.


Kwa kuwa tulifanikiwa kupata maelezo ya Baba wa Uzao yakiwa kamili katika maandishi, tunayaweka hapa kama yalivyo ili upate kuyasoma vema na kwa utimilivu;



⇩⇩⇩⇩⇩⇩⇩⇩

THAWABU YA KUMWINUA RAIS DKT. JOHN MAGUFULI KWA MALANGO (SIKU) TISA
Katika Mathayo 10:41(b) Kitabu kinasema kuwa “… ampokeaye Mwenye Haki atapata Thawabu ya Mwenye Haki.” Aidha, katika Mwanzo 12:3 Kitabu kinasema kuwa “Nami nitawabariki wanaokubariki naye akulaaniye nitamlaani.” Mantiki ya mistari hiyo haijawahi kubadilika tangu ilipoandikwa hadi leo hii.
(1)        Rais Dkt Magufuli, katika utendaji wake hana historia yakushindwa, hivyo amebarikiwa na MUNGU BABA. Kitabu kimesema kuwa ukimwinua aliyebarikiwa na wewe unabarikiwa na MUNGU BABA. Hivyo baraka tumepata tena za halali kabisa;

(2)        Rais Dkt Magufuli ni Mwenye Haki.  Utajuaje kama unayemuombea ni Mwenye Haki? Yeyote unayemwinua, falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho (Efeso 6:12) zikainuka, basi ujue huyo ni mwenye haki. Kwa nini falme na mamlaka hizo ziinuke unapomuombea huyo mwenye haki? Ni kwa kuwa alikuwa amegeuzwa fidia yao, wanachukia kwa kuwa unakuwa umewaondolea anayeteseka badala yao! Ili uamini kuwa Rais Dkt Magufuli ni Mwenye Haki, Mimi sikuwahi kuombea yeyote falme na Mamalaka katika ulimwengu wa roho zikainuka kinyume na mimi kama walivyoinuka safari hii nikiwa namwinua Rais Dkt Magufuli. Walivunja mpaka mahali ninaposimama kuhubiria wakidhani nimemficha hapo! Hiyo ni dhahiri kuwa Kiongozi huyu ni Mwenye Haki. Kwa mujibu wa kitabu, ukimwinua atendaye kwa Haki, na wewe unapewa Thawabu ya Haki na MUNGU BABA;
  
(3)        Rais Dkt Magufuli ni Mwaminifu kwa Ahadi zake mwenyewe (Luka 16:12).  Kituo hiki cha kuwa Mwaminifu, kwa kauli zako mwenyewe, hata Watumishi wa Aliyetuumba sote huwa hawana!  Yeye katika hili ni Mwalimu, maana tumeona aliyoahidi miaka mitano kwetu ameyatenda.  Hivyo, ukimwinua Mwaminifu unapata Thawabu ya kuwa na Uaminifu. MUNGU BABA amemtetea Rais Dkt Magufuli kwa sababu ya Uaminifu wake wa ile kauli aliyokuwa ameisema kwenye Hotuba zake kuwa “sitawaangusha.” Kweli hajatuangusha.
Kila mwenye Akili anakubaliana na jambo hilo kuwa hajaangusha Watanzania, hasa wale wasio na watetezi. Katika hali kama hiyo, ilikuwa ni lazima Uumbaji wote umtetee: Jua; Mwezi; Nyota; Bahari; Mito; Maziwa; Wadudu; Wanyama; Ndege; Miti; Mimea; Hali ya Hewa; na Watu pia wanamtetea kwa sababu ya kuwa Mwaminifu kwa kauli yake mwenyewe.

Tukirudi katika 2Nyakati 20:20-26, baada ya Mfalme Yehoshefati kumkimbilia MUNGU BABA, na kuagiza Taifa lake limwamini Nabii na MUNGU BABA, maadui wote wa lile Taifa waligeukiana na kukatana mapanga wao kwa wao.  Kwa upande wa Mfalme Yehoshefati na Wananchi wake, walikuwa na siku nne za kuokota nyara za maadui waliokuwa wamekuja kuwashambulia.

