LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 9, 2020

WAWEKA HAZINA WATAKAOSHINDWA KUFIKIA MALENGO YA UKUSANYAJI MAPATO KUKIONA CHA MOTO


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe Selemani Jafo ameagiza Wekahazina ambao Halmashauri zao hazijafikia malengo waliyojiwekea kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa Fedha watolewe kwenye nafasi zao kwani watakua wameshindwa kutimiza jukumu lao la msingi lililopelekea kupewa cheo hicho.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai – Disemba, 2019) kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Jafo amesema Mamlaka ya Wekahazina iko chini yake hivyo kwa yeyote atakayeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji ataondolewa na kuwekwa na watu wengine wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kufikia malengo yaliyowekwa katika ukusanyaji wa mapato.

Amesema Wakurugenzi wa halmashauri ambazo hazitafikia malengo atapeleka mapendekezo kwa Mamlaka inayohusika ili iweze kuwachukulia hatua stahiki kwa kushindwa kukusanya mapato inavyotakiwa na kurudisha nyuma jitihada za Serikali za kuongeza mapato.

Akizungumzia ukusanyaji wa Mapato hayo Waziri Jafo amesema kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 Halmashauri zilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 765.48 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na kipindi cha nusu mwaka (Julai hadi Desemba, 2019) Halmashauri zimekusanya Jumla ya Shilingi bilioni 356.81 ambayo ni asilimia 47 ya makisio ya mwaka.

Akifafanua taarifa za mapato ya vyanzo vya ndani katika kipindi cha Julai - Desemba, 2019 umeonesha kuwepo kwa ongezeko la mapato yaliyokusanywa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 56.7 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha Julai - Desemba, 2018 sawa na ongezeko la asilimia 19. 

“Uchambuzi unaonesha kuwa Halmashauri 63 kati ya Halmashauri 185 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 50 na zaidi ya makisio kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 na halmashauri mia ishirini na mbili (122) zimekusanya mapato ya ndani chini ya asilimia 50 ya makisio ya mwaka.
Halmashauri hukusanya mapato mengi au kidogo kwenye vyanzo tofauti kulingana na hali halisi ya shughuli za kiuchumi za kila Halmashauri hivyo, ongezeko hilo limetokana na sababu mbalimbali ikiwemo ushuru wa zao la Korosho katika Halmashauri za Mikoa ya Mtwara na Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma” Amesema Jafo.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miezi sita (Julai – Desemba, 2019), Halmashauri za Wilaya za Tunduru na Kibondo zimekusanya mapato kwa asilimia 104 ya makisio ya mwaka 2019/2020.

Pia Waziri Jafo amezitaka Halmashauri zote zilizokusanya zaidi ya asilimia 100 hadi Desemba, 2019 na zile ambazo zimejitathmini na kuona upo uwezekano wa kuzidi asilimia 100 ya bajeti za mapato ya ndani ifikapo Juni, 2020 zinaelekezwa kufanya mapitio ya Bajeti kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 ili ziweze kuongeza Bajeti za mapato na matumizi ya fedha hizo.

Jafo amesema katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Bilioni 29.75 na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekusanya mapato kidogo kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Milioni 186.1.

Akifafanua Ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri Kimkoa kwa Kuzingatia Asilimia ya Makusanyo amesema Mkoa wa Geita umefanya vizuri ambapo umekusanya wastani wa asilimia 63 ya makisio ya Halmashauri za Mkoa huo.

Aidha, Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Tanga ambao umekusanya wastani wa asilimia 36 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo.

Pia Waziri Jafo ameweka wazi Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa Kuzingatia Wingi wa Mapato kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 83.86 na Mkoa wa mwisho katika wingi wa ukusanyaji wa mapato ni Mkoa wa Katavi ambao umekusanya Shilingi bilioni 4.68.

Akifafanua Ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri kwa Kuzingatia aina ya Halmashauri kwa Kigezo cha asilimia ya makusanyo ukilinganisha na makisio Waziri Jafo amesema kwa upande wa Majiji Jiji la Dar es Salaam limeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 71 ya makisio yake na halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya kwa asilimia 41 ya makisio yake ya mwaka.

Upande wa Manispaa, Ilemela imeongoza kundi hilo kwa kukusanya asilimia 75 ya makisio yake na Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya kwa asilimia 26 ya makisio yake.

“ Katika Halmashauri za Miji, Mji wa Njombe umeongoza kwa kukusanya kwa asilimia 88 ya makisio yake ambapo Halmashauri ya Mji wa Babati imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 30 tu” Amesema Jafo.

Aidha, kwa kundi la Halmashauri za Wilaya amesema Wilaya za Tunduru na Kibondo zimeongoza kwa kukusanya asilimia 104 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa Fedha 2019/20 wakati Halmashauri za Mafia, Ukerewe na Gairo zimekuwa za mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 18 ya makisio.

Waziri Jafo aliongeza kuwa kwa upande wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa Kuzingatia Aina za Halmashauri kwa Kigezo cha Wingi wa Makusanyo Jiji la Dodoma limeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 29.75 na Jiji la Dar es Salaam limekuwa la mwisho kwa kukusanya Shilingi bilioni 6.03.

“Halmashauri za Manispaa, Ilala imeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 29.13 na Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 694.93," Amesema Jafo.

Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa mapato katika Halmashauri za Miji ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 4.64. Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 459.44” alisema Jafo.

Kwa upande wa Halmashauri za Wilaya, Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi kwa Halmashauri za Wilaya ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 3.89 na Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya Shilingi Milioni 186.08.

Waziri Jafo amezitaka Halmashauri zote kuendelea kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki na kudhibiti ukusanyaji wa fedha na mbichi na ameweka wazi kuwa Taarifa ya mwisho ya kota ya nne ya ukusanyaji wa mapato ya ndani sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ataitoa tarehe 18.06.2020 kabla ya Bunge kuvunjwa hivyo kila mtu ahakikishe anatekeleza jukumu hili kwa ufanisi ili kufukia malengo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akizungumza na wandishi wa habari kuhusiana na taarifa ya ukusanyaji wa mapato kwa robot ya mwaka.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akiwa kwenye mkutano wake na wanahabari jijini Dodoma leo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages