Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiongea wakati wa kuzindua mpango huo.
Serikali imezindua mpango maalumu wa kutoa elimu ya afya kwa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na kuwapo kwa ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Corona ikiwa ni mwendelezo wa kuwafikia watu wengi katika ngazi ya mtaa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizundua mpango wa elimu ya afya kwa umma kwa siku 20 ambao utaongozwa na vikundi vya kijamii kwa kushirikiana na Red Cross chini ya Wizara ya Afya.
Waziri Ummy amesema lengo la kuzindua mpango huo ni kukata mnyororo wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona Kati ya mtu na mtu kwa kutumia vikundi vya kijamii ambavyo vitaelimisha na kutoa taarifa sahihi kwa Jamii kuhusu ugonjwa wa Corona.
“Vikundi hivi vya kijamii, vitashirikiana na Wizara ya Afya, Red Cross na UNICEF kutoa elimu ya afya kwa umma.
Katika mpango huo Magari 18 yatatumika kwa siku 20 na yatakwenda katika maeneo ya masoko, stendi za mabasi na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri amefafanua kuwa siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, vikundi vya kijamii vitakwenda katika maeneo ya nyumba za ibada kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kutoa elimu ya afya kutokana na kuwapo kwa ongezeko la ugonjwa wa Covid-19.
“Niwatoe hofu Watanzania, tutashinda hii vita endapo kila mmoja katika Jamii atazingatia maelekezo ya Wataalamu wa Afya,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri amesema mbali ya Elimu ya afya kutolewa katika Mkoa wa Dar es Salaam, pia vikundi vya kijamii vitakwenda katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza na Arusha kwa ajili ya kutoa elimu ya afya kwa umma kuhusu kujikinga na maambukizi ya ugonjwa Corona.
“Serikali inawashukuru Watanzania kuhusu suala la kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, wameelewa, wamepokea hili vizuri sana, hata katika ngazi ya Kijiji nje ya nyumba wameweka ndoo ya maji na sabuni, kwa hili tunawashukuru Sana Watanzania na tunawatia moyo wa kuendelea kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni,” amesema Waziri.
Waziri amewasisitiza Watanzania kuepuka mikusanyiko na misongamano ili kukabiliana na ugonjwa huo Kama walivyofanya kwenye hatua ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Elimua ya Afya kwa Umma wa Wizara ya Afya, Dkt. Ammaberg Kasangala amesema atahakikisha elimu kwa Jamii inatekelezwa ili kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona nchini.
“Nitashirikiana na Red Cross na wenzangu wa kitengo cha elimu ya afya kwa umma ili kuhakikisha Mipango ya utoaji wa elimu kwa wananchi inatekelezeka,” amesema Dkt. Kasangala.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