Hiki ndicho kilichotokea kwa Rais Dkt Magufuli na Watanzania kwa sababu ya kuishinda HOFU iliyoletwa na corona.  Sasa ni majira ya kuokota nyara za wale wote waliokuwa wamekuja kuishambulia Tanzania na Rais Dkt Magufuli.  Hii imekwishakuwa (Ufunuo 21:6).
           
(4)              Rais Dkt Magufuli anaishi moyo wake!  Nimewahi kusema jambo hili kuwa, katika majira zote saba, hakuna aliyewahi Kuishi Moyo!  Yaani, kuahidi na kutenda bila kujali mazingira uliyokutana nayo.
Amewahi kusema mara nyingi kuwa haogopi yeyote, ilimradi hamuonei.  Ni kweli ndivyo ilivyo.  Tabia ya aina hiyo huwa anayo MUNGU BABA peke yake, na yule anayekubali kumpokea MUNGU BABA. Waliotumwa wote katika: Ezekieli 28:15 (kerubi); Mwanzo 2:15 (Adamu); Kutoka 3:10 (Musa); 1Wafalme 17:1 (Eliya Mtishibi); Matendo 10:38 (Yesu); Yohana 9:7 (Adamu wa Pili); na Isaya 33:6(Miaka1000); hawakufanikiwa Kuishi Moyo maana katika majira yao ilikuwa bado siyo rahisi Kuishi Moyo, hata kama walikuwa wametumwa na MUNGU BABA.
Rais Dkt Magufuli yeye, kwa mujibu wa yale tunayoyaona akitenda; amefanikiwa Kuishi Moyo.  Hili siyo mimi peke yangu ambaye nimeliona. Chuo Kikuu cha Dodoma, wanakubaliana nami kwa ile PhD waliyompatia ya kubadilisha Jamii ndani ya Miaka Minne (4) peke yake.
Vitabu vya Development Studies vinasema, angalao Miaka Kumi (10) unaweza kuonyesha dalili za kubadilisha fikra za Jamii.  Yeye Rais Dkt Magufuli, imemchukua Miaka Minne tu kubadilisha Jamii ya watu karibu milioni sitini kwa sababu ya Kuishi Moyo. Wasomi wa falsafa, Saikolojia, Theolojia na Sayansi Jamii, wanajua kuwa hii ni zaidi ya ufahamu wa kawaida ulioandikwa ‘‘(It is living beyond revelation)”.
Ndiyo maana, ukimuombea Rais Dkt Magufuli kwa jina la Mwana utaishia kulaumu, maana hutapata Thawabu. Kwa hiyo, katika malango haya tisa, tumepata Thawabu ya Kumwinua Rais aliyebarikiwa. Ukimbariki aliyebarikiwa Kitabu kinasema na wewe utabarikiwa na MUNGU BABA. 
 
Hitimisho
Thawabu kubwa ambayo tumeipata katika kumwinua Rais Dkt Magufuli; wote tunaotenda kwa Haki ni kutokuwa fidia ya waovu tena. Hii ilikuwa ni tabia ya dunia na ulimwengu kuwa kila anayetenda kwa Haki awe fidia yao. Aidha, kila anayetenda kwa Haki, katika majira zote alikuwa anaishia kuumizwa kwa sababu ya mazuri aliyotenda, badala ya kufurahia. Matokea ya haya malango (siku) tisa, tuliyomwinua Mhe. Rais Dkt Magufuli, ni utendaji wa ule msemo wa chema hakidumu, kutosikika tena popote.  Pia, ule msemo kuwa tenda wema uende zako, MUNGU BABA ameufuta kabisa. Imekwishakuwa (Ufunuo 21:6).

1 comment:

  1. Tanzania Taifa Baba chanzo halisi cha amani ya mataifa yote mabara yote Maana MUNGU BABA ameshukia hapa na anaishi ndani yaanaetenda kwa haki

    ReplyDelete

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages